Saturday, May 5, 2018

WATAALAM WA AFYA MOJA WAITAKA WIKI YA CHANJO KWA MIFUGO NCHINI

Baadhi ya Wataalamu wa Afya moja  wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya  mkutano  wa “Cross-Border” uliowakutanisha wataalamu  hao kutoka katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma kujadili  mikakati ya  kudhibiti ugonjwa wa Kimeta, Jijini, Arusha
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Timothy  Wonanji ,akisisitiza jambo  wakati wa Mkutano wa mkutano wa “Cross-Border” uliowakutanisha wataalamu  wa Afya moja kutoka katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma  kujadili  mikakati ya  kudhibiti ugonjwa wa Kimeta, Jijini, Arusha.

Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Janneth Mghamba,akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa mkutano wa “Cross-Border” uliowakutanisha wataalamu wa Afya moja kutoka katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma kujadili mikakati ya  kudhibiti ugonjwa wa Kimeta , Jijini, Arusha.

Baadhi ya Wataalamu wa Afya moja  kutoka katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma wakifuatilia mkutano  wa “Cross-Border” uliowakutanisha kujadili mikakati ya  kudhibiti ugonjwa wa Kimeta, Jijini, Arusha.

Katika kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti wa ugonjwa wa Kimeta na  Kichaa cha mbwa nchini wataalamu wa Afya moja ambao  ni wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Afya ya Wanyama wafugwao na wanyamapori pamoja na sekta ya Mazingira, wameitaka serikali kuanzisha wiki ya chanjo kwa mifugo nchini ili kuhamasisha chanjo hizo kwa kuwa na mkakati wa pamoja na kwa wakati mmoja na hatimaye kuweza kudhibiti maaambukizi ya magonjwa hayo kwa binadamu.
Ugonjwa huu huwapatawanyama na binadamu kwa njia ya kung’atwa na Mbwa, Paka, Fisi au mnyama mwingine anaye ugua kichaa cha mbwa. Ugonjwa huu hauna tiba ila unazuilika kwa njia ya chanjo.

Wakiongea jijini Arusha  wakati wa Mkutano wa Ujirani wa kujiandaa, kujikinga na udhibiti wa magonjwa, uliowakutanisha wataalamu hao kutoka katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma, wamebainisha kuwa wameamua kutoka na azimio hilo kutokana na kuwa katika baadhi ya wilaya za mikoa hiyo milipuko ya  ugonjwa  wa kimeta imekuwa ikijirudia hata ndani ya mwaka moja.
Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Janneth Mghamba,amesema Wizara imekuwa ikipokea taarifa za ugonjwa  wa Kimeta mara kadhaa katika baadhi ya Wilaya za Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro hali inayodhihirisha hakuna mikakati ya kutosha ya udhibiti wa ugonjwa huo.
“Kinga ni bora kuliko matibabu, hivyo ili kudhibiti haya magonjwa yanayotoka kwa wanyama hatuna budi kujikita katika chanjo ya wanyama hao ili kupunguza maabukizi ya wanyama hao kwa binadamu ,  Chanjo ya Kimeta na kichaa cha mbwa kwa wanyama ni ndogo kuliko matibabu yake. Tukiwa na uhamasishaji mzuri wa chanjo na hasa kupitia hata wiki ya chanjo, serikali itaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hutumika katika tiba ya magonjwa hayo” Alisema Mghamba.
Aidha Mghamba aliongeza kuwa , katika kuhakikisha kunakuwepo na mikakati ya udhibiti wa ugonjwa huo imewakutanisha wataalamu wa afya wa mikoa husika  kwa kutumia dhana ya afya moja ili waweze kujadili kwa pamoja na kuwa na mipango ya udhibiti ya pamoja kwani magonjwa hayana mipaka, Aidha hatua hiyo ya kuwa na mikakati ya pamoja itaweza kupunguza gharama za udhibiti wa magonjwa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Timothy Wonanji  na Daktari wa wanyamaWilayani Monduli,Dkt. Yandu Marmo  wamefafanua kuwa upo mwingiliano mkubwa wa wanyama na binadamu, katika hali hiyo uwezekano wa magonjwa ya wanyama kuwaambukiza binadamu ni mkubwa. Aidha walieleza kuwa kukiwepo na kampeni maalum ya kuhamasisha kuchanja wanyama kutapunguza maabukizi ya magonjwa hayo.
Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 60% ya magonjwa wanayoyapata binadamu yanatoka kwa wanyama. Kwa kulitambua hilo,Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini, Afya Moja ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na  mazingira katika kujiandaa , kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu ,wanyamapori na mifugo.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.