*Asema wanaotaka fedha wataipata
shambani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
wakazi wa Ruangwa na mkoa mzima wa Lindi wachangamkie fursa ya kulima mihogo na
alizeti kwa sababu mazao hayo yana uhakika wa soko.
Alitoa wito huo wakati akizungumza na
wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako
anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri
Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Nimekuja
na fedha, wangapi wanataka kupata fedha?” alihoji Waziri Mkuu katika mikutano yake
na kuitikiwa “Sisi” na umati wa watu walionyoosha mikono juu kuonesha kuwa wako
tayari kupokea fedha hizo. Mikutano hiyo ilifanyika kwenye vijiji vya Namilema,
Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi, Chibula na Matumbu.
“Mnataka
fedha siyo? Fedha iko shambani! Nimewaletea fursa ya mwekezaji anayetaka
kununua mihogo yote katika mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu na kusababisha
kicheko kwa watu waliokuwa wakinyoosha mikono yao.
“Limeni
mtu mmoja mmoja au jiungeni kwenye vikundi ili mpate ekari tatu hadi nne kwa
sababu mna uhakika wa soko. Mwekezaji huyu anataka kununua mihogo yote na ya
wilaya hii peke yake haitoshi kiasi ambacho anataka. Kwa hiyo tumekubaliana na
wabunge wenzangu kwamba kiwanda hiki kitajengwa Nanjilinji ambako ni katikati
ya mkoa ili iwe rahisi kusomba na kupeleka mazao hayo,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema eneo la Nanjilinji lililoko wilayani Kilwa, linafikiwa kwa urahisi
na wakazi wote kutoka Kilwa, Nachingwea, Ruangwa, Lindi Vijijini na Liwale.
Akifafanua
zaidi, alisema mwekezaji aliyepatikana (bado ni mapema kumtaja) yuko tayari
kufuata mazao waliko wakulima na atakuwa akiwalipa hukohuko. “Yeye anachotaka
ni mihogo ya kutosha, ndiyo maana nawasisitizia muanze kulima zao hili kwa
wingi cha msingi mfuate kanuni bora za kilimo,” aliongeza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amewataka wakazi hao walime zao la alizeti kwa wingi kwa sababu
amekwishapatikana mwekezaji wa kununua zao hilo na kwa bei nzuri.
“Nilipokwenda
Singida nilikutana na mmiliki mmoja wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti
akasema anahitaji kununua zao hilo kwa wingi kwa sababu inayozalishwa kule haitoshi.
Ameshakuja hapa na kuangalia ardhi ya hapa amesema inafaa kwa zao hilo,”
alisema.
“Yeye
atawaletea mbegu na kila ekari moja inahitaji kilo tano. Ukivuna kila ekari
unapata magunia 20 na kila gunia lina uwezo wa kutoa lita 20. Bei ya dumu
mojala lita 20 ni sh. 60,000 kwa hiyo katika ekari yako moja una uhakika wa
kupata sh. milioni 1.2. Hata ukitoa gharama ya kulima na palizi, bado huwezi
kukosa walau sh. milioni moja kwa kila ekari.”
Alimwagiza
Mkuu wa Idara ya Kilimo (Umwagiliaji na Ushirika) wa wilaya hiyo, Bi. Violeth
Byanjweli afanye kazi ya kuratibu ni wakazi wangapi wana mashamba ya alizeti na
wangapi wako tayari kuanzisha kilimo hicho ili mbegu zitakapoletwa iwe ni
rahisi kuwasambazia huko waliko.
“Hiki
kilimo ni cha miezi mitatu tu na palizi yake ni mara moja tu. Kwa hiyo mvua za
Januari zikianza, changamkieni hiyo fursa na baada ya miezi mitatu kila mtu
atakuwa na hela yake badala ya kusubiria korosho ambazo mnavuna mara moja kwa mwaka,”
alisisitiza.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.