NA.MWANDISHI WETU
JAMII
imeshauriwa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini kama wana
maambukizi ya VVU ili kupata huduma mapema na kuchukua hatua muhimu ya
kunendelea kulinda afya za wasio na maambukizi.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu
Mhe.Jenista Mhagama alipokuwa akizindua kituo cha kutolea huduma za tiba
na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa
Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Machi 1, 2019.
Waziri
Mhagama aliwahimiza wananchi kupima VVU ili kufanikisha mpango wa 90
tatu na kutoa hamasa kubwa kwa wanaume kuwa mstari wa mbele katika
kupima afya zao,na wakina mama kisiwe kipimo chao.
“Ili
kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi nchini, asilimia 95 ya
watanzania ambao hawana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI inapaswa
walindwe ili wasiambukizwe na kundi la wanaume wawe mstari wa mbele
kujitokeza kupima afya zao,”alisema Mhagama.
Waziri
aliongezea kuwa ni vyema jamii kuendelea kujilinda ili kuepuka
maambukizi mapya yanayosababisha takwimu za maambukizi nchini kuongezeka
badala ya kupungua.
“Pia
asilimia tano ya watanzania ambao wana maambukizi ya virusi vya
UKIMWI inapaswa walindwe ili asilimia hizo zisiongezeke kutokana na
mpango wa 90 tatu”, alisisitiza Mhagama.
Alisema
pia kwenye asilimia hiyo 90 watakaopima na kukuta wamepata maambukizi
wanapaswa kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ili kuhakikisha
maambukizi mapya yanatokomezwa kabisa hapa nchini.
Aliwataka
wananchi wa eneo hilo kutumia kituo hicho kwa kutunza afya zao na
kuishi kwa furaha kwani kinawahusu wenye maambukizi na wale wanaohitaji
kujua afya zao.
Kwa
upande wake Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti alisema
Mirerani ndiyo sehemu inayoongoza kwenye mkoa huo kwa kuwa na watu wengi
wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kulinganisha maeneo mengine
katika mkoa huo.
Alisema
maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Manyara ni asilimia 2.3 na kwenye mji
mdogo wa Mirerani ni asilimia 16 hivyo eneo hilo pekee ndilo
linasababisha mkoa huo kuwa na asilimia kubwa za maambukizi na kuwataka
wananchi kuchukua hatua za dhati za kupambana kuanzia ngazi ya mtu mmoja
mmoja kwa kuhamasisha kupima na kutumia dawa endapo unagundulika na
maambukizi.
"Huu
ugonjwa umekaa mahali pabaya mno, ningekuwa na jeshi kama lililojenga
ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ningetumia kuzuia
UKIMWI lakini siwezi kufanya hivyo ila niwahimize mjitokeze kwa hiari
kuja kupima katika kituo hiki," alisisitiza Mnyeti.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa kudhibiti UKIMWI, Bw.
Godfrey Simbeye alisema kituo hicho kimegharimu jumla ya shilingi
Milioni 250 ambapo shilingi Milioni 200 ni kwa ajili ya ujenzi wa Jengo
la Kituo na Shilingi Milioni 50, ununuzi wa samani na vifaa tiba na
litahudumia watu 49,802.
Simbeye
ameiomba serikali isaidie mfuko kuhakikisha kinapatikana chanzo cha
uhakika cha upatikanaji wa fedha kwani michango pekee haitoshelezi Mfuko
huu .
Aidha
amewaomba wadau wengine na wafanyabiashara kujitokeza kuchangia katika
mfuko huo kupitia namba ya simu 0684 909090 ili kuendelea kudhibiti VVU
na UKIMWI nchini.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko
alisisitizia umuhimu wa wananchi kushiriki na kutumia kituo hicho
kikamilifu kipima afya zao na kuanza dawa kwa kadri watakavyoelekezwa na
wahudumu wa afya.
Mbunge
wa jimbo la Simanjiro Mhe. James Ole Millya aliishukuru Serikali kwa
kufanikisha ujenzi wa kituo hicho na kuwaasa wananchi kujikinga na
maambukizi mapya ya VVU ili kuendelea kuwa na afya njema na kujiletea
maendeleo yao.
Mwakilishi
wa watu wanaoishi na VVU Wilayani Simanjiro, Wariandumi Kweka alisema
kituo hicho kitawasaidia kwani awali walikuwa wanakwenda umbali mrefu
kufuata huduma hiyo na wengi kukatishwa tamaa na hali hiyo na kuendelea
kuitaka jamii kubadili mitazamo hasi juu yao na kuwapa ushirikiano na
kupinga imani potofu za baadhi ya madhehebu yanayopinga matumizi ya
dawa hizo kwa imani ya kupona bila kutumia dawa za kufubaza virusi
hivyo.
=MWISHO=
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.