WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.
Amesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi atakuja mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyarudishwa Serikalini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Desemba 17, 2016) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru na wananchi wa kijiji Bwawani na kitongoji cha Mapinu katika kata ya Nduruma akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.
“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema.
Amesema Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..
"Ninataarifa kwamba hapa Arumeru kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza. Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya umiliki. Hatutawavumilia,” amesema.
Amesema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo.
“Kuanzia leo marufuku Jeshi la Polisi kutumiwa na mtu binafsi kuwanyanyasa wananchi. Mtafanya hivyo kama kuna uvunjifu wa amani na si vinginevyo,” amesema.
Awali, akisoma taarifa ya wilaya mkuu wa wilaya ya Arumeru Bw. Alexander Mnyeti alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji ambayo hayajaendelezwa. Mkuu huyo wa wilaya amesema kitendo cha kutoyaendeleza mashamba hanayo kisababisha wananchi kuyavamia hali inayochangia kushamiri kwa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo. Amesema tayari ofisi yake imefanya uhakiki wa mashamba hayo na kumuomba Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli kufuta hati za mashamba 12 ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali imepeleka sh. bilioni 800 katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akizindua nyumba ya walimu na vyumba vinne vya madarasa katika shule ya sekondari ya Orjolo, hatua ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kufanyiakazi na kupunguza changamoto ya makazi kwa walimu.
Amesema changamoto ya makazi imekuwa ikiwakabili walimu kwa mrefu hivyo Serikali imeamua kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo zinawezesha familia sita kuishi pamoja. Pia amewataka wazazi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule na kuhakikisha wanafuatilia miendendo ya elimu kwa watoto wao.
“Tumeondoa ada na michango yote iliyokuwa inawakera na kusababisha mshindwe kuwapeleka watoto shule. Jukumu lenu kwa sasa ni kufuatilia mienendo ya watoto wenu hadi kwa walimu ili kuhakikisha wanaingia darasani na wanasoma,” amesema.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk, Wilson Mahera alisema mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari ya awamu ya pili (SARPCCO II) umewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,vyoo 20 pamoja na vyumba vya madarasa 6 vyenye jumla la Sh. milioni 289.52.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.