WAZIRI
MKUU Kassim Mjaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 15 kwa ajili ya kutoa
mafunzo kwa vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo waweze kushiriki kama nguvu
kazi kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.
Alitoa
kauli hiyo jana usiku (Alhamis, Desemba 8, 2016) kwenye sherehe za utoaji wa
tuzo ya muajiri bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo zimeandaliwa na
Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Waziri
Mkuu alisema Serikali imeanza kujielekeza katika kutoa mafunzo kwenye sekta za
kipaumbele kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kama kilimo biashara,
mafuta, gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za ngozi.
Alisema
jitihada zinaendelea kwenye maeneo mengine ili waajiri wawe na wigo mpana wa kuwapata
wafanyakazi wenye stadi stahiki kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wao kuwa
nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri mkubwa kwa lengo la kuongeza tija.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia changamoto inayolalamikiwa
na waajiri ya uwepo wa tozo mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka tofauti za
Serikali kwa huduma ileile kuwa wanaitambua na tayari mchakato wa kuainisha
sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara
nchini.
“Lengo
letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze
kuvutia zaidi na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi katika kuendelea kuziainisha sheria
zinazokwaza biashara ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,” alisema.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwashauri waajiri wote nchini waendelee kufanyakazi zao
kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi. Pia
aliwasihi wafanyakazi wote kufanyakazi kwa bidii na uaminifu mkubwa ili waajiri
waweze kupata faida, hivyo kuwaboreshea maslahi yao.
Alisema
“tunaposema Hapa Kazi Tu, tunamaanisha kazi kwenye sekta zote za uzalishaji na
utoaji wa huduma bora nchini, iwe sekta ya binafsi au kwenye utumishi wa umma.
Nawasihi ndugu zangu Watanzania, wekeni nadhiri kwamba katika mwaka 2017
mtafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na ufanisi mahala pa
kazi,”.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista
Mhagama aliwaomba waajiri wawasaidie kuweka msukumo katika juhudi za
kutoa mafunzo kwa ajili ya uzoefu na kuongeza ujuzi kwa kutoa nafasi kwa
wahitimu kupata uzoefu kwenye maeneo yao ya kazi.
Hata
hivyo Mheshimiwa Jenista alisema anatambua umuhimu wa waajiri na
wafanyakazi katika utekelezaji wa sera
ya maendendeleo ya nchi hasa kwa kuongeza ajira kupitia sekta ya viwanda kwa asilimia
40 kufikia mwaka 2020, mafanikio ya mpango huo yanategemea mchango wa waajiri
kutoka sekta binafsi.
Pia
aliwapongeza ATE kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu hasa
kwa kutoa tuzo katika eneo la kuendeleza vipaji, ambapo aliwaomba tuzo ijayo
waongeze kigezo cha kumpata mwajiri aliyetumia rasilimali zake kuongeza ujuzi
kwa wafanyakazi wake ambao ndio chanzo cha kuinua tija na ushindani kibiashara.
“Natambua
kuwa ATE mnatoa mafunzo katika sheria za kazi na usimamizi wa rasilimali watu
ambayo husaidia kupunguza migogoro mahali pa kazi na hivyo kujenga mazingira
tulivu maeneo ya kazi. Naomba kutumia wasaa huu kuwakumbusha waajiri
kuwawezesha wafanyakazi kwenda kuhudhuria mafunzo mbalimbali ili kuweza kukidhi
ushindani katika mazingira ya biashara,” alisema.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji wa
tuzo hiyo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimali
watu katika taasisi na makampuni mbalimbali mwanachama hapa nchini.
Alisema
kuwa tuzo hizo zinafuata mbinu za Kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu
wa Rasilimali watu katika makampuni ya Kibiashara makubwa na madogo na yale ya
kati ili kuinua ujuzi wa wafanyakazi wanaofanya kazi kwa kujituma sehemu za
kazi.
Dk.
Mlimuka alisema kuwa tuzo hio pia ilijikita zaidi katika kuangalia maeneo
muhimu ya rasilimali watu, uongozi, utawala, usimamizi wa Rasilimali watu,
kusaidia jamii pamoja na kuwajibika katika jamii, ubora na uzalishaji.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.