*Asema si sahihi kuwatoza wazawa kwa fedha za kigeni
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wadau wa masuala ya utalii nchini
wafanye mapitio ya gharama za huduma wanazowatoza watalii na amesisitiza
kuwa si sahihi kuwatoza wazawa kwa kutumia fedha za kigeni au gharama
sawa na wageni.
Aliyasema
hayo jana (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza na wanachama wa
Umoja wa Wenye Mashamba Jozani (UWEMAJO) mara baada ya kukagua miradi
ya umoja huo.
Waziri
Mkuu alisema kuwa kuna baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za kitalii
wazawa wanatozwa gharama sawa na wageni. Hivyo, aliwasisitiza waandae
viwango maalumu kwa ajili ya wazawa ili kuhamasisha utalii wa ndani.
Alisema
ni lazima wadau hao wakatengeneza mazingira mazuri yatakayowavutia
wazawa kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii nchini.
“Kitendo cha kuwatoza wazawa gharama sawa na wageni kitasababisha baadhi
kushindwa kutembelea maeneo hayo.”
Akiwa
katika eneo hilo, Waziri Mkuu alisema amefurahishwa na namna ambavyo
umoja huo unavyotunza mazingira pamoja na viumbe maliasili nyingine kama
kobe, kasa, samaki na hivyo kulifanya eneo hilo kuwa kivutio cha
utalii.
Kadhalika,
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi hao kuendeleza
ushirika wao huo kwa sababu utawawezesha kupata mikopo pamoja na misaada
mingine kama elimu kuhusu kilimo bora.
Waziri
Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha wakulima wananufaika
kutokana na kilimo chao. Aliongeza kuwa ushirika unapaswa kuwa chachu ya
mafanikio, hivyo, amewapongeza wananchi hao kwa kuwa na ushirika imara.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi watumie ipasavyo vyandarua
vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa malaria.
Aliyasema hayo wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Kizimkazi
Dimbani, Wilaya ya Kusini.
Waziri
Mkuu akiwa wilayani humo alishiriki maadhimisho ya Siku ya Afya ya
Kijiji kwa kugawa vyandarua kwa wanawake wajawazito. Wakati akigawa
vyandarua hivyo, alisisitiza umuhimu wa kutumia vyandarua kwa malengo
yaliyokusudiwa badala ya kuvitumia kama uzio katika bustani za
mbogamboga.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.