Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Tafara ya
Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro kuwa shughuli zote za Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba,
2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 zitaendelea kama ilivyokuwa awali
kwa kuzingatia taratibu na mipaka ya Vijiji na Vitongoji iliyokuwepo awali
kwenye maeneo yao.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Kijiji cha Oloirobi, ambapo amewataka wananchi hao kuondoa hofu na
wasiwasi badala yake kuendelea kuishi kwenye maeneo yao kwa amani, kwa kuwa
nchi yao ya Tanzania ni Nchi ya amani na utulivu, inayowajali wananchi wake,
kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na usawa.
Akiwasilisha ujumbe huo,
amesema kuwa, Mhe. Rais amepokea kero na malalamiko kutoka kwa Viongozi na Vyombo
vya habari na kuwaagiza askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
kutowanyanyasa wananchi pamoja na kuheshimu Mamlaka za Serikali za Mitaa
zilizopo, kwani Mhe. Rais Samia bado anatambua uwepo wa Serikali za Vijiji na Vitongoji
vya maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro.
Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa
Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda licha ya kuwashukuru wananchi kwa uvumilivu na imani
yao kwa Serikali, amemuhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atasimamia maelekezo yote
yaliyotolewa kwake, akiahidi pia kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizokuwa
zimesimama ama kusuasua hasa katika Sekta ya Afya na Elimu zinarejea katika
ubora wake na kwa viwango vinavyohitajika.
Katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi
ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula pamoja na Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania CP Awadh Juma Haji
pamoja na Viongozi wengine wa Serikali na wa Chama Cha Mapinduzi CCM.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.