1.
Mheshimiwa Naibu
Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa
zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa
lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019. Aidha,
naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa
Bunge kwa mwaka 2018/2019.
2.
Mheshimiwa Naibu
Spika, awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya
njema na kutuwezesha kukutana tena kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji
wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa
mwaka 2018/2019.
3.
Mheshimiwa Naibu
Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kutokana na fikra na uongozi wao makini katika ujenzi wa Taifa letu.
Ni dhahiri kuwa juhudi zao katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango
ya Serikali, zinaleta manufaa makubwa kwa wananchi.
4.
Mheshimiwa Naibu
Spika, hivi
karibuni tumewapata Waheshimiwa Wabunge wapya kutokana na chaguzi ndogo
zilizofanyika. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mhe. Dkt. Godwin Mollel
(Mbunge wa Jimbo la Siha) na Mhe. Maulid Mtulia (Mbunge wa Jimbo la Kinondoni)
kwa kuchaguliwa na kisha kuapishwa na Bunge lako Tukufu ili waendelee
kuwatumikia wananchi wa majimbo yao na Watanzania kwa ujumla. Ni matumaini
yangu kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili
waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
5.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Bunge lako lilimpoteza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini,
Mheshimiwa Leonidas T. Gama. Vilevile, baadhi ya waheshimiwa Wabunge na
wananchi tunaowawakilisha walipata misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. Aidha,
kulitokea maafa na majanga ambayo yalisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa
mali. Pia, kumekuwepo na ajali za barabarani ikiwemo ajali mbaya iliyotokea
tarehe 24 Machi 2018 wilayani Mkuranga na kugharimu maisha ya Watanzania 26.
Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema waliopata majeraha. Aidha, ninatoa
pole kwa ndugu jamaa na marafiki kwa misiba iliyotokea. Mwenyezi Mungu
azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!
6.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutoa
salamu za pole kwa Waheshimiwa Wabunge wenzetu waliopata majeraha mbalimbali
kufuatia ajali ya gari tarehe 29 Machi 2018 walipokuwa wakitoka Dodoma kuelekea
Dar es Salaam. Wabunge hao ni Mheshimiwa Haji Ameir Haji (Mbunge wa
Makunduchi), Mheshimiwa Khamis Ali Vuai (Mbunge wa Mkwajuni), Mheshimiwa
Bhagwanji Maganlal Meisuria (Mbunge wa Chwaka), Mheshimiwa Makame Mashaka Foum
(Mbunge wa Kijini) na Mheshimiwa Juma Othman Hija (Mbunge wa Tumbatu). Tuzidi
kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya wenzetu hawa ili waweze tena kuungana
nasi kutekeleza majukumu yao katika Bunge lako hili Tukufu.
7.
Mheshimiwa Naibu
Spika, napenda
kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya
kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za
Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, niwashukuru
sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na
Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa
Biharamulo Magharibi; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na
Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Kamati hizo zimetoa
mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha
ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Aidha, nichukue nafasi hii
kuwapongeza sana Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za
Bunge kwa kuaminika na kuchaguliwa kuongoza Kamati hizo.
8.
Mheshimiwa Naibu
Spika, ninawashukuru
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya,
Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano
wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru wafanyakazi
wote wa Serikali na Taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yao na kukamilisha
kuandaa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/2019.
9.
Mheshimiwa Naibu
Spika, kwa
namna ya pekee kabisa, napenda kumshukuru Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mbunge
wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Mhe. Anthony Peter Mavunde,
Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Mhe.
Stella Alex Ikupa, Mbunge Viti Maalumu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu; Makatibu Wakuu Bibi Maimuna K. Tarishi, Profesa Faustin R. Kamuzora, na
Bwana Eric F. Shitindi, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipatia
katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
10.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia
kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi marafiki, taasisi na mashirika
ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa
kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na
kuiletea nchi maendeleo.
11.
Mheshimiwa Naibu
Spika, ninawashukuru
wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono na niwapongeze kwa
kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni kwa ufanisi, wakati mimi Mbunge wao
nikitekeleza majukumu ya kusimamia utendaji wa Serikali. Kipekee, ninamshukuru
mke wangu mpendwa, Mary na familia yangu kwa upendo wao, uvumilivu na maombi
yao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru sana.
MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI
12.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo wa kazi za
Serikali kwa mwaka 2018/2019 ni kuboresha utendaji wa Serikali na kuwezesha
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/2019. Aidha, Mpango na Bajeti
umezingatia azma ya Serikali ya kufikia malengo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo
wa Miaka Mitano ambao umepangwa kuhitimishwa mwaka 2020/2021 ukiwa na dhima kuu
ya “kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya
watu”. Vilevile, Mpango huu umezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015
na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa
mwaka 2015 pamoja na utekelezaji wa hotuba yake wakati akizindua Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015.
MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
13.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa tunaingia
kwenye Bunge la tatu la bajeti kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatuwezi kumsahau
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutimiza ndoto na matarajio ya
Watanzania kwa kujenga nchi yenye uchumi imara. Katika kipindi hiki,
tumeshuhudia mambo makubwa aliyoyafanya yakiwemo kujenga ari ya uzalendo kwa
kuilinda na kuisemea nchi yetu bila woga; kudumisha amani, utulivu na
mshikamano; kuimarisha ulinzi na usalama kwa kukomesha vitendo vya mauaji
yaliyojitokeza Mwanza, Amboni (Tanga), Mkuranga, Kibiti, Rufiji (Pwani) pamoja
na kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
14.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingine
alizofanya ni kujenga nidhamu ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe;
kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma; kuanzisha
mahakama ya rushwa na ufisadi; kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi zikiwemo
za madini na maliasili. Aidha, amefufua Shirika la Ndege la Tanzania;
ameanzisha ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR); ameendeleza
ujenzi wa barabara zikiwemo barabara za juu (flyovers) na amenunua meli na
vivuko. Kazi nyingine ni ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme kama vile Stiegler’s
Gorge; usambazaji umeme hadi vijijini na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima
(Uganda) hadi Tanga (Tanzania).
15.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine
makubwa aliyoyafanya ni kuimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa,
vifaa na vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya; kutoa elimumsingi
bila malipo kwa watoto wa Kitanzania; ujenzi wa miradi ya maji; na kuimarisha
bei za mazao ya kibiashara. Aidha, Mheshimiwa Rais ametimiza ndoto ya Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya
Serikali mjini Dodoma. Haya ni baadhi tu ya mambo aliyoyafanya na yatatolewa
ufafanuzi wa kutosha kupitia wizara za kisekta.
HALI YA UCHUMI
16.
Mheshimiwa
Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo
uchumi wake unakua kwa kasi. Viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika
kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8,
kiwango ambacho kilikuwa juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki ambapo Uchumi wa Kenya ulikuwa kwa asilimia 6.1, Rwanda
asilimia 6.0, Uganda asilimia 5.5, Burundi asilimia 0.0 na Sudan Kusini
asilimia hasi 6.3. Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) zinaonesha kwamba katika kipindi cha kuanzia Januari hadi
Desemba 2017, pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.1
ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016. Shughuli zilizochangia ukuaji huo kwa viwango vikubwa ni pamoja na uchimbaji wa
madini na mawe asilimia 17.5; huduma za usambazaji maji safi na majitaka
asilimia 16.7; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 16.6; habari na
mawasiliano asilimia 14.7 na ujenzi asilimia 14.1. Aidha, sekta ya kilimo, misitu na uvuvi ilikua
kwa asilimia 3.6, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu mwaka 2010.
17.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia Desemba
2017, deni la Taifa lilikuwa Dola za Marekani milioni 25,419.6. Viashiria vyote
vya deni vinaonesha kuwa deni linahimilika kwani, thamani ya deni la nje kwa
Pato la Taifa ni asilimia 19.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani
ya deni la nje kwa uuzaji wa bidhaa nje ni asilimia 81.8 ikilinganishwa na
ukomo wa asilimia 150; na thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia
117.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 200. Kwa kuzingatia vigezo hivyo,
bado tuna uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ili kugharamia shughuli
za maendeleo. Kwa ujumla, viashiria vya kuimarika kwa uchumi, vinatoa mwelekeo
mzuri wa kufikiwa kwa malengo yetu ya kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa
na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
SIASA
18.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka 26 sasa
imepita tangu mfumo wa siasa wa vyama vingi uanzishwe nchini. Katika kipindi
hicho tumeona ushiriki wa Watanzania katika siasa ukiendelea kuongezeka na
uhuru wa kujiunga na vyama vya siasa kwa kuridhishwa na itikadi za vyama hivyo
pia ukiongezeka. Ni vyema tukajenga utamaduni wa kuheshimu wananchi pale
wanapoamua kujiunga na chama cha siasa watakachokipenda. Jukumu letu kama viongozi wa siasa ni kunadi
sera zetu kwa wananchi na kuhamasisha ujenzi wa demokrasia inayolenga kuleta
maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote pamoja na kudumisha
amani, utulivu, mshikamano na kujenga umoja wa kitaifa.
