Monday, July 3, 2017

MIVARF YAWAONGEZEA KIPATO WAKULIMA 56,637 MKOANI KAGERA

Program ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) imewajengea uwezo wakulima 56,637 mkoani Kagera kwa kuwawezesha kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa Benki ya Wakulima ya Ushiriki Kagera (KFCB) Bi. Adelina Kilaja tarehe 17 Mei, 2017 mkoani Kagera, wakati wataalamu wa MIVARF walipotembelea Benki hiyo na kujionea maendeleo yaliyofikiwa na benki hiyo kupitia uwezeshaji kutoka Programu ya MIVARF.

MIVARF imekwamua shughuli za Benki ya (KFCB) na kuwaongezea wigo mpana wa kuwahudumia wananchi kwa wingi zaidi ambapo awali haikuwa rahisi. “Program ya MIVARF umetuwezesha kuhamia katika mfumo wa Tehama ambao umerahisisha utendaji wetu wa kazi kwa kiwango kikubwa Zaidi, alieleza Kilaja”.

Benki yetu wateja wake wengi ni wavijijini, ambao ni Wakulima na Wafugaji hivyo benki imefanikiwa kuwajengea uwezo katika masuala ya Akiba na Mikopo, elimu ya kilimo bora, hii isingewezekana bila uwezeshaji kutoka MIVARF uliowawezesha wakulima hao kujikwamua katika maisha yao na kuwaongezea kipato, alisema Kilaja.  

Aidha, alifafanua kuwa kabla ya program ya MIVARF, benki ya KFCB ilikuwa na wateja wa moja kwa moja 7132 kwa  Desemba 2016 na wateja wa vyama vya Akiba na Mikopo walikuwa 26,874 kutokana na uwezeshaji wa MIVARF idadi ya wateja hao imefikia 56,637 Desemba 2016.

“Asilimia 70 ya wateja wetu tunaowahudumia ni wakulima wadogowadogo ambao hujishughulisha na kilimo cha Maharage na Mahindi kwa wingi. Ili kuhakikisha huduma inakuwa bora MIVARF imewajengea uwezo wafanyakazi wa benki hii na kutuboreshea mfumo wa uendeshaji wa kibenki ambapo benki imeweza kuanzisha huduma za Uwakala za kibenki pamoja na sim banking” Alisisitiza Kilaja.

Akifafanua Meneja wa IBUGA SACCOS Brighton Ferdinand alikiri kuboreshwa kwa huduma za utoaji mikopo katika SACCOS yao na kushukuru Benki ya KFCB kwa mkopo walio wapatia wa milioni 101 ambao umewasaidia kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wakulima Mkoani Kagera katika Wilaya ya Muleba.

Aidha, baadhi ya wanufaika wa Mikopo hiyo wameeleza kuwa kutokana na mikopo waliyoipata kutoka katika vyama vya Akiba na Mikopo wameweza kuendeleza kilimo chao kwa tija na kuongeza kipato hali iliyowezesha kumudu gharama kilimo, biashara na elimu.


Programu ya Mundombinu ya Masoko, Uongezaji thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inagharamiwa na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo likiwa ni kuongeza kipato kwa wakulima na kuchangia katika kuboresha uhakika wa chakula kwa kaya zenye kipato cha chini hasa maeneo ya vijijini.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.