WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amekerwa na kitendo cha Mamlaka ya Maji wilayani
Maswa kupandisha bili ya maji kutoka sh 5,000 hadi sh. 28,000 jambo
ambalo amesema halikubaliki na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony
Mtaka akutane na wahusika leo.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumalija, wilayani Maswa mara
baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha Msingi cha Kumalija.
“Haiwezekani
bili ikapanda kwa kiasi hicho. Hapo utakuwa unamsaidia mwananchi myonge
au utakuwa unamnyonga. Bili haiwezi kupandishwa kwa asilimia kubwa
kiasi hicho yaani imetoka shilingi elfu tano hadi shilingi elfu ishirini
na nane.”
Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni
ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga
kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na
salama, hivyo upandishaji huo wa bili hauna tija kwa wananchi wanyonge.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu alisema Serikali imetoa sh.
milioni 440 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la upasuaji, ukarabati
wa wodi na duka la dawa, upanuzi wa wodi ya watoto na ujenzi wa wodi ya
wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa, ambapo ujenzi wake
unaendelea.
Alisema
mbali na fedha hizo, pia Serikali imepeleka sh. milioni 881 wilayani
Maswa ambapo kati yake sh. milioni 481 ni kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa kituo vya afya cha Malampaka, kwa ajili ya uboreshaji wa
miundombinu ya kituo cha afya cha Mwabayanda.
Akizungumza
kuhusu elimu msingi bila malipo, Waziri Mkuu alisema kuanzia mwaka 2016
hadi 2019 Serikali imepeleka wilayani Maswa jumla ya sh. bilioni 2.1,
kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa Maofisa
Elimu wa kata na Walimu Wakuu katika shule 28 za msingi.
Pia
Waziri Mkuu alisema Serikali kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 imepeleka
wilayani Maswa jumla ya sh. bilioni 2.7 kwa ajili ya fidia ya ada,
chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule
katika shule 16 za Sekondari.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.