19.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, kumefanyika chaguzi ndogo za Wabunge katika majimbo matano na
Madiwani katika kata 59 kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu
mbalimbali. Chaguzi hizi zilisimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ufanisi.
Katika chaguzi ndogo za ubunge zilizofanyika katika majimbo ya
Songea Mjini, Singida Kaskazini, Longido, Kinondoni na Siha; Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kilishinda majimbo yote. Vilevile, katika uchaguzi wa Madiwani, CCM
ilishinda katika kata 58 na CHADEMA ilishinda katika Kata moja. Nichukue nafasi
hii kuvipongeza vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo na
kipekee nakipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata ushindi mkubwa na wa
kishindo katika maeneo mengi.
20.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Msajili imeendelea kuhakikisha kuwa demokrasia ya vyama vingi
vya siasa inaimarika. Katika mwaka 2017/2018, Ofisi ya Msajili iliratibu kikao
cha Baraza la Vyama vya Siasa ambacho pamoja na kufanya uchaguzi wa Viongozi wa
Kamati za Baraza hilo, kilijadili mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria Mpya ya
Vyama vya Siasa na marekebisho ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa.
Vilevile, Ofisi ya Msajili inaendelea kukusanya maoni ya wadau kwa lengo la
kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992
pamoja na kanuni zake.
MUUNGANO
21.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, kumefanyika vikao mbalimbali
vya kisekta vya ushirikiano kati ya Wizara za SMT na SMZ kwa lengo la
kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano wetu. Baadhi ya changamoto
hizo ni masuala ya fedha, biashara na ajira katika taasisi za Muungano. Katika kipindi hicho, viongozi na wataalamu wa pande
mbili za Muungano walikutana kwa ajili ya kujadili hoja zinazohusu sekta za
fedha, biashara, viwanda na uwekezaji, ujenzi na uchukuzi, maliasili na utalii.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
22.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea
kutekeleza zoezi la kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Tangu
utekelezaji wa zoezi hilo uanze mwezi Septemba 2016, jumla ya watumishi wa umma
3,829 kutoka Wizara na taasisi mbalimbali wamehamia Dodoma katika awamu ya
kwanza na ya pili, na awamu ya tatu inaendelea. Katika kufanikisha azma hii,
Serikali inaboresha miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, umeme,
mifumo ya maji safi na maji taka, ofisi, makazi na kuimarisha huduma za elimu,
afya, mawasiliano na michezo.
23.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga
kuijenga Dodoma kuwa mji bora na wa kisasa unaoendana na mahitaji na mifumo ya
miji bora duniani. Ili kufikia azma hiyo, Serikali inashirikiana na wadau
ikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kuujenga Mji wa Dodoma. Napenda
kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambaye mara tu baada ya kuhamia Dodoma amezindua “Kampeni
ya Kijanisha Dodoma” inayolenga kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Kampeni hiyo
inahusisha kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya ukanda wa kijani.
24.
Mheshimiwa Naibu Spika, niupongeze Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa
kufungua ofisi zake za muda mjini Dodoma mwezi Desemba 2017. Natoa wito kwa
mashirika mengine ya kimataifa na mabalozi waige mfano huu wa kuhamishia ofisi
zao Dodoma. Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Mashirika ya
Kimataifa na wanadiplomasia katika kurahisisha maandalizi yao ya kuhamia
Dodoma. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kuwekeza
Dodoma kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji ikizingatiwa nafasi yake
kijiografia inayosaidia mikoa yote hapa nchini kufikika kwa urahisi na haraka
zaidi. Nichukue fursa hii kuipongeza Kamati inayoratibu zoezi la Serikali
kuhamia Dodoma inayosimamiwa na Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Bibi Maimuna K. Tarishi, Katibu Mkuu (Waziri
Mkuu na Bunge).
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
25.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza
mipango mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na wananchi kujiletea maendeleo.
Moja ya jitihada zilizofanywa na Serikali ni kuanzisha mifuko ya
uwezeshaji ambayo inatoa mikopo kupitia vikundi vya vijana, wanawake, wazee,
watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum.
26.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulidhamini mikopo yenye
thamani ya takriban shilingi bilioni 13 kwa SACCOS 58, VICOBA 172 na kampuni
mbili. Aidha, Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi umetoa mikopo ya
Shilingi bilioni 62.8 kwa wajasiriamali 85,982. Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake
ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 kwa vikundi 5,169 katika
Halmashauri 153. Mfuko wa Kilimo Kwanza ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 62.7 kwa miradi 189 katika wilaya 76.
27.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Mfuko wa Taifa wa
Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 783 ambapo
vijana 840 kutoka Halmashauri mbalimbali walinufaika. Aidha, katika kipindi
hicho, Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia asilimia 5 ya mapato yao ya ndani
zilitenga shilingi bilioni 15 ikiwa ni mikopo ya masharti nafuu kwa vijana.
Vilevile, Halmashauri 48 zilitenga ekari 217,882 kwa ajili ya shughuli za
uzalishaji mali kwa vijana nchini. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea
kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
28.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali
inaratibu jumla ya mifuko na programu 31 za uwezeshaji ambazo usimamizi wake
upo katika taasisi mbalimbali za Serikali na za binafsi. Kila mfuko au programu
imeanzishwa kwa sheria yake au taratibu maalumu zinazosimamia utendaji wa mfuko
husika. Serikali imeona kuna umuhimu wa kupunguza idadi ya mifuko kwa lengo la
kuongeza ufanisi wa utendaji wake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Hivyo,
tumeanza kufanya mapitio ya utendaji wa mifuko hiyo kwa nia ya kuunganisha
baadhi ya mifuko yenye majukumu yanayofanana. Hatua hiyo, itasaidia kuwa na
mifuko michache yenye tija ambayo itaharakisha kufikiwa kwa malengo
yaliyokusudiwa.
Ukuzaji Ujuzi
29.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukuza
ujuzi wa nguvukazi tuliyonayo ni miongoni mwa ajenda muhimu ya kisera katika
kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Serikali inatoa msukumo wa kipekee
kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi nchini kwa lengo la kuwapatia ujuzi na stadi
za kazi wananchi hasa kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili
waweze kumudu ushindani katika soko la ajira na hivyo kuwawezesha kushiriki
katika ujenzi wa uchumi jumuishi wa viwanda.
30.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa
na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2014, unaonesha kuwa
asilimia 79.9 ya nguvukazi ni yenye kiwango cha chini cha ujuzi, asilimia 16.6
kiwango cha kati wakati ni asilimia 3.6 tu ndiyo yenye kiwango cha juu. Ili
kufikia uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria kubadili mwenendo huo kwa
kuhakikisha nguvukazi yenye kiwango cha juu cha ujuzi inafika asilimia 12 na
kiwango cha kati asilimia 34. Kwa msingi huo, Serikali inaendelea kutekeleza
programu ya kukuza ujuzi pamoja na programu nyingine ili kukidhi matakwa ya
uchumi wa viwanda.
31.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, jumla ya vijana 7,817 wamewezeshwa kupata ujuzi kupitia programu
hiyo. Kati yao, vijana 220 walipata mafunzo kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar
es Salaam na vijana 3,440 kupitia Taasisi ya Don Bosco. Mafunzo waliyopewa ni
katika fani za ufundi stadi wa ushonaji nguo, useremala, uashi, TEHAMA,
uchongaji wa vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, vyuma, terazo, vigae na ujuzi
wa kutengeneza bidhaa za ngozi. Aidha, kupitia VETA vijana 3,989 walipata
mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi kwa fani za uashi,
useremala, ufundi magari, upishi na uhudumu katika hoteli.
32.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya vitendo
yalitolewa pia kwa wahitimu 168 kupitia viwanda na kampuni mbalimbali katika
fani ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi. Vilevile, Serikali imeandaa na kuzindua
Mwongozo wa Kitaifa wa Uanagenzi na Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo ya Vitendo
kwa wahitimu kwa lengo la kuweka utaratibu wa utoaji wa mafunzo hayo kwa wadau
wote ili waweze kuajirika. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa mafunzo ya
ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 10,500 katika fani mbalimbali.
Ninazishukuru kampuni binafsi ambazo zinaendelea kutoa nafasi za mafunzo ya
vitendo kwa wahitimu wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi
katika nyanja mbalimbali ili tuweze kukuza ujuzi wa rasilimali watu ya taifa.
