*Awaagiza viongozi wa mikoa nchini wabaini fursa walizonazo na wazitangaza
WAZIRI MKUU amewaagiza viongozi wote wa mikoa nchini wahakikishe wanashirikiana na makundi yote kuzibaini fursa zilipo katika maeneo yao, kuziorodhesha na kuzitangaza kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya biashara na uwekezaji ili zipate wawekezaji haraka
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Novemba 21, 2018) wakati akizindua
Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji la Mkoa wa Tabora, ambapo ameagiza fursa zote ziandaliwe na kuandikwa vizuri ili wenye mitaji kutoka ndani na nje waweze kuziona na kuja kuwekeza.
Pia Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Tabora na watendaji wote wa Serikali wawajibike kwa wananchi kwa kusikiliza kero zao na kizitatua kero zote zinazochelewesha biashara na uwekezaji katika maeneo yao.
Kadhalika Waziri Mkuu amezitaka idara zote za Serikali katika ngazi za mikoa na wilaya zishirikiane na kubununi njia rahisi zitakazosaidia kuzijua fursa zilizopo kwenye maeneo yaona kuzitangaza ili kusaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana wanaomaliza shule, vyuo na vyuo vikuu kwa kujiajiri wenyewe.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili Taifa lifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. “Viwanda vinalenga kutengeneza ajira nyingi kwa akina mama na vijana na kuiwezesha Serikali kupata fedha za kigeni zitokanazo mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi .”
Waziri Mkuu amesema fedha hizo za kigeni ni muhimu sana katika kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo kama ile inayoendelea sasa ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Stiegler’s Gorge, miradi ya usafirishaji umeme na mingineyo.
“Ubunifu na mipango ya namna hii inayotekelezwa na Mkoa wa Tabora inakwenda bega kwa bega na dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa na watendaji wengine wote wa Serikali katika kuhakikisha tunafikia uchumi wa viwanda.
Kadhalika, sote tumesikia fursa zilizopo Mkoani Tabora zikiwemo maliasili kama vile misitu, mbao, uzalishaji wa asali pamoja na kilimo cha tumbaku, pamba, alizeti na shughuli nyingine nyingi za ujasiriamali mdogo na wa kati.”
Pia, Waziri Mkuu ametaja fursa mpya zinazojitokeza mkoani Tabora ambazo ni bomba la mafuta ghafi linalotoka HOIMA nchini Uganda kwenda Tanga ambalo litapita mkoani humo pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
Amesema hizo ni miongoni mwa fursa zitakazousaidia mkoa wa Tabora ujulikane zaidi, hivyo kuibua uhitaji wa uwekezaji zaidi katika shughuli za kibenki, hoteli, huduma za mikutano na starehe, maeneo ya michezo, shule na shughuli nyinginezo. “Mambo yote haya yataibua fursa lukuki za uwekezaji mkoani Tabora.”
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande mwingine inaendelea na jitihada kubwa za kuunganisha mikoa yote na mtandao wa barabara za lami ukiwemo mkoa wa Tabora kwa kuwa kuimarika kwa miundombinu usafirishaji ndani na mikoa ya jirani, kutatoa fursa nzuri katika kuifungua Tabora na kuleta mwelekeo mpya wa kiuchumi na kijamii.
“Nitoe rai kwa uongozi mzima wa Mkoa wa Tabora kuendeleza kazi hii nzuri mnayoifanya kwa wana Tabora na msirudi nyuma. Endeleeni kuwa wabunifu zaidi, shirikisheni makundi yote ya kijamii ili kupanga na kutekeleza mambo haya kwa pamoja.
Hakikisheni mnatoa kipaumbele kwa akina mama na vijana katika kuwasaidia mitaji na elimu kwa lengo la kuinua na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Kufanya hivyo, mtawezesha jamii inayowazunguka kunufaika haraka na mipango yenu ya maendeleo.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kazi nzuri inayofanya ambapo tayari wameshakwenda mikoa saba nchini Tanzania Bara na Zanzibar wakisaidia kuziibua fursa, kuziandika kwenye vyombo vyao na pia kuzitangaza kupitia majukwaa hayo wanayoyaandaa, ambayo yamesaidia sana kupata wawekezaji mbalimbali. Mkoa wa Tabora ni mkoa wa nane.
“Niwaombe TSN mshirikiane na mikoa mingine kuandaa na kuhimiza majukwaa haya ya fursa za biashara na uwekezaji. Ni matumaini yangu kuwa kila baada ya jukwaa kama hili kutafanyika tathmini za kina ili kupima matokeo yaliyotarajiwa.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa TSN baada ya kukamilisha majukwaa katika ngazi za mikoa waangalie uwezekano wa kuandaa majukwaa kama hayo kwenye ngazi za wilaya na kisekta, ambapo ametolea mfano sekta za kilimo, madini, ufugaji au ujasiriamali ili wasaidie kuziibua na kuzitangaza fursa zilizopo kwenye sekta hizo kama wanavyofanya sasa.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.