Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira,Vijana na watu wenye ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema serikali itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) katika kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi kwa kushughulikia masualaya wafanyakazi nchini
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo tarehe 7 Januari 2018, jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na viongozi hao wa TUCTA, walipokutana kwa ajili ya kujadiliana na kushauriana juu ya mazingira bora na wezeshi ya wafanyakazi, sekta ya kazi na ajira nchini .
“Hatuwezi kupata tija na ufanisi katika sekta ya kazi bila vyama vya wafanyakazi kushughulikia malalamiko na manunguniko ya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi hasa katika mikataba ya ajira na stahiki zao kwa mujibu wa sheria .TUCTA msipo simamia haya hata serikali tutashindwa kutimiza wajibu wetu kikamilifu. Serikali itaendelea kushughulikia masuala ya wafanyakazi na sekta ya kazi kwa kuzingatia miongozo, kanuni na sheria za kazi na ajira katika kutafuta suluhu ya masuala ya kazi” alisema Mhagama.
Mhagama aliwahakikishia TUCTA kuwa serikali itayashughulikia madai yote ya wafanyakazi ambayo yanazingatia sheria. Aidha Mhagama aliwataka TUCTA kuvitaka vyama vya wafanyakazi kufanya vikao na wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi na wawapatie elimu juu ya masuala ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya tafsiri sahihi ya sheria za kazi tulizonazo nchini.
Kwa upande wake Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamghokya ameishukuru serikali kwa ushirikiano wanaoupata toka serikalini kupitia majadiliano ambayo yamesaidia migogoro ya wafanyakazi kupungua katika maeneo ya kazi. ushirikiano huo umekuwa ni mhimili mkubwa kati ya serikali, waajiri na wafanyakazi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi utawala bora, George Mkuchika, Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazina Ajira), Anthony Mavunde na Katibu Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa na Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira) Erick Shitindi.
Msingi wa serkali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) kukutana kwa majadiliano na mashauriano unatokana na nchi ya Tanzania kusaini mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), ukiwemo mkataba namba 98 wa mwaka 1949,ndio uliweka mazingira hayo ya serikali,waajiri na wafanyakazi kukutana ili kuweka dhana ya kuaminiana na kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi na ajira.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.