Ajira
33.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imeendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini. Hadi
kufikia Februari 2018, jumla ya ajira 482,601 katika sekta rasmi zimezalishwa
nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 345,547, sawa na asilimia 72 zimezalishwa
kutokana na shughuli za umma ikiwemo miradi ya maendeleo ya Serikali kama vile
ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na
miradi ya TASAF; na ajira 137,054 sawa na asilimia 28 zimezalishwa katika sekta
binafsi.
34.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaandaa
mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa wanashiriki na kunufaika
na miradi mikubwa ya kitaifa. Vikao kati ya Serikali na wafanyabiashara
vimefanyika ili kuwaandaa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo. Katika
mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuratibu masuala ya ukuzaji ajira nchini
ikiwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ili iendane na
mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Masuala ya Kazi na Wafanyakazi
35.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha
kwamba kunakuwepo tija, ufanisi na mahusiano mema mahali pa kazi, Serikali
inasimamia Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria Na.7 ya Taasisi
za Kazi. Sheria hizo zinalenga kuhakikisha haki na wajibu kwa mfanyakazi na
mwajiri vinapatikana. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imehimiza kuanzishwa kwa
mabaraza ya wafanyakazi, kufunga mikataba ya hali bora pamoja na kufanya kaguzi
mbalimbali mahali pa kazi ili kujiridhisha kuwa viwango vya kazi
vinazingatiwa.
36.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha
Julai 2017 hadi Februari 2018, jumla ya kaguzi 102,860 zimefanyika katika
maeneo mbalimbali ya kazi nchi nzima. Sambamba na kaguzi hizo, elimu kuhusu
sheria za kazi, wajibu na majukumu ya wajumbe wa baraza kwa waajiri na
wafanyakazi kupitia vyama vyao ilitolewa. Jumla ya waajiri 640 na wafanyakazi
3,624 walipatiwa elimu hiyo. Aidha,
mabaraza 441 ya wafanyakazi yaliundwa na 46
yalihuishwa upya.
37.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ilipokea na kusajili migogoro ya kikazi 6,113
ambapo migogoro 4,816 sawa na asilimia 79, ilitatuliwa kwa
njia ya usuluhishi na uamuzi. Katika mwaka
2017/2018, utafiti kuhusu sekta na vyanzo vinavyoongoza kwa migogoro ya kikazi
umefanyika. Sekta ya usafirishaji iliongoza kwa kuwa na migogoro 547; ulinzi
binafsi 512; viwanda 434; elimu 420; huduma za hoteli 399 na taasisi za umma
321. Aidha, aina ya vyanzo vinavyoongoza kusababisha migogoro ya kazi ni
kuachishwa kazi bila kufuata taratibu sahihi; madai mbalimbali na kuvunjwa kwa
mikataba isivyokuwa halali. Utafiti huu utaisaidia Serikali kwa kushirikiana na
waajiri na vyama vya wafanyakazi kuweka mipango ya pamoja na kuzuia migogoro
sehemu za kazi kabla haijatokea.
38.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa waajiri na
wafanyakazi na kuendeleza mijadala yenye tija ili kupunguza migogoro mahali pa
kazi. Serikali pia itaendelea
kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi, kusajili,
kusuluhisha na kuamua migogoro katika maeneo ya kazi. Aidha, itashirikiana kwa
karibu na vyama vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya mara
kwa mara kwa lengo la kuongeza tija na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
SEKTA BINAFSI
39.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua
mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa letu. Kwa kutambua
umuhimu huo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji
nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuboresha miundombinu wezeshi kama vile
reli, barabara, umeme na maji. Hatua nyingine ni kupunguza na kufuta baadhi ya
kodi zinazoathiri ufanisi wa sekta binafsi; kuhuisha sera na sheria pamoja na
kuimarisha majadiliano yenye manufaa baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018, jumla ya miradi 175 yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.4 ilisajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji
nchini (TIC). Miradi hiyo inatarajiwa kutoa fursa za ajira 20,178.
40.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea
kuimarisha majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa nia ya
kuondoa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta binafsi. Katika mwaka
2017/2018, Serikali imefanya mikutano minne na wawakilishi wa sekta binafsi.
Miongoni mwa mikutano hiyo, ni ule uliofanyika tarehe 19 Machi, 2018 ambao
uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi za
umma kukutana na wawakilishi wa sekta binafsi ili kutatua kwa haraka changamoto
zilizobainishwa katika mkutano huo. Serikali inawahakikishia wafanyabiashara na
sekta binafsi kwamba inawathamini na itaendelea kushirikiana nao kutatua
changamoto zinazowakabili ili kujenga uchumi wa viwanda.
SEKTA YA HIFADHI YA JAMII
41.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea
kusimamia utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii
ikiwemo kutungwa kwa sheria inayounganisha Mifuko ya Pensheni ya PSPF, LAPF,
PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma unaojulikana
kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma. Sheria hiyo pia, imefanya
marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii ili kuufanya
Mfuko huo uhudumie wafanyakazi wa sekta binafsi pamoja na kutoa huduma ya
hifadhi ya jamii katika sekta isiyo rasmi.
42.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutungwa kwa sheria hiyo kutasaidia kuondoa
changamoto iliyotokana na wingi wa mifuko ya hifadhi ya jamii inayolipa mafao
yanayotofautiana kwa watumishi wa umma wenye masharti ya kazi yanayofanana.
Vilevile, sheria hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya baadhi ya mifuko
kutokuwa endelevu kutokana na idadi ndogo ya wanachama, ushindani usiokuwa na
tija na gharama kubwa za uendeshaji. Sheria imeweka kipindi cha mpito cha miezi
sita kitakachoanza tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo. Lengo ni
kuwezesha maandalizi ya utekelezaji wake kufanyika pasipo kuathiri shughuli na
huduma muhimu kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa ikiwa ni pamoja na kupokea
mafao yao.
Napenda kuwataarifu Watanzania kupitia Bunge
hili kwamba tayari Mheshimiwa Rais amesaini muswada huo kuwa sheria ya nchi.
Utekelezaji wa sheria hii utaboresha mafao ya wafanyakazi.
43.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itakamilisha
mapitio ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 na hivyo kuandaa
Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ambayo itakuwa jumuishi. Lengo la Serikali ni
kuwezesha huduma za hifadhi ya jamii kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan
waliopo katika sekta isiyo rasmi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
44.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uratibu na
utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kwa
kuhakikisha upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika
kutimiza azma hiyo, Serikali imeunda kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa
12 ya Geita, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Singida, Rukwa,
Shinyanga, Simiyu na Tabora. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha
kuwa mikoa mingine nayo inaunda kamati hizo.
45.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa
kushirikiana na wadau imeendelea kutoa vifaa saidizi kwa jamii ya watu wenye
ulemavu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila utegemezi. Baadhi ya vifaa
vilivyotolewa ni viti mwendo 240, bajaji 6, magongo ya kutembelea 350, kofia
pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum kwa wenye uoni hafifu 70, shime sikio
20, vyerehani 8, vifaa vya kukuzia maandishi 65, mafuta maalum ya kukinga ngozi
dhidi ya mionzi ya jua 35, viti maalum vya kuogea 50 na nyenzo nyingine za
kujimudu. Vilevile, Serikali imeendelea kuviboresha vyuo vya watu wenye ulemavu
vya Yombo, Dar es Salaam na Sabasaba, Singida. Serikali pia inakamilisha
uanzishwaji wa kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu kutoka vyuo mbalimbali
nchini ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa za ajira zinazopatikana kwenye
sekta binafsi na umma.
46.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto kwa kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa
watoa huduma katika vituo vinavyolea watoto wenye ulemavu wa ngozi kwenye mikoa
ya Shinyanga, Mara, Tabora, Simiyu, Tanga, Mwanza, Kigoma na Singida. Lengo la
utoaji elimu ni kuwajengea uelewa na kuwapa mbinu watoa huduma waendelee
kuimarisha ulinzi kwa watoto pamoja na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii waone
umuhimu wa kulea watoto hao kwenye ngazi ya familia.
47.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni
pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Watu wenye
Ulemavu. Serikali pia itaendelea na zoezi la kuanzisha madawati ya watu wenye
ulemavu na kuhamasisha sekta binafsi na umma kuweka
miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Serikali itahimiza waajiri
wote nchini kuajiri watu wenye ulemavu wenye sifa kwenye nafasi mbalimbali na
pia kutoa matangazo ya ajira yanayohamasisha wenye ulemavu kuomba nafasi
zinazotangazwa. Vilevile, itahamasisha na kuelimisha jamii kuhusu mahitaji
maalum ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwaheshimu, kuwatambua, kuwathamini na
kutowanyanyapaa.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
Hali ya Upatikanaji wa Chakula
48.
