KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala
ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka watendaji wa Mikoa, Wilaya
na Halmashauri kusimamia vizuri utekelezaji wa Programu ya Kilimo na Uvuvi
katika maeneo yao kwani ni sekta muhimu katika uchangiaji wa uchumi na usalama
wa chakula nchini.
Ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma, katika warsha
ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa
watendaji wa Mikoa na Halmashauri.
Dkt. Yonazi amesema kuwa Serikali imeona kuna ulazima wa
kuwepo kwa usalama wa mbegu katika kilimo hivyo kupitia Wakala wa Mbegu za
Kilimo nchini ASA imeweza kuwekeza mbegu kwa wingi ili kuyafikia maono ya
serikali.
“Serikali imeendelea kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa
mbegu bora ambapo hadi kufikia Aprili 2023, jumla ya tani 49,962.35 za mbegu
bora zimepatikana sawa na asilimia 26.68 ya mahitaji ya tani 187,197 kwa
mwaka,”alisema Dkt. Yonazi.
Aliongezea kuwa, serikali imejitahidi kuweka nguvu katika
upatikanaji wa mbegu hizo ili kuhakikisha
uwepo wa usalama wa chakula nchini, na kwa upande wa sekta ya uvuvi
imehakikisha kunakuwa na manufaa ya rasilimali zilizopo katika sekta hiyo kwani
bado hazijatumika vizuri.
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ina mpango wa kununua
meli zitakazotumika katika uvuvi wa kina kirefu cha bahari na hivyo kuweza
kuongeza lishe na hatimaye nchi kunufaiika na rasilimali za uvuvi.
Aliendelea kufafanua kuwa, Programu hii pia, itahusisha
ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na upanuzi wa
vituo vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki cha Kingolwira Morogoro.
“Lazima tushirikishe wadau ili tupeleke elimu ya kuweza
kuzalisha vifaranga na kujenga mabwawa, natoa msisitizo kwa viongozi wa mkoa
kuwa kuna jukumu la usimamizi, tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi huu,
kushauri na kuutekeleza kwa wakati.” Alisisitiza Dkt. Yonazi
Awali, akiongea wakati wa Ufunguzi wa Warsha hiyo Bw. Paul
Sangawe Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, alisema lengo la programu hii kwa
upande wa sekta ya uvuvi, ni kuendeleza ufugaji wa viumbe maji pamoja na kuanza
uvuvi wa bahari kuu.
“Tunatazamia katika program hii meli zitanunuliwa kwa
matumizi ya pande zote mbili za Muungano na kuwezesha nchi yetu kwa mara ya
kwanza kufanya uvuvi katika bahari kuu ili kuweza kutumia rasilimali tulizonazo
kwa ufanisi, lakini vile vile uzalishaji wa mbegu pamoja na usambazaji, na
kuhakikisha fedha ambazo za mkopo ambazo tumepewa kutoka shirika la IFAD
takribani dola 58.8 milioni,zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija katika
utelezaji wa program hii.” Alisisitiza
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchumi na
Uzalishaji toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Afisa Kilimo Mkuu Dkt. Rehema Mdendemi
amesema programu hii ya maendeleo ya kilimo na uvuvi itaenda kuboresha maisha
ya wakulima na wavuvi , na kujitosheleza kwa usalama wa chakula na kuleta ajira
hivyo program hii ni ya muhimu kwa serikali na wanachi kwa ujumla.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.