WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi
wa dini wasibaki nyuma katika suala zima la kuwekeza kwenye viwanda ili waweze
kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifikisha Tanzania kwenye
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Serikali ya awamu ya tano imeazimia kukuza
uchumi wa viwanda. Nawaomba msiwe nyuma katika suala hili, tumieni fursa ya
ardhi tuliyonayo hasa katika ujenzi wa viwanda vya usindikaji ili kuongeza
thamani ya mazao,” amesema.
Waziri
Mkuu ametoa rai hiyo leo (Alhamisi, Julai 12, 2018) wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 52 ya Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT). Mkutano huo wa siku mbili, umehudhuriwa na maaskofu zaidi ya 80,
wenyeviti wa makanisa na wawakilishi wa vyama vishiriki.
Amesema uwepo wa viwanda hivyo utachangia
ukuaji wa sekta ya kilimo na kuongeza ukuaji wa mnyonyoro wa thamani ya mazao.
Akitoa mfano fursa zilizopo hivi sasa, Waziri Mkuu aliwaeleza Maaskofu hao
kwamba bei ya ufuta kwa mwaka huu imepanda na kufikia sh. 3,100/-
ikilinganishwa na sh. 1,400/- ambayo ilikuwa ni bei ya mwaka jana.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa
dini kwa kwa kubwa wanayofanya ya kukemea maovu kama vile ujangili, ukatili wa
kijinsia na matumizi ya dawa za kulevya.
"Serikali inaheshimu mahubiri yenu sababu
tunajua yana nguvu sana. Kupitia mahubiri yenu, watu wakimjua Mungu, watakuwa
na hofu ya Mungu, kwa hiyo watu watakuwa waadilifu na maovu mengine yatapungua," amesema.
"Nitumie fursa hii kuwajulisha kwamba
Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa wa nchi zilizosimamia vizuri mapambano dhidi ya dawa za
kulevya barani Afrika.
Kwa hiyo tumepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa wa kimataifa utakaofanyika
hapa nchini Septemba, mwaka huu."
Amesema mshikamano uliopo baina ya viongozi wa
Serikali na viongozi wa dini hauna budi kuendelea. "Natoa wito kwa Wakuu
wa Mikoa na Wilaya wajenge mshikamano wa pamoja na viongozi wa dini katika
maeneo yao husika. Viongozi wa Kitaifa nasi, tutaunga mkono katika ngazi ya
kitaifa," amesema.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na maaskofu hao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Kikristo Tanzania, Askofu Dkt. Anilikisa Cheyo alisema Jumuiya hiyo inaendelea
kusisitiza suala la umoja na mshikamano wa Kitaifa.
“Suala la umoja wa kitaifa na amani ya nchi yetu
ni masuala mtambuka; tena ni nguzo ya utaifa wetu. Tunashukuru jinsi Serikali inavyosimamia
masuala haya kwa hekima na uthabiti. Tunaahidi kuwa tutaendelea kuliombea Taifa
letu pamoja na viongozi wake ili mzidi kuilinda amani ya Taifa letu pamoja na
watu wake.”
“Hata wakati inapotokea masuala haya
yanapoguswa au kuumizwa, Kanisa limeendelea kuhimiza mara zote kutafuta
ufumbuzi wake kwa njia ya mazungumzo,” amesema.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.