Mheshimiwa Naibu Spika,
hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula
nchini imeendelea kuimarika. Katika msimu wa 2016/2017 na 2017/2018, uzalishaji
ulifikia tani milioni 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.3 ya
chakula kwa kipindi hicho. Kutokana na uzalishaji huo, nchi ilikuwa na ziada ya
tani milioni 2.6 za mazao yote ya chakula na hivyo, kujitosheleza kwa asilimia
120. Aidha, hadi kufikia Januari, 2018 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
ulikuwa umenunua jumla ya tani 26,038 za mahindi na akiba ya chakula iliyopo
ghalani ni tani 92,074.
Mazao ya Biashara na Kuimarisha Ushirika
49.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeamua
kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni
chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima,
kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea
kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni. Uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji
wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto
kadhaa. Miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi
ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu
mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza vema wajibu wao, wizi,
dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia kilimo cha
kitaalamu.
50.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine za
kushuka uzalishaji wa mazao hayo ni huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti,
ukosefu wa pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama
vikuu vya ushirika. Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba ulipungua kutoka tani
456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande wa
tumbaku, uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624
mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 mwaka 2015/2016.
51.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua
hatua za kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia
chaguzi za vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532
na kufanya kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika zinaendelea. Pamoja na hatua
hiyo, Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja kupitia
maafisa kilimo na Bodi za Mazao. Hatua nyingine ni kufuta baadhi ya tozo
zilizokuwa kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba
mauzo yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.
52.
Mheshimiwa Naibu Spika,
kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusimamia
mazao makuu ya biashara, tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa kuongezeka
uzalishaji wake. Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa mazao ya asili
ya biashara ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la mavuno
ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la uzalishaji wa mazao ya
biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo wa bei za mazao hayo
hususan korosho na kahawa.
53.
Mheshimiwa Naibu Spika,
katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuimarisha
vyama vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha
mazao ya kimkakati ya biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa
stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya
ushirika kwa njia ya minada. Pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo
limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa
yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora
wakinufaika na bei ya juu zaidi.
Pembejeo za Kilimo
54.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali imerahisisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima
baada ya kuanza kuagiza mbolea kwa kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa
Pamoja. Hadi kufikia mwezi Machi 2018, upatikanaji wa mbolea hapa nchini
ulikuwa tani 310,674, sawa na asilimia 64 ya mahitaji ya tani 485,000 kwa
mwaka. Kwa upande wa mbegu bora za kilimo, upatikanaji umefikia tani 51,700,
sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji ya tani 60,000 kwa mwaka. Kwa mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea kuboresha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja
ili uendelee kuleta ufanisi na tija iliyokusudiwa.
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
55.
Mheshimiwa Naibu Spika,
katika mwaka 2017/2018, Serikali imekamilisha maandalizi
ya awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo. Programu hiyo itatekelezwa
kwa miaka 10 katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaweka mkazo katika kutekeleza malengo makuu ya programu
hiyo. Msukumo utawekwa kwenye kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ya
kipaumbele kwa kuimarisha upatikanaji na matumizi ya pembejeo na zana za
kilimo; kuimarisha huduma za ugani; kuimarisha kilimo cha umwagiliaji;
kuimarisha huduma za utafiti wa mazao ya kilimo na kuhakikisha matokeo ya
utafiti yanawafikia wakulima; kuweka na kusimamia mipango ya matumizi bora ya
ardhi ya kilimo; kuimarisha usindikaji wa mazao ya kilimo na kuwezesha
upatikanaji wa masoko ya mazao.
56.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tumeamua kwa dhati kusimamia kwa karibu sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri
Watanzania wengi. Tutahakikisha kuwa mkulima ananufaika na kilimo chake kwa
kuwafikishia wakulima pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu kwa wakati; kuimarisha
miundombinu ya kilimo na kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika. Pia,
Serikali itatoa kipaumbele katika kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda kwa
lengo la kuongeza thamani na faida kwenye shughuli za kilimo.
Mifugo
57.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba mifugo bora na ya kisasa ni fursa kubwa ya
kupunguza umaskini hapa nchini. Hata hivyo, ili mifugo hiyo iweze kuleta
matokeo makubwa, hususan upatikanaji wa soko la uhakika ndani na nje ya nchi,
hapana budi mifugo itambuliwe bayana. Kutokana na mahitaji hayo ya utambuzi,
Serikali inatekeleza zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya chapa ya moto
ambapo hadi Februari 2018, ng’ombe 16,408,022 wamepigwa chapa. Idadi hiyo ni
sawa na asilimia 94.4 ya ng’ombe 17,390,090 waliotegemewa kupigwa chapa. Zoezi
hili ni endelevu na ninawaomba wadau watoe ushirikiano wa kutosha kwa Serikali ili
kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Maliasili na Utalii
58.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu
wa sekta ya maliasili na utalii katika ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza
ajira, Serikali inaongeza juhudi za kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo misitu,
wanyamapori, malikale, ufugaji nyuki, uvuvi, pamoja na kuhakikisha rasilimali
hizo zinanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Serikali pia imechukua hatua za kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato
katika sekta hizo, kupambana na ujangili, kuzuia upotevu wa mazao ya misitu na
kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi.
Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeanza mapitio ya Sera za Taifa za
Utalii, Misitu na Ufugaji Nyuki ili ziendane na mazingira ya sasa na kuimarisha
zaidi ulinzi wa rasilimali hizo.
59.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya
utalii, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2017 imeongezeka hadi kufikia
watalii milioni 1.33 ikilinganishwa na watalii milioni 1.28 mwaka 2016. Pia, mapato yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka
2017 ikilinganishwa na Dola za Marekani
bilioni 2.13 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia sita. Takwimu hizo
zinabainisha kwamba, sekta ya utalii ina fursa kubwa ya kulipatia taifa fedha
za kigeni na kuzalisha ajira kwa wingi.
Tutaendelea kuimarisha sekta hii kwa kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha
miundombinu ya maeneo ya utalii pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani, utalii
wa mambo ya kale na kihistoria katika miji ya zamani ikiwemo Bagamoyo, Kilwa na
Mikindani.
Viwanda
60.
Mheshimiwa Naibu
Spika, sote
tunatambua kwamba kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi wa
Taifa unaotegemea viwanda. Hadi kufikia mwezi Februari 2018, viwanda vipya
3,306 vimeanzishwa. Aidha, Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa
kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri; kuendeleza na
kuboresha miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji.
Pia, kuhuisha sera, sheria na kanuni
pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua
stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo. Vilevile, Mikoa na
Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda.
61.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya hifadhi ya
jamii inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo, pamoja
na miradi mingine, NSSF na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza
wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari mkoani Morogoro. Lengo la
Mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme MW 40. Mradi huo
unatekelezwa katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere lenye ukubwa wa hekta
63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo
Dakawa.
Hadi sasa ekari
2,000 za mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la Mkulazi na ekari 1,100
zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya kwanza ya ufungaji
wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo mwezi Desemba, 2018 ili uzalishaji
uanze mwaka 2019. Miradi hii itakapokamilika itazalisha zaidi ya ajira 100,000.
Aidha, tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu mwezi Juni, 2017 ajira za moja
kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja
24,000 ikijumuisha wakulima wadogo wa mbegu na kilimo cha nje
zimezalishwa.
62.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2018/2019, Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo,
uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya
biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda. Vilevile, Serikali
itaweka msisitizo katika kubuni mikakati ya uanzishwaji na uendelezaji wa
viwanda vidogo na vya kati.
Madini
63.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha usimamizi katika sekta ya
madini ili kuiwezesha sekta hiyo kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi,
kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja
na kukusanya taarifa za uzalishaji wa madini, kuimarisha ukaguzi wa uzalishaji
na mauzo kwenye migodi mikubwa na midogo na kufuatilia ukusanyaji wa maduhuli.
Zoezi la ukaguzi limewezesha kukamatwa kwa madini yaliyokuwa yakitoroshwa yenye
thamani ya Dola za Marekani takriban 898,523 na shilingi milioni 557.
64.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Februari,
2018 maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kutoka sekta ya madini yalifikia
shilingi bilioni 180.4. Pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yametokana na
usimamizi makini katika sekta ya madini na uamuzi wa Serikali kufungua soko la Tanzanite nchini. Aidha, Serikali
imeimarisha soko la madini nchini kwa kuhakikisha kuwa madini yanauzwa kwa
ushindani.
65.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba, tarehe 20 Septemba 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alielekeza ujengwe
ukuta katika eneo linalozunguka mgodi wa Tanzanite
uliopo Mererani ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi
wa ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 24.5 umekamilika. Nitumie fursa hii,
kuwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
kwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
66.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea
kujenga uwezo wa wazawa ili washiriki kikamilifu katika sekta ya madini.
