Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amewataka wakandarasi wanaojenga majengo ya Wizara Awamu ya Pili katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma kuongeza kasi ya ujenzi ili kumaliza kwa wakati.
Dk. Jingu alitoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipofanya ziara yake kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi huo ambapo alisema ujenzi unaendelea vizuri huku akiwahimiza kuongeza wafanyakazi.
Pia aliwaagiza kuongeza muda wa kazi na kuongeza vifaa hatua itakayorahisisha kazi hiyo kufanyika kwa kasi inayotarajiwa ili ofisi hizo kuanza kutumika mara moja akisema kulingana na hali ya ujenzi baadhi ya majengo yatamalizika kabla ya muda uliopangwa.
“Kwa ujumla ni kwamba ujenzi unaenda vizuri ushauri mkubwa ni tuongeze kasi ya utendaji kazi na hasa kununua mahitaji ya vifaa kwa ujumla na wafanyakazi waongezwe itaweza kusaidia kwenda kwa kasi ambayo viongozi wetu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Waziri MKuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wanatarajia,” alisema Dkt. Jingu.
Aidha alieleza kwamba ni azima ya serikali kuhakikisha Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya Nchi linakuwa na miundo mbinu yenye ubora na imara kama ilivyokuwa ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Nchi.
Naye Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe alibainisha kuwa ujenzi unaoendelea ni wa wizara 26 na majengo 26 ukiwa umefikia hatua mbalimbali akisema umefikia asilimia 28 hadi asilimia 54.
“Kwa mfano ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora umefikia asilimia 54, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na Wizara ya Katiba na Sheria umefikia wastani wa silimia 35 kazi hii inaenda vizuri na inatarajiwa kumalizika katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni hadi Oktoba mwaka 2023 kwa ujenzi wa jumla lakini baadhi ya majengo yatakamilika kuanzia Machi 2023,” alieleza Katibu huyo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi kutoka SUMA JKT Mhandisi Hagai Mziray aliahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu ya kuhakikisha wanaongeza vifaa na kasi ya ujenzi kufikia Aprili 2023 ujenzi uwe umekamilika.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.