*Asema lengo ni kuimarisha shughuli za utalii, kuongeza ajira
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ukarabati wa Hoteli ya Mkoani
ambapo amesema lengo la maboresho hayo ni kuimarisha shughuli za utalii
na kupunguza tatizo la ajira.
Amesema
ili kuhakikisha lengo la Serikali linafikiwa amemuagiza Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Khamis
Mussa Omar ahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuleta
manufaa yaliyokusudiwa.
Ameyasema
hayo leo (Jumapili, Januari 19, 2020) baada ya kukagua mradi huo uliopo
katika wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huo wenye thamani
ya sh. bilioni nne unatekeleza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar
(ZSSF)
Waziri
Mkuu amesema mradi wa ukarabati wa hoteli ya Mkoani ni muhimu katika
kuimarisha sekta ya utalii na huduma za malazi hususani kwa wageni
wanaotembelea kisiwa hicho cha Pemba sambamba na kutengeneza ajira kwa
wanawake na vijana.
“Ukarabati
huu unatarajia kutoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya ajira,
teknolojia, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha ustawi wa wananchi
wetu. Endeleeni kuiamini Serikali yenu.”
Akisoma
taarifa ya ukarabati wa mradi huo, Meneja Uwekezaji wa ZSSF, Bw.
Abdulaziz Ibrahim Idd amesema ukarabati huo ulianza Julai 2019 na
unatarajiwa kukamilika Machi 2020.
Amesema
ukarabati wa jengo hilo ambalo awali lilikuwa la ghorofa moja
umehusisha pia kuongeza ghorofa mbili na kufikia tatu, hali ambayo
italifanya jengo hilo kuwa na vyumba 16 vya kulala kutoka vinane vya
awali vikiwemo viwili kwa ajili ya watu mashuhuri.
Meneja
huyo amesema kuwa mbali na kuongezeka kwa vyumba pia umejengwa ukumbi
wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 100, mgahawa wa kisasa pamoja
na sehemu ya kufulia nguo kwa ajili ya wageni na watu wote watakaohitaji
huduma hiyo.
“Kwa
sasa ujenzi huu umefikia asilimia 80 na unatarajia kukamilika mwezi
Machi mwaka huu. Mradi huu utakapokamilika utakuwa ni moja ya chanzo cha
ajira za kudumu 50, hivyo kuinua uchumi kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla.”
Hoteli
hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifunguliwa
Septemba 1974 na iliendeshwa na Serikali yenyewe kwa lengo la kutoa
huduma kwa wageni na hata wenyeji waliofika Pemba.
Lakini
kutokana na uchakavu wake Serikali ikaamua kusitisha huduma zake na
kuifunga ili kutafuta mwekezaji ambaye ataiendelea. Hoteli hiyo imekuwa
haitumiki kwa kipindi cha takribani miaka 12.
Hata
hivyo, Baraza la Mapinduzi chini ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed
Shein likaamua kuikabidhi ZSSF hoteli hiyo kwa lengo la kuifufua na
kuiendeleza.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.