Uwezeshaji huo utakwenda pamoja na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu
teknolojia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kwa lengo la kupunguza athari za
mazingira na maafa katika maeneo ya migodi. Aidha, Serikali itakamilisha
taratibu za kumpata mwekezaji
atakayejenga mitambo ya kuchenjua madini nchini.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
67.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu
wa rasilimali ya ardhi kama kitovu cha uzalishaji mali, Serikali inachuka hatua
madhubuti za kuiendeleza. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza Mpango Kabambe wa
Majiji, Manispaa na Miji; udhibiti wa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na
uimarishaji wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi nchini. Napenda
kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba Mipango Kabambe ya Manispaa za Iringa, Singida
na Mji wa Kibaha imekamilika na mipango mingine 20 ipo katika hatua mbalimbali
za uandaaji. Hadi sasa, michoro 1,110 ya
mipango miji iliidhinishwa kati ya 1,148 iliyopokelewa kutoka Halmashauri za
miji mbalimbali.
Natoa wito kwa
wananchi wote nchini wanapofanya shughuli za maendeleo kuzingatia mipango
kabambe inayoandaliwa na mamlaka za upangaji miji.
68.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua
hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto ya migogoro ya ardhi miongoni mwa
watumiaji ikiwemo migogoro ya mipaka ya vijiji, wakulima na wafugaji,
wanavijiji na hifadhi na mapori ya akiba. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni
kuunda timu ya kisekta ya kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo imetembelea
Mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Morogoro na Tabora na kufanya majadiliano na
wadau 1,106. Hatua mbalimbali za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinaendelea
kuchukuliwa.
Nishati
69.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali
imechukua hatua thabiti kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa kutosha na wa
uhakika kwa ajili ya uchumi wa viwanda.
Hatua zilizochukuliwa zinalenga kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya
usafirishaji wa umeme na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na
mijini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa
ya Kinyerezi I (MW 185), Kinyerezi II (MW 240) na Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto
Rufiji (Stiegler’s Gorge) utakaozalisha MW 2,100.
70.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imepanua na kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme kwa
kutekeleza miradi mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na: Mradi wa Rufiji -
Chalinze - Dodoma wenye msongo wa kV 400; Mradi wa Singida – Arusha – Namanga
wenye msongo wa kV 400; na Mradi wa Makambako – Songea wenye msongo wa kV 220. Utekelezaji wa miradi hii umeongeza hali ya
upatikanaji umeme nchini kufikia asilimia 67.5. Aidha, uunganishaji umeme kwa
watumiaji umefikia asilimia 49.5.
71.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) ambao umepangwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji
7,873 ambavyo havijapata umeme nchini. Kati ya hivyo, vijiji 7,697 vimepangwa
kupatiwa umeme wa Gridi ya Taifa na vijiji 176 pamoja na visiwa vitapatiwa
umeme nje ya gridi kwani ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaongeza fedha
za mfuko wa REA ili kuhakikisha vijiji vilivyosalia pamoja na taasisi zinazotoa
huduma za kijamii vijijini zinapata umeme. Serikali pia, itaendeleza miradi ya
kuunganisha Gridi ya Taifa na gridi za nchi jirani za Zambia, Kenya, Burundi na
Rwanda.
Bomba la Mafuta (Hoima – Tanga)
72.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 5 Agosti
2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa
Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni waliweka Jiwe la
Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
bandari ya Tanga. Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi
huo kwa upande wa Uganda ulifanyika katika eneo la Hoima tarehe 11 Novemba,
2017. Bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litakuwa na urefu wa kilometa
1,445 ambapo kilometa 1,115 zitajengwa Tanzania. Mradi huo utakuwa na manufaa
kwa wananchi wa pande zote mbili ambapo ajira takriban 10,000 zitazalishwa
wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1,000 wakati wa uendeshaji wake.
Barabara
73.
Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali
inaendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini. Katika kipindi cha Julai 2017
hadi Februari 2018, ujenzi wa Km. 776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami
umekamilika na Km. 1,760 zinaendelea kujengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa
Km. 17,054 zimekarabatiwa katika kipindi hicho. Vilevile, ujenzi wa madaraja ya
Kilombero na Kavuu umekamilika na ujenzi wa madaraja ya Sibiti, Mto Mara,
Lukuledi, Ruhuhu, Momba na Mlalakuwa unaendelea. Madaraja mengine 996 katika
maeneo mbalimbali nchini yamekarabatiwa.
74.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea
na jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Hadi kufikia Februari 2018, ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la TAZARA
ulifikia asilimia 70 na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo
(Ubungo Interchange) umeanza. Aidha, maandalizi ya Awamu ya Pili hadi ya Nne ya
Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka yanaendelea. Katika
mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kujenga kilometa 597 za barabara kuu na za
mikoa kwa kiwango cha lami na kilometa 72 za kiwango cha lami zitakarabatiwa.
Barabara za Vijijini na Mijini
75.
Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali imeanzisha Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency – TARURA)
kwa lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji na kuongeza kasi ya wananchi
kujiletea maendeleo. TARURA
imepewa jukumu la kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara zenye
urefu wa kilometa 108,946.2 za vijijini na mijini. Katika mwaka
2017/2018, TARURA imesimamia matengenezo
ya barabara zenye urefu wa kilomita 4,183.3, madaraja 35, makalavati makubwa 43
na madogo 364 na drift nne. Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa TARURA
kuwaelimisha wananchi, viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuhusu majukumu na mfumo wa utendaji kazi wake.
Reli
76.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) itakayokuwa na urefu wa Km. 1,219. Hadi
sasa, ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye Km. 300
umeanza na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2019. Aidha, tarehe 14 Machi 2018,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha kutoka Morogoro hadi
Makutupora chenye urefu wa kilomita 422. Ujenzi wa reli hii utasaidia kukuza
sekta nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda, madini, utalii pamoja na
kutoa fursa nyingi za ajira. Utekelezaji wa mradi huu unakadiriwa kutoa ajira
30,000 za moja kwa moja na nyingine 600,000 zisizo za moja kwa moja.
Bandari
77.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya
Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa majini. Uboreshaji huo utaanza na Gati Na.
1 – 7; kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia
meli; kuimarisha mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga gati maalumu la
kuhudumia meli za magari. Vilevile, Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua ofisi
katika baadhi ya nchi jirani kwa lengo la kuongeza urahisi wa kutoa huduma.
Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea na uboreshaji wa bandari za Dar es
Salaam, Tanga na Mtwara. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa dirisha moja la
forodha (Tanzania Electronic Single Window System-eSWS) ili kuwaweka pamoja
wadau wote wa kuondosha shehena bandarini na mipakani. Kukamilika kwa mradi
huo, kutarahisisha na kupunguza muda na gharama za utoaji na upitishaji wa
shehena bandarini.
Mawasiliano
78.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi wa Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa
miundombinu ya itifaki (Internet Protocol – Multiplier Label Switching) pamoja
na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi data
ambacho hadi sasa mifumo ya taasisi 27 imeunganishwa ukiwemo mfumo wa
ukusanyaji mapato wa TRA. Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutaongeza
usalama, usiri wa data, kujikinga na
majanga na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na muingiliano wa mifumo
katika Kituo cha Data cha Taifa na
vituo vingine vitakavyojengwa nchini.
79.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea
na ujenzi wa miundombinu ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini ambapo
vijiji 1,921 vimepatiwa huduma hiyo. Aidha, Serikali imeimarisha huduma za simu
na intaneti katika taasisi za umma zikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya
polisi na ofisi za posta. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake hadi katika ngazi ya
wilaya. Vilevile, kuendelea kusimamia kampuni za simu nchini ili ziweze kutoa
kumbukumbu sahihi kwa lengo la kukokotoa mapato yatokanayo na malipo ya huduma
za simu za kitaifa na kimataifa.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
80.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza
kwa mafanikio mpango wa utoaji wa elimu ya awali na elimumsingi bila malipo.
Tangu kuanza kwa mpango huo, Serikali imekuwa inapeleka kwa wakati na moja kwa
moja shuleni fedha zote za ruzuku ya elimumsingi. Kiasi cha shilingi bilioni
20.8 kinapelekwa kila mwezi kwa shule zote za msingi na sekondari nchini,
ikijumuisha fedha za posho maalum kwa Walimu Wakuu, Waratibu wa Elimu Kata na
Wakuu wa Shule.
