Na; Mwandishi Wetu - Iringa
Naye, Mmoja wa Wanufaika wa Mafunzo
hayo, Bi. Felister Gerald ameishukuru serikali kwa kutambua mchango wa vijana na
kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kuwajengea uzoefu na ujasiri wa
kufanya kazi.
Vijana wahitimu wa Vyuo vya
elimu ya juu zaidi ya 3,200 nchini wamenufaika na Mafunzo ya vitendo mahala pa
kazi “Internship Training” yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira ambapo zamani ilikuwa ni Wakala wa Huduma za Ajira (TAESA).
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa
katika ziara Mkoani Iringa kutembelea waajiri wenye vijana wanaowapatia mafunzo
katika sehemu zao za kazi yaani “Interns”.
Waziri Mhagama alieleza kuwa
mafunzo hayo yamekuwa yakihusisha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu
ambapo wanapatiwa fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya kazi kwa
lengo la kuwapatia uzoefu wa kazi utakaowasaidia kuajiriwa au kujiajiri.
“Kuanzishwa kwa mafunzo hayo
ilikuwa ni moja kati ya maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba
vijana hususani kwenye masuala ya ajira nchini, hivyo vijana waliomaliza kozi
mbalimbali kupatiwa ujuzi katika maeneo ya kazi ili waweze kuwa na uzoefu pale
wanapojiajiri ama kuajiriwa,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa Mpango huu wa
mafunzo ya vitendo mahala pa kazi umekuwa na mchango mkubwa na ni chachu katika
kuwezesha nguvukazi ya taifa hususan vijana waliohitimu kwa kuwajengea uzoefu,
weledi na maadili ya kazi yanayohitajika pindi wanapoajiriwa.
“Tunataka kuona vijana
wanapomaliza mafunzo haya wanakuwa na dhana ya kuchangamkia fursa mbalimbali
ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu hii ya
tano kwa kuwa tayari mnauzoefu,” alisema Mhagama
“Ofisi ya Waziri Mkuu
itaendelea kufanya tathmini ya mafunzo haya na mafunzo mengine yanayotolewa chini
ya Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuona namna ujuzi wanaopatiwa vijana
nchini unakuwa wa manufaa katika kuwezesha vijana wanakuwa sehemu ya kufikisha
taifa lao katika uchumi wa kati,” alieleza Mhagama
Aidha Waziri Mhagama alitoa
wito kwa vijana ambao wamenufaika na mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidi, weledi
na maarifa kwa kuonyesha umahiri wa kujenga uchumi wa taifa.
Sambamba na hayo, alitoa pongezi
kwa waajiri wote nchi katika sekta ya Umma na Binafsi kwa namna
walivyoshirikiana na Serikali katika kuwapatia vijana mafunzo hayo kwa muda wa
miezi sita hadi mwaka mmoja na wamekuwa sehemu ya mafanikio katika kuziwezesha
taasisi kufikia malengo.
Naye Mkuu
wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela alieleza kuwa Programu hiyo ya
mafunzo kwa Vitendo sehemu za Kazi imekuwa na manufaa makubwa kwa vijana na
ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha ujao kutenga
bajeti zaidi kwa ajili ya kuwezesha vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali
nchini ili waweze kunufaika na mafunzo hayo.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa GIBRL Business Solutions Ltd, Bi.
Hadija Jabir alisema kuwa uwepo wa vijana wanaopatiwa mafunzo hayo katika
kampuni yake umekuwa na tija.
“Kama mwajiri nimeona ufanisi
wa vijana hao, naiomba serikali iwapatie nafasi zaidi ya vijana hao wanaohitimu
kufanya mafunzo katika sehemu za kazi ili yale waliyojifunza kwa nadharia
waweze kuyatekeleza kwa Vitendo,” alisema Jabir
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.