WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameunda tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali
ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 hadi mchana huu na
wengine 70 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika
baada ya lori la mafuta kupinduka, mjini Morogoro.
“Hii
tume inaanza kazi leo (Jumapili, Agosti 11, 2019), Hadi ijumaa inipe
taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii
si mara ya kwanza ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi
Watanzani pale gari linapoanguka tusitume kama fursa twende tukaokoe
binadamu waliopo pale”.
Waziri
Mkuu ameunda tume hiyo leo (Jumapili, Agosti 11, 2019), wakati
akizungumza na waombolezaji waliofika katika hospitali ya Mkoa wa
Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao. Niko mbele yenu
nikimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli aliyenituma kuja kuungana nanyi
kwenye siku hii ya huzuni”.
Waziri
Mkuu amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri
jukumu lake kwa sababu ajali imetokea saa mbili asubuhi katikati ya mji,
hivyo tunataka kujua ajalj ilipotokea kila mmoja alitumiza jukumu lake.
Amesema
ajali imetokea karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi na kuna polisi sasa je
hawa wananchi waliopata ajali walienda na madumu ya kuchotea mafuta
inamaana waliamka asubuhi wakijua ajali itatokea. “Najua pale ajali
inapotokea trafiki wana wahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu
walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia.Je lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani”.
Waziri
Mkuu amesema lazima wajiridhishe ndani ya Serikali kama wamewajibika.
“Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake.
Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu.
Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika
kuwapoteza Watanzania”.
Pia,
Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha
kwamba zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu
wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa, Rais Dkt. Magufuli tayari ameshatoa kibali cha
kutolewa fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa
zinazohitajika.
Akizungumzia
kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo
inatangazwa kupitia vyombo mvalimvali vya habari, Waziri Mkuu amesema ni
vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw.
Stephen Kebwe.
“Kwenye
vyombo vya habari tuelewane kwenye takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme
suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini
yake. Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyinginyingi mnajenga
hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa
mtafuteni mkuu wa mkoa”.
Wakati Huo huo,
amesema Rais Dkt. Magufuli alipokea taarifa mapema ya ajali ya lori la
mafuta na kusababisha vifo vya Watanzania 69, ambapo alimtaka aende
mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwasilisha salamu za pole kwa wananchi wa
Morogoro na Tanzania kwa ujumla kufuati tukio hilo la kuhuzunisha.
Waziri
Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawaombea marehemu na majeruhi lakini
pia amawataka wafiwa na wananchi wote wawe watulivu katika kipindi hiki
kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao.
“Mheshimiwa
Rais amehuzunishwa sana na msiba huu ndio maana amenituma nilete ujumbe
huu kwenu.Lakini pia nimekuja na salamu za pole kutoka kwa Makamu wa
Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Jambo hili si dogo ni kubwa kwani
tumepoteza ndugu zetu wengi. Kwa idadi hii kubwa ya ndugu zetu
waliotangulia mbele za haki na wale waliopo kwenye maumivu si jambo la
faraja”.
Waziri
Mkuu amesema wananchi wasipeleke miili kwanza makaburini ili waweze
kupitia na kutambua ndugu na rafiki kwa ajili ya kuwa na kumbukumbu ya
kudumu. “Hali si nzuri ndugu zetu wameungua sana wapo wengine mnaweza
msiwatambue lakini mnaweza kutambua kwa alama. Wapo wengine walivaa
bangili, heleni, mkanda havijaungua”.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kama hawajawatambua Serikali imeweka utaratibu wa
vipomo vya vinasaba, ambapo kumbukumbu hizo zimechukuliwa na wataalamu
wetu wa afya. “Kama ukipita ukishindwa kumuona bado tunakuruhusu
kukupima vinasaba na kulinganisha na vyakwako. Bado haki ya kumpata
ndugu yako iko pale pale madaktari wapo, mitambo ipo tutachukua vinasaba
na kuainisha tutatoa nafasi leo hadi saa 10 kufanya utambuzi”.
Amesema
Serikali inaratibu vizuri jambo hilo lakini kuanzia saa 10 itaruhusu
wale waliotambuliwa kuchukua mwili lakini kama hawajajipanga vizuri
itauzika na kama kuna jina litaliandika na kama hakuna jina wataandika
namba ya vinasaba ili kutoa fursa kwa ndugu siku nyingine waende
wakapimwe na kuoneshwa kaburi la ndugu yao.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.