81.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji mzuri wa
mpango wa elimumsingi bila malipo umechangia kuimarika kwa mahudhurio ya
wanafunzi darasani; kuongezeka kwa ubora wa elimu inayotolewa shuleni kutokana
na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuongezeka kwa
udahili wa wanafunzi. Kwa mfano, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la
kwanza imeongezeka kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,120,667 mwaka 2016, sawa
na ongezeko la asilimia 35.2. Kwa mwaka huu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa
darasa la kwanza ni 2,078,379. Vilevile, wanafunzi waliofaulu mtihani wa kuhitimu
darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi
448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 538,826 mwaka 2016; na mwaka 2017 wanafunzi
562,695 wamechaguliwa kuingia sekondari.
82.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na
sekondari ikiwemo ukarabati wa shule za sekondari kongwe 89 ili kuboresha
mazingira ya shule na kuinua ubora wa elimu. Aidha, Serikali imenunua na
kusambaza vifaa vya maabara vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kwa shule
za sekondari 1,696 kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa
nadharia na vitendo. Vilevile, walimu 3,347 wa masomo ya sayansi na hisabati na
mafundi sanifu wa maabara 386 wameajiriwa.
83.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kutoa kipaumbele kwenye elimu, imeleta hamasa kubwa kwa
wananchi kuchangia maendeleo ya elimu. Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa
wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia kwa hiari maendeleo ya elimu
kupitia Ofisi za Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri. Aidha, naziagiza
Halmashauri zote nchini kuratibu na kusimamia ipasavyo michango ya hiari ya
elimu inayotolewa na wananchi na matumizi yake, hususan kwa kuanzisha Mfuko
Maalum wa Elimu katika Halmashauri husika ambao utasimamiwa na Bodi.
84.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza
bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365
mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 483 mwaka 2017. Hatua hiyo imewezesha idadi ya
wanaonufaika na mikopo hiyo kuongezeka kutoka wanafunzi 98,300 mwaka 2015 hadi
wanafunzi 119,435 mwaka 2017/2018. Serikali pia inaendelea kujenga na
kukarabati miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu nchini ili kuboresha mazingira
ya vyuo hivyo na kuviwezesha kuzalisha wataalam mahiri wanaoweza kujiajiri au
kuajiriwa katika soko la ajira. Natoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na wadau wa elimu kufanya
tathmini na kuboresha mfumo wa
ufundishaji wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini ili kuwapatia mbinu
zitakazowawezesha kujiajiri.
85.
Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya
Elimu wa mwaka 2017 hadi 2021 pamoja na mpango kazi wake unaolenga kutekeleza
vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2025. Utekelezaji wa mpango huo wa sekta ya elimu utasaidia
kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi wa kati na wa juu ifikapo mwaka 2021.
Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya ukarabati
wa shule kongwe, kujenga ofisi za udhibiti ubora katika wilaya mbalimbali
nchini, kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari na kujenga
vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari.
Maji
Huduma ya Maji Vijijini
86.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji
wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini kwa kujenga, kupanua na
kukarabati miradi ya maji. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya miradi 71 imekamilishwa
vijijini na mingine 366 inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa miradi
hiyo, umewezesha kuongezeka idadi ya wananchi wanaopata maji vijijini. Pia, Serikali imepanga kubadilisha mitambo
inayotumia nishati ya dizeli kusukuma maji na kufunga mitambo inayotumia
nishati ya jua ili kuwapunguzia wananchi gharama za uendeshaji na matengenezo.
87.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itakamilisha
ujenzi wa miradi ya
maji 387 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuanza miradi mipya ya maji
vijijini; kutekeleza miradi ya maji vijijini katika maeneo kame na yenye shida
kubwa ya maji; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa mabwawa pamoja na upanuzi wa
miundombinu ya maji kutoka kwenye mabwawa na visima vilivyochimbwa. Vilevile,
Serikali itaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika maeneo ya
Tabora, Kigoma na Same - Mwanga- Korogwe.
Huduma ya Maji Mijini
88.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018,
Serikali imejenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo
mbalimbali mijini ili kufikia malengo yaliyowekwa. Juhudi hizo zimewezesha hali
ya upatikanaji wa maji kwenye miji mikuu ya mikoa kufikia wastani wa asilimia
78. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na DAWASA,
upatikanaji wa maji umefikia asilimia 75. Aidha, upatikanaji wa maji katika
miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya kitaifa
umefikia asilimia 60. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kukamilisha
miradi mingi ya maji iliyopo.
Afya
Utoaji wa Chanjo
89.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia
shughuli za utoaji wa chanjo nchini ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa
kitaifa na kimataifa yanafikiwa. Hadi
sasa, Tanzania imefikia kiwango cha juu cha asilimia 97 ya utoaji wa chanjo ya pentavalent kwa watoto inayokinga
magonjwa ya kifaduro, dondakoo, pepopunda, homa ya ini na mafua. Kutokana na
kufikia kiwango hicho, mwezi Desemba 2017, Serikali ya Tanzania ilipongezwa na
Shirika la Afya Duniani kwa hatua hiyo kubwa. Lengo la Shirika la Afya Duniani
ni kila nchi kufikia kiwango cha uchanjaji wa asilimia 90.
90.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio hayo
yamefikiwa kutokana na usimamizi madhubuti wa Serikali katika utoaji wa chanjo.
Niwapongeze sana viongozi na watendaji wa sekta ya afya pamoja na mamlaka zote
zinazohamasisha na kutoa huduma za chanjo hapa nchini.
Upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba
91.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na
vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya. Bajeti kwa ajili
ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
imeongezwa kutoka shilingi bilioni 252 mwaka 2016/2017 na kufikia shilingi
bilioni 269 mwaka 2017/2018. Kutokana na ongezeko hilo, upatikanaji wa aina 135
ya dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini umeimarika na
kufikia asilimia 89.6.
Huduma za Tiba za Kibingwa
92.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeboresha na
kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini. Huduma zilizoimarishwa ni pamoja na upandikizaji wa figo na vifaa vya
kuongeza usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji kwa kutumia
tundu dogo na kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Vilevile, Serikali imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambapo dawa zinapatikana na muda wa kupata
huduma ya mionzi ya saratani umepungua. Kutokana na
maboresho hayo, idadi ya wagonjwa waliopewa rufaa ya matibabu nje ya nchi
imepungua kutoka wagonjwa 304 mwaka 2016/2017 na kufikia 103 mwaka 2017/2018. Hatua
hiyo imesaidia kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali ingetumia kuwapeleka
wagonjwa hao nje ya nchi.
ULINZI NA USALAMA
93.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya mipaka ya
nchi yetu ni salama. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuliimarisha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutoa mafunzo na mazoezi ya kijeshi,
kulipatia vifaa, zana, mitambo bora na ya kisasa pamoja na kuweka na kuimarisha
miundombinu muhimu na ya kimkakati ili kuliwezesha jeshi kutekeleza jukumu lake
la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Vilevile, Serikali imeweka alama za mipakani
ili kuimarisha ulinzi na kulinda vema mipaka ya nchi. Aidha, Jeshi la Wananchi
linashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mamlaka za kiraia na
mataifa mengine kupambana na matishio mapya ya kiusalama yakiwemo ugaidi,
uharamia, uhamiaji haramu, biashara haramu za dawa za kulevya na usafirishaji
haramu wa binadamu.
94.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu
limeendelea kudumisha ushirikiano na nchi nyingine duniani kupitia mafunzo ya
pamoja na operesheni za kikanda na kimataifa chini ya Umoja wa Afrika na Umoja
wa Mataifa. Katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani, tarehe 7 Desemba
2017 nchi yetu ilipoteza askari 15 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika
mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa askari wetu wanaolinda amani. Kwa
mara nyingine, naomba kuungana na Mheshimiwa Rais na Watanzania wote kuzipa
pole familia za mashujaa hawa waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi wa
amani. Licha ya changamoto zinazojitokeza, Tanzania itaendelea kushirikiana na
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani
kwenye nchi mbalimbali duniani ili kuendelea kuifanya dunia kuwa mahali salama
pa kuishi pamoja na kuyaongezea majeshi yetu uzoefu na mbinu za kisasa za ulinzi wa amani.
95.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa
usalama wa raia, Serikali imelipatia Jeshi la Polisi vitendea kazi muhimu
ikiwemo vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uchunguzi ili liweze kupambana na
ujambazi na matukio mengine ya kihalifu nchini. Aidha, imejenga Kituo cha
Kisasa cha Mawasiliano (Call Centre) Dar es Salaam ambacho kinawezesha wananchi
kutoa taarifa ya matukio hayo kwa urahisi. Pia Serikali imehamasisha jamii
kushiriki katika ulinzi wao na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
lengo la kuwapatia taarifa za wahalifu na uhalifu. Natoa wito kwa wananchi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola ili
kudhibiti matukio ya kihalifu nchini.
