Na; Mwandishi Wetu
Vijana
Mkoa wa Ruvuma wamefurahia fursa ya mafunzo ya ujasiriamali na
usimamaizi wa biashara yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo
yatawawezesha vijana hao kukuza na kurasimisha shughuli zao za
kiuchumi.
Akifungua Mafunzo hayo
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I
Issa alieleza kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali ni muhimu sana na yanalenga
kuwawezesha vijana wanaomiliki biashara wanapata mbinu za kuendeshaji na
kusimamia biashara zao.
“Mafunzo haya ya
ujasiriamali yameleta tija kwa vijana na wameweza kujiajiri kwa kufanya
shughuli mbalimbali za kiuchumi zenye faida,” alisema Issa
Alieleza kuwa vijana
wanapaswa kuchangamkia fursa hizo zinapojitokeza ili waweze kuunganishwa na
fursa za mitaji na mitandao ya huduma za biashara, pia kuwajengea uwezo wa
kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kujiamini na kuweza kuweza kupata faida.
“Vijana mnapaswa kutambua
ninyi ndio nguvukazi ya Taifa, hivyo kuwa wabunifu ni jambo la msingi katika
biashara zenu mkitambua fursa mlizonazo ili muweze kushindana katika biashara,”
alisema Issa
Akibainisha aina ya mafunzo
ya ujasiriamali watakayopatiwa vijana hao yakiwemo masuala ya uchambuzi wa
masoko, dhana ya ujasiriamali, uchambuzi wa mahitaji ya mteja, kutambua
ushindani wa soko, mkakati na uendeshaji biashara, utambuzi wa masoko,
usimamizi wa fedha, vihatarishi vya biashara na namna ya kuvikabili, usimamizi
wa biashara na rasilimali watu, urasimishaji wa biashara na vyanzo vya mitaji.
Aliongeza kuwa Programu hii
ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana itawawezesha kutambua mapungufu
waliyonayo na kutumia mwanya huo kuangalia fursa walizo nazo katika ushindani
wa biashara zao.
“Ni muhimu vijana mkawekeza
katika biashara mnazozimudu kimtaji, kiusimamizi kwa ushindani na kufanya
maamuzi sahii,” alieleza Issa
Alieleza kuwa kila Mkoa una
fursa zinazoweza kutumiwa na wajasiriamali katika kujiendeleza kiuchumi, vijana
wanatakiwa kuchangamkia fursa hizo ili waweze kunufaika kwa njia mbalimbali.
Alifafanua kuwa Ofisi yake
imekuwa ikiendesha mafunzo ya aina hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
ikiwemo Taasisi za Umma, Wadau wa Mendeleo, Sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
“Zaidi ya Vijana 10,000
wameweza kufikiwa na programu mbalimbali za mafunzo ikiwemo Kijana jiajiri,
Ajira yangu, Kliniki ya vijana wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu, mifuko ya
uwezeshaji na watoa huduma,” alisema Issa
Aidha, alitoa shukrani zake
kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuona haja ya kuwekeza kwa vijana kwa kuwapatia
ujuzi ili waweze kujiajiri, kuajiri na kuchangia katika pato la taifa.
Kwa Upande wake, Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Hakimu Mafuru amewahimiza vijana wa Mkoa
huo kuchangamkia fursa za mafunzo kama hayo yanayotolewa na Serikali pamoja na
wadau mbalimbali kwa kuwa yatawawezesha kujitambua na kujisimamia wenyewe na
kuongeza tija kwenye biashara zao.
Mmoja wa Vijana walioshiriki
katika Mafunzo hayo, Bi. Pudencia Msangawale alieleza kuwa mafunzo hayo
yatajibu changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo kama wajisiriamali ikiwemo
masuala ya ujuzi, maarifa, kurasimisha biashara, namna bora ya kuhudumia wateja
na utafutaji wa masoko.
“Ninawashukuru Ofisi ya
Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa elimu
waliyotupatia yametuwezesha kujitambua, kuwa wabunifu, waaminifu na kuweza
kujisimamia katika biashara,” alisema Msangawale.
Mafunzo hayo yanaratibiwa na
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na
Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo yatafanyika katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara
ikiwemo Dodoma ambapo tayari yamekisha fanyika, Ruvuma, Geita, Mwanza, Lindi,
Mbeya, Tanga na Arusha.
MWISHO
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.