*Ni baada ya
kupokea mabango ya wananchi wakidai kunyanyaswa
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa
Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha
wananchi kesho (Jumapili) saa 4 asubuhi.
“Sasa hivi
natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho saa 4 asubuhi uje hapa
Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na
kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.
Ametoa agizo
hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa
kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya
mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na
kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.
Waziri Mkuu
alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na
kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi
ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.
“Hawa ndiyo
nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo
wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee
taarifa kesho mchana,” alisisitiza.
Baada ya
kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo
na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza
lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na
la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri
Mkuu.
Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa
Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa
wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila
wanapokutana na viongozi hao.
“Tunanyanyaswa
na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna
wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini
wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.
Alidai hata Naibu
Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya
kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na
kuingizwa mgodini kisha akaondoka.
Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema
kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu
ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.
“Hapa pana
ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela;
tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,”
alisema.
Alipoitwa na
Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa
kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka
hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba
yoyote.
“Yale ya nyuma
yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa
makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa
anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki
amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.
Waziri Mkuu
anaendelea na ziara ya jimboni kwake.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.