WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub
Mohammed Mahmoud awachukulie hatua watumishi wote watakaobainika kufanya
ubadhilifu wa fedha za mapato ya Serikali.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma katika ngazi mbalimbali
wajiimarishe katika ukusanyaji wa mapato na wahakikishe fedha zote
zinazopatikana zinaingizwa kwenye mfuko wa Serikali.
Ametoa
agizo hilo leo (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza na
watumishi, viongozi wa mkoa wa Kusini Unguja katika mkutano uliofanyika
kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, eneo la Tunguu.
Waziri
Mkuu ambaye yuko Unguja kwa ziara ya kikazi, amesema ni muhimu kwa
watumishi kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze
kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.
“Mkuu
wa Mkoa usiogope chukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayebainika kula
fedha za mapato ambazo zinatolewa na wananchi kwa njia ya kodi.
Mtumishi wa aina hiyo hafai kuwa mtumishi wa umma.”
Waziri
Mkuu amemtaka kila mtumishi wa umma awajibike katika kufanya kazi kwa
bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao
ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanasimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
Amesema
huduma za jamii kama za afya, maji lazima ziimarishwe nchini na
viongozi wa halmashauri wahakikishe zinapatikana ipasavyo. “Huduma
zikiwa zinatolewa vizuri wananchi hawatolalamika.”
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub alisema halmashauri za wilaya
zimeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kutoa huduma kwa jamiii
kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Kusini ukusanyaji wa mapato
umeongezeka kutoka sh. milioni 241 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi sh.
milioni 524.51 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ongezeko la
asilimia 118.
Alisema,
kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati ukusanyaji wa mapato
umeongezeka kutoka sh. milioni 304.27 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi
kufikia sh. milioni 632.89 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ongezeko
la asilimia 108 ya ukusanyaji wa mapato.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.