*Ni utekelezaji wa uamuzi wa Rais Dkt. John Magufuli
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameikabidhi
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nyumba 103 zenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni
tano kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini zilizojengwa
na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ikiwa
ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Baada ya kukabidhi nyumba hizo, Waziri Mkuu
amesema kwamba makazi hayo yawe chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya
Uhamiaji nchini katika kutambua wajibu wao wa kutoa
huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao.
Akikabidhi nyumba hizo leo (Jumanne, Juni 2,
2020), Waziri Mkuu amesema “Uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais ambao leo hii
tunashuhudia utekelezaji wake kupitia makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya
Maafisa na Askari wa Uhamiaji kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa
hapo awali ambapo waliishi uraiani.”
Ameongeza kuwa “Ni
ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya Shirika la Nyumba
la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya vielelezo vya utekelezaji wa
ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwapatia Maafisa na
Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba 103.”
Pia, Waziri Mkuu amesema “Nyote mtakubaliana
nami kwamba leo ni siku muhimu kwa sekta ya nyumba kwani ujenzi wa nyumba za
namna hii ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi
za Serikali sambamba na kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”
“Vilevile, utekelezaji wa mradi huu umetoa ajira
zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na ajira 800 za mafundi na ajira 200 kwa watoa
huduma za chakula yaani mama lishe. Upatikanaji wa ajira hizo umechangia
kuongeza kipato kwa walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya umaskini.”
Amesema ujenzi wa majengo hayo ni mwendelezo
wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015
inayosisitiza ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi kwa watumishi wa umma kwa
lengo la kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na
kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kuwahudumia
Watanzania.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Shirika
la Nyumba la Taifa, kuendelea na kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi
pamoja na biashara kwani lengo la Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kuwa Mwendelezaji Miliki Mkuu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema watendaji wa shirika hilo wanapaswa
kuongeza kasi
ya ukusanyaji kodi ili kuongeza mapato ya shirika. “Serikali kwa upande wake,
itaendelea kutoa Ushirikiano wa karibu kwa Shirika katika kutatua changamoto
zinazokabili utekelezaji wa malengo ya shirika hili.”
Wakati
huo huo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuimarisha ulinzi
na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho mbalimbali kama vile
Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti, vibali vya ukaazi, viza,
usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa njia ya kielektroniki. “Utekelezaji
mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya
ushindi wa pasipoti yenye ubora duniani kwa mwaka 2019.”
Waziri Mkuu amesema ushindi huo, umelipatia
sifa na heshima kubwa Taifa Kimataifa. “Halikadhalika, nimefurahishwa na
taarifa kuwa ujenzi wa Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea
vizuri. Ninawahimiza endeleeni hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”
Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna
Makakala aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwezesha Idara ya
Uhamiaji, kupata nyumba 103 za makazi kwa ajili ya Maafisa na Askari wa
Uhamiaji kwani hatua hiyo ni kielelezo cha vipaumbele vya Serikali katika
kuboresha makazi ya askari wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na
wananchi kwa ujumla.
“Aidha,
tunalipongeza pia Shirika la Nyumba la Taifa, kwa kubuni mradi mkubwa kwa ajili
ya kuboresha mazingira ya makazi ya Wananchi kwa kujenga na kuuza nyumba kwa
bei nafuu, ambapo nasi tumekuwa wanufaika wa mradi huu. Gharama za nyumba 103
za makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ni kiasi cha sh. 5,306,000,000.”
Alisema
upatikanaji wa nyumba hizo utasaidia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji
kuishi katika maeneo yao maalum, badala ya ilivyokuwa hapo awali ambapo
walilazimika kutafuta nyumba za makazi uraiani. Sambamba na hilo, itasaidia
kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, kwani itakuwa ni rahisi kuwapata
askari walio katika eneo moja mara wanapohitajika.
Makabidhiano
hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba
la Taifa, Dkt. Maulid Banyani, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo na Maafisa
wengine wa Serikali.
MWISHO
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.