WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi
wa ujenzi wa daraja la mto Lukuledi lenye urefu wa kilomita 30.45 linalounganisha
mikoa ya Lindi na Mtwara na na kusema kwamba
ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Amesema ujenzi wa daraja hilo unatakaogharimu
sh. bilioni 5.4 ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo hasa wa wilaya za
Ruangwa na Masasi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo kilimo na
huduma za kijamii.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumanne, Julai
11, 2017) alipotembelea mradi huo wa ujenzi wa daraja hilo katika kijiji cha
Nandanga alipowasili wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake
ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.
“Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na
mamba walipokuwa wakikatiza katika eneo hilo. Ujenzi wa daraja hili ni muhimu, watu
wengi wa Ruangwa wanavuka kufuata matibabu katika hospitali ya Ndanda, wilayani
Masasi na wakazi wa Ndanda wanavuka kufanya shughuli za kilimo wilayani
Ruangwa.”
Pia Waziri Mkuu amewaomba wananchi wa maeneo
hayo kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo ili
aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kumaliza mradi huo kwa wakati.
Kwa
upande wake Mbunge wa jimbo la Ndanda, Mheshimiwa Cecil Mwambe ameipongeza na
kuishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendele0 na
kubadilisha maisha yao.
Amesema mradi wa ujenzi wa daraja hilo ni faraja
kwa wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa eneo hilo ni makazi ya mamba, hivyo
kukamilika kwake kutaokoa maisha ya watu pamoja na kurahisisha usafiri wa watu
na bidhaa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi
na salama katika vijiji vya Litama, Luchelegwa, Nandanga, Ipingo na Chiapi kuwa
historia baada kuungwanishwa na mradi wa maji wa Mbwinji.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwa
nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Litama, Chiapi, Nandanga, Luchelegwa
alipowasili wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi
ya siku nne Mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza Kampeni yake ya kumtua mama ndoo, hivyo itahakikisha wananchi
katika maeneo yote nchini, hususan ni ya vijijini wanapata huduma ya maji safi
na salama katika umbali usiozidi mita 400.
Ameitoa kauli hiyo baada ya wananchi wa
vijiji hivyo kumueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao
zikiwemo za maji, barabara, umeme, ambapo aliwahakikishia kwamba Serikali
imeshaanza kuboresha huduma hizo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezindua
Zahanati ya Nandanga ambayo imejengwa
kwa fedha kutoka mfuko wa jimbo umegaharimu kiasi cha sh. milioni 73.47 na
kuwahakikishia kwamba Serikali itawapelekea wataalam wa kutosha ili kuwahudumia.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.