Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu amewakumbusha
watumishi wa ofisi yake kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara
ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuyafikia
malengo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo
wakati akifungua kikao chake na watumishi wa ofisi hiyo kilichofanyika Jijini
Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu huyo
amesema upo umuhimu wa kujizoeza kupima afya hususan kwa magonjwa sugu
yasiyoambuiza kwani yameendelea kuwa changamoto hasa kwa watu wenye umri
mkubwa.
“Ni muhimu tumepata
fursa ya kukumbushwa kupima afya zetu, hii ni changamoto inayotukabili, hivyo
ni muhimu kuzingatia ushauri wa afya na masharti ya namna ya kuboresha masuala
yanayohusu afya zetu, “alisema Dkt. Yonazi
Pamoja na hilo
aliwakumbusha watumishi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuendelea
kutekeleza majukumu wakiwa wenye afya na kuwa na matokeo chanya.
Aidha aliutumia
mkutano huo kuwaasa watumishi hao kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu
yao ya kila siku huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa
umma.
“Mkutano huu ni sehemu
ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo tulianza kuiadhimisha tarehe
16 Juni, 2023 na leo ndio kilele.Wiki hii tunaitumia kutafakari namna
tunavyotekeleza majukumu yetu kwa kipindi kilichopita, kujadili namna ya kutoa
huduma bora kwa jamii ya Watanzania, kujifunza mbinu mpya na kuibua changamoto
zinazotukabili katika kutekeleza majukumu yetu kwa lengo la kuzitafutia
ufumbuzi,”alisisitiza
Pia aliwahimiza
Watumishi kuendela kufanya kazi kwa upendo na kuheshimiana kwani kwa kufanya
hivyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani.
“Ni falsafa yangu
kuona watu ninaowaongoza wanafanya kazi kwa upendo na kushirikiana, ni lazima
kuhusiana na kuwa na mashirikiano mazuri, napenda kufanya kazi na watu
wanaoheshimiana na wenye amani siamini kama mtu anaweza akafiri vizuri iwapo
hana amani ndani”alisisitiza Dkt. Yonazi
Akitoa neno la shukrani
Mwenyekiti ya TUGHE wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Numpe Mwambenja alipongeza
uwepo wa mkutano huo huku akieleza kuwa ni nyenzo muhimu kwa kuongeza motisha
kwa watumishi wa umma, na imeonesha kujali na kuendelea kuleta umoja kazini.
“Mkutano huu umekuja
wakati sahihi na muda sahihi, tunawapongeza viongozi wetu kuendelea kutuweka
pamoja na kutukumbusha kupendana, kushirikiana na kuishi kwa amani, hili
tumelithamini sana na tunaahidi hatuta waangusha tutachapa kazi na kuendele
kuhudumia jamii ya Watanzania na kuitumikia nchi yetu kwa ujumla,”alisema
Numpe.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.