Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba
na Sheria imeipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na
Uratibu kwa Usimamizi mzuri wa kukabiliana na Maafa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama
wakati wa wasilisho lililohusu namna Serikali ilivyojipanga katika
kukabiliana na maafa pamoja na mfumo wa usimamizi wa Uratibu wa maafa
katika kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na Utekelezaji wa Mpango wa
Ujenzi wa Vituo vya utoaji huduma za matibabu kwa waraibu wa Dawa za kulevya
nchini lililowasilishwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na
Uratibu Mhe. Jenista Mhagama leo Bungeni Jijini Dodoma.
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ilifanya
kazi kubwa nayakupongezwa kutokana na jitihada zilizofanyika kuhakikisha
waathirika wa mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanag mkoani Manyara
wanaokolewa na kurejesha hali.
“Tunapongeza sana Uongozi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kazi mliyofanya ni kubwa ya kuokoa maisha ya
wananchi na mal zao licha ya baadhi yao kupoteza maisha kama kamati
tunawapongeza sana,” Alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mhe. Dkt. Mhagama alisema, inatia moyo sana
kuona Wizara ama idara inazozisimamia zinafanya kazi ambazo watanzania
wanazitarajia kwa hiyo kamati nayo inajiskia kama ni sehemu ya hayo mafanikio
makubwa yaliyopatikana.
“Maafa ni majanga lakini tunapokabiliana nayo
na kuyafanyia kazi vizuri inatupa nguvu sasa, tunapenda tukupongeze Mhe. Waziri
Jenista Mhagama, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi na Watendaji wako wote kwa
moyo wa uzalendo mliouonyesha katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilipitia,”
Alieleza Mhe. Dkt. Mhagama.
Vilevile Kamati pia ilipongeza Mamlaka ya
Kudhibiti na Kukabilana na madawa ya kulevya kwa kazi nzuri inayofanya ya
kujenga vituo vya Uraibu na kushauri kujengwa vituo zaidi kwa Mikoa ya kusini
pamoja na kuendeleza mapambano ya uzalishaji na biashara ya Dawa za kulevya
kama vile Bangi,Mirungi na dawa nyingine.
Akitoa maoni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Edward Olekaita Kisau, alifafanua
kwamba namna Serikali ilivyokabiliana wakati wote wa maafa na baada ya maafa
ili kuhakikisha inarejesha hali na shughuli kuendelea kama ilivyokuwa awali na
janga la Hanang’ ni mfano mzuri unaoweza kuchukuliwa katika uratibu mzima wa
masuala ya kukabiliana na majanga nchini.
Naye Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Dkt
Alice Kaijage akitoa maoni kuhusu wasilisho la Utekelezaji wa Mpango wa
Ujenzi wa Vituo vya Utoaji wa Huduma za Matibabu kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya
nchini alibainisha kuwa ni wakati mzuri sasa kwa Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) kuongozewa fedha za maendeleo
kwani kazi inayofanywa na mamlaka hiyo ni kubwa na kuleta matokeo chanya kwa
Taifa.
Awali akiwasilisha taarifa hizo mbele ya
kamati hiyo Waziri wa Nchi Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama Alisema
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kutoa elimu
kwa jamii kupitia majukwaa mbalimbali kwa lengo la kuijengea uelewa na
uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kupunguza madhara yanayotokana na
maafa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya
Menejimenti ya Maafa imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa maafa kwa Kamati
za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na vifaa, Serikali imefanya manunuzi na kuratibu
upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya msaada
wakati wa dharura na kuvihifadhi katika maghala ya kuhifadhia vifaa vya misaada
ya kibinadamu ili kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na maafa,” Alieleza
Mhe. Jenista.
Aidha Waziri huyo alitoa wito kwa
wananchi kutokudharau utabiri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) kwani mamlaka ina vifaa vinavyoendana na teknolojia ya kisasa
ambapo utabiri wa hali ya hewa kwa wakati huu, umekuwa na una
usahihi wa asilimia 85% mpaka 95%.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.