Na Mwandishi wetu -
Dodoma
Serikali imesema itaendelea kuongeza jitihada
katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na wizara husika ili kuhakikisha
makundi hayo yanakuwa salama.
Kauli hiyo ilitolewa Mei 12, 2022 na
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakati
akiongoza kikao cha Kamati Elekezi ya Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza
Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma
kikihudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali na wadau
wa maendeleo nchini.
Katibu Mkuu huyo alisema ipo haja ya kuongeza
nguvu katika mapambano hayo kila mdau kwa nafasi yake ili kuongeza jitihada za
utekelezaji wa mpango huo kutokana na kuongezeka kwa vitendo na matukio ya
ukatili katika maeneo mbalimbali.
“Inabidi tuongeze nguvu yaani Serikali, Wizara
za kisekta , Idara,Taasisi, Asasi za kiraia,wadau na vyombo vya ulinzi
katika mapambano haya wote kwa nafasi zetu ili kuongeza kazi ya utekelezaji wa
mpango huu na kufikia hilo lazima tuwe na rasilimali kulinda na kutetea makundi
ambayo yamekuwa yakiathirika kutokana na vitendo hivyo,”alisema Dkt. Jingu.
Pia aliongeza kwamba kwa mujibu wa muongozo wa
maandalizi ya mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023
unaelekeza kutengwa kwa fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za MTAKUWWA huku
akiziomba taasisi na wadau kuona namna ya kuongeza rasilimali kufikia malengo
ya Serikali ya kukomesha vitendo vya ukatili.
“Wenzetu wadau wa maendeleo na Asasi za kiraia
nimewaomba tuongeze rasirimali katika vita hii kwa sababu inahitaji ushirikiano
wa pamoja kwani inamgusa kila mmoja wetu katika jamii zetu itatusaidia kutatua
changamoto zinazokabili juhudi hizi na pia mnaweza kuajiri vijana wenye fani za
masuala ya maendeleo ya jamii au zinazofanana na haya mambo kuongeza kasi ya
mapambano,” alibainisha Katibu Mkuu huyo.
Aidha Mtaalamu wa Masuala ya Usalama wa Mtoto
kutoka Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Bi. Vailet Mollel alieleza
kwamba kwamba wamekuwa wakitoa elimu katika jamii namna ya kudhibiti vyanzo vya
ukatili huku akiahidi kwama shirika hilo litaendelea kuunga mkono Serikali
katika uandaji wa mkakati mpya wa 2022/2027 pamoja na kuratibu kamati za ulinzi
kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Mkoa.
“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali
hatutaishia hapa tulipo na kuwajengea uwezo wataalamu kama jeshi la polisi,
wanasheria, mahakama, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii ili waweze
kukabiliana na vyanzo vya ukatili kama mila kandamizi na desturi kupitia
uanzishaji wa vikundi vya malezi, viongozi wa dini na viongozi wa
kimila,” alifafanua Mtaalamu huyo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.