Wednesday, October 10, 2018

WAZIRI MKUU ABAINI UBADHILIFU HALMASHAURI YA MPWAPWA


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema atatuma timu maalum kuchunguza wizi unaofanyika kupitia ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa na kwamba hakuna atakayethubutu kuharibu ushahidi kwa kuwa nyaraka zote za ukusanyaji anazo.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 10, 2018) wakati akizungumza na wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma.
Amesema hayo baada ya kubaini ubadhirifu kwenye makadirio na ukusanyaji wa mapato unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Idara ya Fedha na Mipango kwenye Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu amesema maeneo ya ubadhirifu ambayo ambayo ameyabaini ni katika ukusanyaji wa ushuru wa samaki kwenye bwawa la Mtera, Kituo Kikuu cha Mabasi Mpwapwa na kwenye ushuru wa mabango na majengo.

Amesema katika halmashauri hiyo kuna genge la wabadhirifu, ambalo ndilo lililosababisha kufukuzwa kazi kwa Mkurugenzi wa awali wa halmashauri hiyo, ambapo sasa  hawatoi ushirikiano kwa Mkurugenzi aliyekuwepo Bw. Peter Swea kwa kuwa amedhibiti mianya ya ubadhirifu.

Waziri Mkuu akiwa kwenye mkutano huo alimtaka Afisa Mipango wa halmashauri hiyo kusimama na kueleza namna anavyokadiria na kukusanya mapato. "Afisa Mipango hebu tueleze namna unavyopanga katika kukadiria na kukusanya mapato, je unakwenda field "eneo la kazi" au unabandika tu makadirio kwenye makaratasi," amehoji.

Afisa Mipango huyo alieleza kuwa huwa anakwenda kwenye eneo la tukio kabla ya kuandaa makadirio ya mapato na baada ya kutoa maelezo hayo Waziri Mkuu akaeleza namna makadirio na ukusanyaji mapato yaliyofanyika kwenye ushuru wa samaki.

“Katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilikadiriwa kukusanywa sh. milioni 80 lakini fedha zilizokusanywa ni sh. milioni 32 na kwenye mwaka wa fedha uliofuata makadirio uliyashusha kwa asilimia 50 lakini fedha zilizokusanya ni sh. milioni 109.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kwenye ushuru wa mabango kwa mwaka wa fedha 2016/2017 walikadiria kukusanya sh. milioni tisa lakini fedha zilizokusanywa ni sh. milioni moja sawa na asilimia 17. Pia kwenye mwaka wa fedha 2018/2019 makusanyo yaliyokadiriwa ni sh. milioni saba lakini hadi sasa hakuna fedha zozote zilizokusanywa.

"Kwenye ushuru wa majengo mwaka 2017/2018 makadirio yalikuwa kukusanya sh. milioni 5.5 lakini makusanyo yalikuwa sh.milioni 20 zaidi ya asilimia 360. Hapa tunaweza kusema ulifanya vizuri. Hata hivyo kwenye mwaka huu wa fedha licha ya makusanyo hayo makadirio yaliyowekwa ni kukusanya sh. milioni 5.5 lakini hadi jana hakuna fedha iliyokusanywa.”


Waziri Mkuu amesema kwenye ushuru wa kituo cha mabasi katika mwaka wa fedha 2016/2017 fedha ziliokadiriwa kukusanywa zilikuwa sh. milioni 7.2 na makusanyo yalikuwa sh. milioni 10.6 sawa na asilimia 148 na katika mwaka huu wa fedha makadirio yalikuwa sh. milioni 18 lakini hadi jana hakuna kiasi chochote cha fedha kilichokusanywa.

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.