Thursday, July 20, 2017

WAZIRI MKUU AMPA MIEZI MIWILI DED SONGWE KUBADILI UTENDAJI WAKE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa miezi miwili kuanzia leo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe, Bw. Elias Nawera abadili mwenendo wake kiutendaji na ashirikiane vizuri na  Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Samwel Jeremiah.

Amesema Serikali ya awamu ya Tano inawataka watumishi wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kuheshimiana na atakayeshindwa kufanya hivyo hatavumiliwa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Julai 20, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Songwe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.

Amesema watumishi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yaweze kufikiwa. Pia waheshimiane sehemu za kazi na kila mtu azingatie mipaka ya madaraka yake.

"Mkurugenzi hapa hamsikilizi Mkuu wa wilaya anaondoka kituo cha kazi bila ya kuaga na amewagawa wakuu wa Idara. Namtaka afanye mabadiliko ya utendaji wake ndani ya miezi miwili na Mkuu wa Mkoa fuatilia jambo hili."

Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote wasimamie utendaji wa wakurugenzi wa Halmashauri kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.”Serikali hii si ya mchezo. Serikali hii inahitaji watumishi waadilifu wa kuwatumikia Watanzania.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bibi Chiku Galawa amesema wamejipanga kuhakikisha changamoto zote zinazoukabili mkoa zinaboreshwa pamoja na kufikia malengo ifikapo 2020.

Ametaja malengo hayo kuwa ni kuhakikisha mkoa huo unakuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato, kila mwananchi awe na bima ya afya pamoja na kuwa na hospitali katika kila wilaya.

Kuhusu mpango wa Serikali wa kuwa na uchumi wa viwanda amesema tayari wameshaanzisha viwanda vya maziwa, kukamua alizeti ikiwa ni kuunga mkono mpango huo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.