*Asema
kama tabia hiyo ilikuwepo, mwisho wake ni jana
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini
kuacha kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.
Badala yake
amewataka waandae mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za
mfuko wa Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za
maendeleo jimboni.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na
viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa
huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa ya Songea.
“Nimepata
taarifa kuwa fedha za maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana.
Msiwape fedha mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama
mlikuwa na matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” amesisitiza.
“Fedha
za mfuko wa Jimbo ni za Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye
Halmashauri na yeye anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na
madiwani wenzake ni miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa
imekwishaidhinishwa na vikao husika,” ameongeza.
Alisema
makusanyo ya fedha yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na
jinsi fedha hizo zinavyotumiwa. “Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi
gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani. Suala la
matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi ya
maendeleo,” amesisitiza.
Amesema kuna baadhi
ya watu wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia
kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building). “Hii si
sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa
kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,”
ameongeza.
Akizungumzia
kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu amewataka waangalie
baadhi ya makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini
wanatumia software ambazo
zinawanufaisha na wao pia.
“Tumieni watu
wenu wa TEHAMA kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile
mashine siyo waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna
mianya ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia
kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao.
Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni
kuchunguza na mjiridhishe na hizo software
zao,” amesisitiza.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.