WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ili kuongeza udhibiti wa sekta ndogo ya fedha.
“Kwa muda mrefu sekta ndogo ya fedha haikuwa na udhibiti wa kutosha. Hali hiyo ilisababisha kuwepo na uendeshaji usio rasmi wa shughuli mbalimbali za kifedha kama vile, taasisi zinazochukua amana, vikundi vya fedha vya jamii na wakopeshaji binafsi,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.
Amesema shughuli hizo ambazo nyingi ziliendeshwa katika utaratibu usio rasmi, ziliwaletea wananchi athari mbalimbali ikiwemo kupoteza mali zao zilizowekwa kama dhamana kwenye taasisi hizo.
Amesema baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya wa kutokuwepo udhibiti wa kutosha kwenye sekta hiyo ndogo ya fedha kuendesha vitendo mbalimbali vya kihalifu ikiwemo utakatishaji fedha.
“Kutokana na sababu hizo, Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kuongeza udhibiti wa sekta hiyo ndogo ya fedha na kuiwezesha kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kulinda mali na fedha za wananchi wetu,” amesema.
Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) ambao umesomwa kwa hatua zake zote na kupitishwa na Bunge, ukisubiri kibali cha Mheshimiwa Rais ili uwe sheria kamili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hali ya usalama barabarani bado ina changamoto nyingi licha ya takwimu kuonesha kupungua kwa matukio na vifo vinavyosababishwa na ajali hizo.
Akitoa mfano kuhusu matukio ya ajali nchini, Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016 matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 9,856 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika mwaka 2017 ambayo ni pungufu kwa matukio 4,278 sawa na asilimia 43.
Akifafanua zaidi, amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2018, matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 3,209 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana.
Amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matukio ya usalama barabarani ikiwemo kuendesha operesheni za kuhakikisha sheria zote za usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.