*Ni wa Vyama Vikuu vya SHIRECU, NYANZA
*Waziri Mkuu ataka wampe maelezo ya kina upotevu wa mali za mabilioni
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa
ya Shinyanga (SHIRECU) na Mwanza (NCU) kwenda selo na badala yake amewapa siku
23 wampe maelezo yatakayomridhisha juu ya mahali zilipo mali za vyama hivyo
viwili.
Amefikia
uamuzi huo leo (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati akifunga kikao cha siku moja
cha wadau wa zao la pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga. Viongozi hao
wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya
ushirika.
“Nataka kila
mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama
mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya
kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu.
“Hawa
nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi
yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma ifikapo Januari 15, 2018 saa
3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisisitiza.
Kuhusu
tuhuma za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza
Cooperative Union - NCU), Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na
2017, kilikuwa jumla ya mali 10 ambazo ziliuzwa kinyemela katika
mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi ya mali
hizo zilizopo jijini Mwanza.
Aliwataja
viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa
ni Murtazar Alloo
ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU, Bw. Samson Ng’halida (mnunuzi
wa New Era Oil Mills), Bw. Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo), Bi.
Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la KAUMA), Bw. Timothy Kilumile (mnunuzi wa
jengo la KAUMA), Bw. Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills), Bw.
Peter Ng’hingi (aliyekuwa Mjumbe wa Bodi), Bw. Daniel Lugwisha (aliyekuwa Mhasibu
Mkuu - NCU), Bw. George Makungwi (aliyekuwa Afisa Miliki - NCU) na Bw. Sospeter
Ndoli (aliyekuwa Afisa Utumishi -NCU).
Kuhusu
mali za Nyanza zinazoshikiliwa na benki ya CRDB. Waziri Mkuu alisema benki hiyo
inaidai NCU mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 2.123 na kwamba benki hiyo
inashikilia mali 16 zenye thamani ya sh. bilioni 18.132. Alitaka vyombo vya dola
vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki
ya CRDB.
Kwa upande
wa viongozi wa SHIRECU, Waziri Mkuu alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi
ya sh. bilioni 11 ambazo wanadaiwa na benki ya TIB yakiwemo madeni ya mishahara
ya watumishi ambayo yanafikia sh. bilioni 1.2.
“SHIRECU kwa
sasa haina mali zozote kwa sababu mali zote zinashikiliwa na TIB kutokana na
mikopo,” alisema.
Aliwataja
viongozi wa SHIRECU ambao wanatakiwa kutoa maelezo yao kuwa ni Bw. Joseph
Mihangwa (Meneja Mkuu), Bw. Sillu Mbogo (Kaimu Mhasibu Mkuu), Bw. Maduhu
Nkamakazi (Kaimu Mkaguzi wa Ndani), Bw. James Kusekwa (Kaimu Meneja Uendeshaji)
na wajumbe wa Bodi ya SHIRECU.
Wajumbe
hao wa Bodi ni Bw. Robert Mayongela (Mwenyekiti), Bi. Mary Mabuga (Makamu
Mwenyekiti), Bw. Sigu Maganda (Mjumbe), Bw. Clement Bujiku (Mjumbe) na Bw. Charles
Lujiga.
Waziri Mkuu
ambaye aliwasili mkoani humo leo asubuhi, alikwenda kwanza kukagua kiwanda cha kutengeneza
nyuzi cha JOC na kisha kurejea ukumbini kuendelea na kikao cha wadau wa pamba
ambacho kimeshirikisha wakuu wa mikoa 16, wabunge, ma-RAS, wakuu wa wilaya,
wakulima, wanunuzi wa pamba na wenye viwanda.
Waziri Mkuu
ameondoka Shinyanga kuelekea Ruvuma ambako atakuwa na ziara ya siku moja.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.