WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaomba waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo
nchini wahakikishe nyumba zao za ibada hazitumiki kuleta migogoro.
Ametoa
ombi hilo jana usiku (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na
mamia ya waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu pamoja na viongozi wa
dini walioshiriki ibada ya futari wilayani Chato, mkoani Geita.
Akizungumza
na waumini hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli,
Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais alishapanga kufika Chato ili
kushiriki nao ibada ya iftar lakini ametingwa na majukumu ya kitaifa akaona ni vema amtume yeye ili amwakilishe.
“Mheshimiwa
Rais alishapanga kuja Chato kufuturu pamoja na wana-Chato lakini kadri
siku zinavyozidi kwenda anajikuta anabanwa na majukumu mengi ikiwemo
kukutana na wageni wa kimataifa, kwa hiyo akaona ni vema nije
kumwakilisha katika shughuli hii,” alisema.
“Mheshimiwa
Rais anawaombea heri katika siku zilizobakia za mfungo wa Ramadhan ili
mmalize salama na Mungu akijalia muweze kusherehekea pamoja, na pia
anawatakia heri wale watakaoendelea na sita tushawal.”
Akisisitiza
kuhusu amani na utulivu nchini, Waziri Mkuu alisema: “Hatupendi kusikia
kuwa msikiti fulani wamechapana viboko kwa sababu ya kugombea uongozi
au kwenye kanisa fulani waumini wamepigana wakigombea mchungaji wao.”
“Tutumie
nyumba zetu za ibada kudumisha amani na mshikamano wetu. Napenda
niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais John Pombe Magufuli
itaendelea kuheshimu dini zote.”
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini hao kwamba mwezi mtukufu
wa Ramadhan ni wa toba kwa kila muumini. “Huu mwezi mafundisho yake
yanasisitiza amani, uvumilivu na kusameheana. Nipende kuwasihi kwamba
tuendelee kudumisha utulivu tulionao,” aliongeza.
“Nipende
kusisitiza kwenu wana-Geita na wana-Chato kwamba jukumu kubwa mlilonalo
ni kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu amjalie afya
njema, busara na uongozi wa kimungu katika maamuzi yake. Niwasihi ndugu
zangu Waislamu na Wakristo, tuendelee kuwaombea viongozi wote wa kitaifa
kila siku ili wafanye kazi kwa kuongozwa na Mungu,” alisema.
Awali,
akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Chato,
Sheikh Ally Moto alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa
ya kuweza kushiriki ibada ya iftar pamoja na watoto yatima na wajane.
Alisema
wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na
ili kudumisha amani wilayani humo, waumini wa Kiislamu na Kikisto
wameunda Kamati ya Amani ya wilaya hiyo inayojulikana kama Interfaith Committee.
Naye Mbunge
wa Chato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard
Kalemani alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa futari hiyo
ambayo imejumuisha wana Chato kutoka pembe nne za wilaya hiyo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita, Askofu Mussa
Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita
alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli na kuwapongeza viongozi
wakuu wa kitaifa kutokana na utendaji wao unaogusa mioyo ya Watanzania.
“Ninyi
wote watatu ni viongozi ambao Mungu amewaweka kuongoza nchi yetu.
Katika miezi hii 18, mmefanya mambo makubwa, ni imani yetu kuwa
ataendelea kuwaongoza katika utendaji kazi wenu,” alisema.
Akitoa shukrani, Sheikh
wa Mkoa wa Geita, Sheikh Yusuph Kabaju ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza
wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa
fursa wana-Geita kujumuika pamoja katika futari hiyo na kuahidi
kudumisha amani ya Tanzania.
“Tunakushukuru
kwa kutuunganisha wana Geita katika futari hii japo umeamua kufanyia
ibada hii hapa Chato. Maneno ya Quran tukufu yanasema malipo ya
waliofunga anayapata pia yule aliyefuturisha waliofunga,” alisema.
Sheikh
Kabaju pia alisoma dua ya kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli pamoja na
viongozi wa kitaifa. Pia aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Tanzania.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.