Wednesday, April 25, 2018

WAZIRI MHAGAMA: USALAMA MAHALI PA KAZI KUCHOCHEA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Nchi Ofisi (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimishi ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Dunani wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Bungeni Dodoma Aprili 25, 2018.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda akieleza jambo wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari uliohusu maandalizi ya maadhimishi ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Dunani Bungeni Dodoma, Aprili 25, 2018.

Baadhi wa waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano wake uliohusu maandalizi ya maadhimishi ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi uliofanyika Bungeni Dodoma Aprili 25, 2018.
NA.MWANDISHI WETU
Serikali imesema kuwa usalama mahali pa kazi ni kichocheo cha ujenzi wa uchumi wa Viwanda hapa nchini ikiwa ni moja ya juhudi za Serikali kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa  mkutano na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa dhamira ya Serikali Kujenga uchumi wa Viwanda itatekelezeka kwa ufanisi kutokana na juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanakuwa na mazingira salama yakufanyia kazi kote nchini.
“Serikali haiwezi kutekeleza dhana ya Ujenzi wa uchumi wa Viwanda pasipo usalama mahala pa kazi ndio maana inaweka mkazo katika kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi katika maeneo yote hapa nchini yanakuwa salama ndio maana OSHA imekuwa ikiendelea kusimamia vyema jukumu hili.” Alisisitiza Mhe. Mhagama
Akifafanua Mhe. Mhagama amesema kuwa suala la usalama mahala pa kazi ni jukumu la kila mmoja  na si, la Serikali peke yake kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Aliongeza kuwa watu 10,000 katika sekta isiyo rasmi wamepatiwa mafunzo kuhusu usalama na afya mahala pa kazi hali inayochochea maendeleo  kwa kuongeza tija na kupunguza ajali zinazoweza kuepukika au kuzuilika.
Tutaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa watu wenye ulemavu hasa viziwi zaidi ya 300 watapatiwa mafunzo kuhusu  Usalama mahala pa kazi na afya ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupitia OSHA kushirikisha makundi yote katika kukuza na kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa tuzo kwa waajiri wanaozingatia Afya na Usalama  mahali pa kazi kwa wafanyakazi wao hali inayochochea ukuaji wa uchumi.
Siku ya Afya na Usalama mahali pa kazi itaadhimishwa Kitaifa Mkoani Iringa tarehe 28/ 4/ 2018 ambapo Tanzania itaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo.
Pia Waziri Mhagama alitoa wito kwa waajiri wote kujisajili OSHA ili watambulike na waweze kutoa taarifa zitakazosaidia kuboresha hali na mazingira ya kufanyia kazi.
AWALI
OSHA ni Taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia sheria Na. 5 ya Mwaka 2003 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Taasisi hii inawajibu wa kufanya kaguzi za kiusalama sehemu zote za kazi Tanzania Bara, kufanya Tafiti, Mafunzo na kuweka takwimu zote za usajili pamoja na taarifa za ajali, Magonjwa na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya sehemu za kazi na vile vile ndio Mshauri wa Serikali wa masuala yanayohusiana na Usalama na Afya sehemu za kazi . Taasisi hii imekuwa ikifanikisha program mbalimbali ikiwemo kutoa elimu.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.