*Ni baada ya kujengwa kwenye eneo la wazi na kuziba barabara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi kubomoa uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto na kusitisha mara moja shughuli za ujenzi kwenye eneo hilo.
Uzio huo ambao mbali na kujengwa katika eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto kwenye mtaa wa Mji Mpya kata ya Madukani pia umeziba barabara ya tisa, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 21, 2018) wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi jijini Dodoma, ambapo alitembelea eneo hilo na kuagiza libomolewe na lisalie kama inavyoonekana katika ramani na aliyeuziwa atafutiwe eneo lingine.
“Huu mji umejengwa kwa ramani, hamuwezi kubadili ramani kwa lengo la kumpa mtu eneo. Kwa nini mmeziba barabara ya tisa na huu mji unatambulika kwa barabara, sasa bomoeni hapa nataka barabara iendelee kutumika na eneo la kuchezea watoto libaki wazi,”
Waziri Mkuu amemuagiza mkurugenzi wa jiji ahakikishe wanayatumia maeneo ya wazi kwa ajili ya kujenga sehemu za mapumziko ili kuwawezesha wananchi kupata maeneo ya kupumzika mara wanapomaliza kufanya shughuli zao za kikazi.
Amesema ni vema jiji likatenga ardhi na kupima viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya biashara, makazi, taasisi, huduma za jamii, viwanda pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya mapumziko. “Msifanye makosa kama yaliyofanyika Dar es Salaam.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipangomiji wa jiji la Dodoma, Bw. Joseph Mafulu alimuonyesha Waziri Mkuu ramani ambayo iliyotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ambayo ilibadilisha matumizi ya eneo hilo na kumpa muwekezaji.
Baada ya Bw. Mafulu kuonesha ramani hiyo Waziri Mkuu alitoa ramani halisi ya jiji la Dodoma ambayo inaonesha eneo hilo ni la wazi na ni mahususi kwa ajili ya michezo ya watoto, hivyo alisisitiza kuwa litumike kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu aliwaonya watumishi wa halmashauri ya jiji la Dodoma kutorudia makosa yaliyofanywa na CDA na kwamba jukumu lao ni kuhakikisha wanayasahihisha makosa yaliyofanywa na mamlaka hiyo ili jiji liweze kupangika vizuri.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi aliahidi kuyafanyia kazi kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kesho (Jumatatu, Oktoba 22, 2018) ataandika barua kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi kwa ajili ya kufuta hati ya eneo hilo na muwekezaji watampa eneo lingine.
Awali,Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa halmashauri ya jiji la Dodoma, ambapo aliwataka wabadilike na wasimamie vizuri rasirimali za umma pamoja na kuwahamasisha na kuwasisitiza wananchi wafanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu alisema mtumishi asiyeweza kufanya kazi kwa bidii anaweza kupata matatizo kwa sababu Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini pamoja na mameneja wasimamie vizuri utendaji kazi wa watumishi mbalimbali katika maeneo yao. Alisisitiza kuwa lazima watumishi wafanye kazi na matokeo yaonekane.
Pia Waziri Mkuu alifungua ofisi kuu ya kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupora na kisha alitembelea kiwanda cha kusindika zabibu cha Alko Vintage na kukagua uzalishaji wa mvinyo katika kiwanda hicho kilicho jijini Dodoma.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.