96.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali
inatekeleza mradi wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration)
ambapo mwezi Januari 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Pasi Mpya ya Kusafiria ya
Kielektroniki ya Kimataifa ya Afrika Mashariki. Kuzinduliwa kwa pasi hii
kutapunguza vikwazo vya kusafiri mipakani baina ya raia wa nchi wanachama,
kuimarisha mahusiano na kuchochea shughuli za kiuchumi miongoni mwa raia wa
Jumuiya hii. Natoa rai kwa Watanzania kuanza kutumia pasi hii na kuendelea
kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, ajira na elimu
zinazopatika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
97.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua
hiyo, Serikali imedhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji haramu wanaoingia
nchini kwa sababu mbalimbali. Aidha, ofisi tisa mpya za uhamiaji zimefunguliwa
katika wilaya za Gairo, Iramba, Kakonko, Kilosa, Kiteto, Manyoni, Mvomero, Siha
na Songwe kwa lengo la kuongeza udhibiti wa wahamiaji haramu. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa uhamiaji
mtandao.
BUNGE
98.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka
2017/2018, kumekuwa na mikutano mitatu ya Bunge ambapo masuala mbalimbali
yalijadiliwa na kutolewa ufafanuzi na Serikali. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge,
Mkutano huu wa Bajeti utakuwa unahitimisha idadi ya mikutano minne ya Bunge kwa
mwaka huu wa fedha unaoishia Juni, 2018. Katika mikutano mitatu iliyopita,
maswali ya msingi 359 na maswali ya nyongeza 1,002 yaliulizwa na Waheshimiwa
Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, katika utaratibu wa maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu, maswali ya msingi 17 pamoja na mawili ya nyongeza
yaliulizwa na kujibiwa. Miswada 15 ya Sheria ya Serikali iliwasilishwa,
kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
99.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Bunge
liliratibu na kusimamia shughuli za vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa
huduma za hansard, utafiti, utawala
na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa wabunge na watumishi wa Ofisi ya Bunge. Pia,
Bunge lilijadili na kuridhia Maazimio matano yanayohusu utekelezaji wa Mikataba
ya Kimataifa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge
kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
MAHAKAMA
100. Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali
imeendelea kutoa kipaumbele katika kuongeza ufanisi wa utendaji wa mhimili wa
Mahakama nchini. Katika mwaka 2017/2018, Mahakama imesikiliza na kukamilisha
mashauri 494,525 kati ya 513,329, sawa na asilimia 96.3 ya mashauri yote katika
ngazi zote za Mahakama. Hatua hii imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri
katika mahakama zetu. Hali kadhalika, katika kipindi hicho Serikali
imekamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Mara.
Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Wilaya na za
Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini.
MASUALA MTAMBUKA
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali
101.
Mheshimiwa Naibu
Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali
ilizindua Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Shughuli za
Serikali. Mfumo huo unalenga kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za
Serikali na kuiwezesha Serikali kufanya tathmini ya utoaji huduma kwa wananchi
na mipango ya maendeleo. Mfumo huo umeanza kufanya kazi ambapo kwa sasa Wizara
zote zinawasilisha utekelezaji wa shughuli zao kupitia mfumo huo. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaimarisha matumizi ya mfumo huo hasa katika ngazi za
Mikoa na Halmashauri na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.
Hifadhi ya Mazingira
102. Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza jukumu la usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini.
Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeongeza hamasa na ushirikishwaji mkubwa wa
wananchi katika suala la usafi, utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo
yote ikiwemo makazi yao. Hatua hiyo
imetokana na ushiriki mkubwa wa viongozi wa kitaifa, mikoa na watendaji wa
ngazi zote katika shughuli za usafi na uhifadhi wa mazingira.
103. Mheshimiwa Naibu
Spika, ili
kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi ya mazingira nchini, Serikali
imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira kutoka 62 hadi kufikia 512. Aidha,
kaguzi 380 zimefanyika kwenye viwanda kwa lengo la kufanya tathmini za
mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda
unaozingatia utunzaji bora wa mazingira.
104. Mheshimiwa Naibu
Spika, kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili, napenda kusisitiza kwamba halmashauri
zote nchini ziweke mpango mahsusi wa kuhifadhi mazingira unaojumuisha kupanda
na kutunza miti. Serikali itaweka utaratibu wa upimaji wa utendaji wa wakuu
wote wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri unaozingatia
uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
105.
Mheshimiwa Naibu Spika,
katika mwaka 2017/2018, Serikali imeimarisha utendaji wa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuipatia wataalamu,
vifaa na kuongezea fedha. Aidha, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya ya mwaka 2015, imefanyiwa marekebisho ili kuondoa mapungufu
yaliyojitokeza katika utekelezaji wake. Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya dola, ilikamata jumla ya watuhumiwa 11,071 na kati yao, watuhumiwa
3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao walifikishwa mahakamani. Watuhumiwa wengi waliokamatwa, walijihusisha na
dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na heroine.
106.
Mheshimiwa Naibu Spika,
katika kipindi hicho, jumla ya tani moja na kilo 561.28 za dawa
aina ya heroin zilikamatwa. Kati ya
hizo, kilo 196.28 zilikamatwa kwenye eneo la maji ya Tanzania na nchi kavu na
tani moja na kilo 365 zilikamatwa kwenye bahari kuu kwa kushirikiana na
washirika wa kimataifa na kuteketezwa. Aidha, kilo 5.2
za cocaine, tani 47.7 za bangi na
tani 7.4 za mirungi zilikamatwa. Mamlaka pia ilikamata lita 304,513 za
vimiminika vya kemikali bashirifu na kilo 22,143 za kemikali bashirifu yabisi.
Katika operesheni za uteketezaji wa mashamba ya bangi na mirungi, ekari 572.75
za bangi na ekari 64.5 za mirungi ziliteketezwa.
107. Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali
imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za
kulevya kwa kutumia methadone katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke jijini Dar es Salaam.
Vilevile, Serikali
imeanzisha vituo vipya vya tiba hiyo ili kuwafikia waathirika wengi zaidi
nchini ambapo kliniki saidizi za kutibu waathirika wa dawa za kulevya
zimeanzishwa katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mbeya na Mwanza. Hadi kufikia
Januari 2018, zaidi ya watumiaji 5,560 walikuwa wakipatiwa huduma za tiba ya methadone katika vituo mbalimbali
nchini. Serikali pia imekuwa ikisimamia uanzishwaji wa nyumba za upataji nafuu
(Sober House) ambazo hadi sasa idadi yake ni 22. Aidha, mwezi Februari 2018,
Serikali ilizindua mwongozo wa uendeshaji wa sober houses unaolenga kuwawezesha wamiliki wa nyumba hizo
kuwasaidia waathirika hao ipasavyo.
108.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Machi 2018,
nchi yetu ilishiriki katika Mkutano wa 61 wa Kimataifa wa Commission for Narcotic Drugs (CND) uliofanyika Vienna, Austria na
kushirikisha zaidi ya nchi 150. Katika mkutano huo, Tanzania ilitambuliwa kama
nchi ya mfano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya barani Afrika na kupewa
heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Vyombo vinavyopambana na
Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani (HONLEA) kutoka Afrika,
utakaofanyika Septemba 2018. Mkutano huo utatoa fursa kwa wataalam nchini
kubadilishana taarifa, uzoefu, kujenga mahusiano na kujifunza mbinu
zinazotumiwa na nchi nyingine katika kukabiliana na dawa za kulevya.
109. Mheshimiwa Naibu
Spika, natoa
rai kwa viongozi na watendaji kuwaelimisha vijana kuhusu madhara yatokanayo na
matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, wananchi waendelee kushirikiana na Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kutoa taarifa kuhusu
wanaojihusisha na dawa hizo. Pia ni vema wazazi, walezi na jamii kuwa karibu na
vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili kuwaepusha kuingia kwenye mkumbo wa
matumizi ya dawa za kulevya.
Vita dhidi ya Rushwa
110.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano imeendelea kupambana na rushwa pamoja na ufisadi. Katika kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla
ya majalada 325 yalifanyiwa uchunguzi na TAKUKURU na kuwasilishwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 214 kati ya hayo yalipata kibali cha
kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Aidha, kesi 727 ziliendeshwa mahakamani na kesi 219
ziliamuliwa na watuhumiwa 138 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Kutokana na
operesheni zilizofanywa na TAKUKURU katika maeneo ya ukusanyaji mapato, uzuiaji
wa malipo hewa na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni
58.4 ziliokolewa na kurejeshwa Serikalini.
111.
Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU pia
imefuatilia miradi ya maendeleo 195 yenye thamani ya shilingi bilioni 154.1
katika sekta za elimu, afya, maji na ujenzi ili kuhakikisha kuwa fedha za umma
zinatumika kama zilivyokusudiwa na thamani ya fedha inapatikana. Katika
ufuatiliaji huo, miradi 73 yenye thamani ya shilingi bilioni 30.9 ilibainika
kuwa na kasoro katika utekelezaji wake. TAKUKURU imetoa mapendekezo ambayo
yanafanyiwa kazi na Serikali na tayari hatua za kinidhamu na kisheria
zimechukuliwa kwa wahusika.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
112. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali
imedhamiria kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika jamiii.
Ili kutekeleza azma hiyo, Mpango wa Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama
kwenda kwa Mtoto umepewa kipaumbele. Aidha, elimu ya UKIMWI imetolewa kupitia
vyombo vya habari, majarida na vipeperushi. Vilevile, elimu imetolewa kwa
kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu rika pamoja na kuwashirikisha
viongozi na watu mashuhuri, viongozi wa dini, sekta binafsi na kutekeleza
programu za kupambana na UKIMWI mahali pa kazi.
Kutokana na juhudi hizo, matokeo ya utafiti uliofanyika katika ngazi
ya kaya kuanzia mwezi Oktoba 2016 hadi Agosti 2017 yanaonesha kuwa wastani wa
kitaifa wa maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni
asilimia 4.7. Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba kiwango cha maambukizi
mapya ya VVU kwa mwaka ni asilimia 0.27.
113.
Mheshimiwa Naibu
Spika, Serikali inatoa huduma kwa
wananchi wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) nchini. Hadi kufikia Septemba
2017, WAVIU 972,127 sawa na asilimia 70 ya WAVIU wote walikuwa wanapatiwa dawa
za kufubaza makali ya VVU (ARV’s). Katika mwaka 2017/2018, Serikali kwa
kushirikiana na wadau wamechangia zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwenye Mfuko
Maalum wa UKIMWI ili kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili. Katika mwaka
2018/2019, Serikali itaanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Kudhibiti
UKIMWI wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023. Vilevile, kampeni maalum za
kushawishi wanaume kushiriki katika kupima afya zao na vijana kujitambua
zitaendeshwa.
Uratibu wa Maafa
114.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali imeendelea kuratibu shughuli za usimamizi wa
maafa nchini kwa kuzuia, kupunguza madhara na
kujiandaa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea. Aidha, mfumo wa
ufuatiliaji wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa taarifa za
tahadhari za awali ili kupunguza madhara ya maafa umeboreshwa. Serikali pia
imekamilisha kusimika mashine 36 za kisasa za kufuatilia taarifa za hali ya
hewa katika wilaya mbalimbali nchini pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa
hali ya hewa. Jitihada hizi zimeongeza uhakika wa utabiri wa hali hewa nchini
kufikia asilimia 87.
115.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali imeimarisha ushirikiano katika masuala ya
usimamizi wa maafa kupitia Umoja wa Afrika na jumuiya za SADC, EAC na IGAD.
Ushirikiano huo, umewezesha nchi wanachama kubadilishana taarifa za kuandaa
utabiri wa hali ya hewa na matumizi yake katika kupunguza madhara ya maafa.
Vilevile, nchi hizo zinabadilishana uzoefu pamoja na kutoa mafunzo ya usimamizi
wa maafa kwa wataalam wa nchi wanachama. Katika mwaka 2018/2019, Serikali
itaendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na Wilaya na
kuratibu shughuli za kupunguza madhara ya maafa na misaada ya kibinadamu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru
116.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali iliratibu mbio za Mwenge wa Uhuru kwa lengo la
kukuza mshikamano na kuhimiza shughuli za maendeleo. Katika mbio hizo ambazo
kilele chake kilikuwa tarehe 14 Oktoba 2017 Mjini Magharibi Zanzibar, miradi
1,512 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.06 iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa. Kati ya miradi hiyo,
miradi 150 yenye thamani ya shilingi bilioni 568.8 ilikuwa ya viwanda. Uzinduzi wa mbio za mwenge kwa mwaka 2018
ulifanyika mkoani Geita tarehe 2 Aprili 2018 na kilele chake kitafanyika mkoani
Tanga, tarehe 14 Oktoba 2018. Ninawasihi wananchi kushiriki kwa wingi wakati wa
mbio za Mwenge wa Uhuru kwani zinalenga kuleta umoja na mshikamano kwa wananchi
pamoja na kuhimiza shughuli za maendeleo.
MAHUSIANO YA KIMATAIFA
117.
Mheshimiwa Naibu Spika,
jukumu la kuimarisha
mahusiano na mataifa mengine duniani, mashirika ya kimataifa na washirika wetu
wa maendeleo limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali katika kutekeleza Sera
yetu ya Mambo ya Nje. Katika kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi, Serikali
inafanya mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ili iweze kukidhi mahitaji na matakwa
ya sasa ya Tanzania katika kushughulikia siasa za kimataifa na diplomasia
pamoja na masuala ya mtangamano wa kikanda na kuendeleza Umoja wa Afrika.
118.
Mheshimiwa Naibu Spika,
kwa mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza
diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na watalii; kutafuta fursa za mafunzo; kuendelea kuwashirikisha Watanzania waishio
ughaibuni kuchangia katika maendeleo ya nchi yao pamoja na kutafuta ajira na
masoko ya bidhaa za Tanzania nje. Aidha, Serikali itaimarisha sera ya ujirani mwema kwa lengo la
kukuza mahusiano na kufungua milango ya ushirikiano katika utekelezaji wa
miradi ya kitaifa ya kipaumbele
hususan, reli, barabara, nishati na biashara na majirani zetu.
Vilevile, Serikali itatoa msukumo kwa Mabalozi kutumia ushawishi wao
kuitangaza vyema
miradi ya kipaumbele na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini na kutangaza lugha
ya Kiswahili ambayo ikitumika vizuri inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa
Watanzania.
HITIMISHO
119. Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi
wanashuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi cha
takriban miaka miwili na nusu tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi
mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania iingie madarakani. Mafanikio hayo yanatoa matumaini kwa
Watanzania kwamba yale yaliyoahidiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano
yatatekelezwa.
120. Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo
ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali pamoja na mambo mengine,
itaweka mkazo katika kudhibiti upotevu wa mapato; kuimarisha mfumo wa kukusanya
mapato hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kudhibiti matumizi ya
fedha na rasilimali nyinginezo za umma. Aidha, msukumo utawekwa katika kuhimiza
uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi ya
maendeleo.
121. Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais
wakati anazindua Bunge lako Tukufu tarehe 20 Novemba 2015, pamoja na mambo
mengine aliweka wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa
viwanda kwa lengo la kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania.
Ili kufikia azma
hiyo, Serikali itaendelea kufanya yafuatayo:
Mosi: Kuimarisha na
kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta maendeleo
endelevu;
Pili: Kuboresha
mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na utoaji huduma;
Tatu: Kujenga miundombinu
muhimu ikiwemo reli, bandari, viwanja vya ndege, barabara na madaraja;
Nne: Kuimarisha
uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika sambamba na kuongeza kasi ya
upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi na viwanda;
Tano: Kusimamia viongozi
na watendaji wote ili kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia
wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote; na
Sita:
Kusimamia
kikamilifu rasilimali zilizopo ili zitumike kwenye maeneo yanayochochea ukuaji
uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi.
122. Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa kila
mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya
uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu uaminifu na
kupiga vita rushwa.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2018/2019
122.
Mheshimiwa Naibu
Spika, kwa
mwaka 2018/2019, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake inaliomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Arobaini na Tatu,
Milioni Mia Sita Kumi na Nane, Mia Saba Sitini na Mbili Elfu na Mia Sita Tisini na Nane (Shilingi
143,618,762,698). Kati ya fedha hizo, Shilingi
Bilioni Sabini na Nne, Milioni Mia Tano Ishirini na Saba, Mia Tatu Ishirini na
Moja Elfu na Mia Sita Tisini na Nane (Shilingi 74,527,321,698) ni kwa ajili
ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
Bilioni Sitini na Tisa, Milioni Tisini na Moja, Mia Nne Arobaini na Moja Elfu
(Shilingi 69,091,441,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
123. Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, naliomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Ishirini na Tano, Milioni Mia Tano Ishirini na Moja, na Mia
moja Elfu (Shilingi 125,521,100,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya
fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja
Kumi na Saba, Milioni Mia Mbili na Tano, Mia Nne Themanini na Saba Elfu (Shilingi
117,205,487,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Tatu
Kumi na Tano, Mia Sita Kumi na Tatu Elfu (Shilingi 8,315,613,000) ni kwa
ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
124.
Mheshimiwa Naibu Spika,
naomba
kutoa hoja.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.