SERIKALI imefanya uwekezaji
mkubwa na maboresho katika sekta ya Afya yanayokwenda sambamba na uwepo wa
rasilimali watu itakayotoa huduma zenye ubora ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Mipango ya Rasilimaliwatu katika sekta ya Afya Bw. Issa
Mmbaga kutoka Wizara ya afya wakati wa mawasilisho yaliyohusu upatikanaji wa
rasilimali watu katika sekta ya Afya, kwenye kikao cha wataalam kilichofanyika
Jijini Dodoma.
Bw. Mmbaga alisema kuwa,
baadhi ya maboresho yaliyofanywa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita katika
sekta hiyo ni pamoja na ujenzi wa hosptali mpya, ongezeko la vifaa tiba na
kuboreshwa kwa miundombinu iliyopo katika eneo la huduma.
“Maboresho haya yamesababisha
mahitaji ya ziada ya watumishi katika sekta hii hivyo serikali ina mikakati
maalum ya kuhakikisha kunaupatikanaji wa kutosha wa wataalam ili kuwa na sekta
ya afya yenye nguvu na uwezo wa kutoka huduma bora za afya”. Alisema Bw.
Mmbaga.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Sera na Program Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.
Crispin Musiba, amesema kuwa, uzalishaji wa madaktari na wataalamu wengine
katika sekta ya Afya umekuwa mkubwa zaidi kiasi kwamba, idadi kubwa ya wataalam
hao wapo nje ya ajira.
“Kwa hivyo ili kupunguza
muonekano wa wataalam hao kuwepo nje ya Ajira, tumeita kikao hiki ili kuweza
kuwa accommodate wataalam hao katika kupata ajira, na kikao hiki kimetoka na
maazimio nane (8) ambayo tumepeana muda wa mwezi mmoja ili yaweze kukamilishwa
na kuwasilishwa katika ngazi za juu.” Alisisitiza
Naye Mkurugenzi wa Afya kutoka
Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapalagwe alisema, ipo haja ya kuendelea kuwa
na program za elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii hususan
katika masuala ya huduma za kiafya ikiwemo zile za kibingwa zinazotolewa pamoja
na kuwa na mikakati madhubuti ya tafiti mbalimbali zitakazoweza kusaidia kujua
rasilimali iliyopo katika masuala ya afya.
“Maendeleo yaliyopo katika
sekta ya afya, hayatazaa matunda ikiwa hatutaendelea kutoa elimu kwa umma kwa
upana wake na kuwa na mikakati ya makusudi inayolenga kuboresha kada
hii,”alisema Dkt. Ntuli
Kikao Hicho kilihusisha
wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Utumishi,
Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu.
=MWISHO=
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.