*Awataka wasimamie mifumo rasmi ya ununuzi wa mazao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ofisi za
maafisa ugani zinapaswa kuwepo walipo wakulima, wafugaji na wavuvi na kwamba maafisa
ugani katika ngazi zote lazima wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu.
Waziri
Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Julai 12, 2018) wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa maafisa kilimo, mifugo na uvuvi kutoka Tanzania Bara ulioanza
leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma. Mkutano huo unahudhuriwa
na washiriki 570.
“Maafisa ugani katika ngazi zote lazima
wawezeshwe na wasimamiwe kikamilifu kutekeleza majukumu yao. Wataalam wa Wizara
washuke hadi ngazi ya mikoa na Halmashauri kusaidiana na waliopo kwenye ngazi
hizo.
“Walioko ngazi ya mkoa washuke mara kwa mara
hadi ngazi ya Halmashauri na ngazi ya Halmashauri ishuke na kushirikiana na maafisa
ugani wa kata na vijiji kuelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu utaalam na
maarifa yanayohitajika katika kuendeleza sekta hizi kibiashara,” amesema.
Amesema wakulima, wafugaji, na wavuvi hawana
budi kupatiwa mbinu bora kuanzia hatua ya uzalishaji hadi kupata masoko ikiwa
ni pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi zenye tija katika uzalishaji wa
mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Amesisitiza kwamba maafisa ugani ni lazima wawe
na orodha sahihi ya wakulima, wafugaji na wavuvi wote kuanzia ngazi ya
kitongoji na aina ya mazao wanayoshughulikia, malengo ya uzalishaji na
utekelezaji.
“Maafisa ugani wawe na takwimu sahihi za aina
na kiasi cha mahitaji ya teknolojia na
pembejeo za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo
yao lakini pia wasaidie kuunganisha vikundi vya wakulima, wafugaji, wavuvi na
kuunda ushirika imara ili kuendeleza juhudi za kufufua ushirika kama mkombozi
kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.”
“Ukiwa na ushirika imara hata kama unataka
kuwapatia taarifa ya haraka kuhusu ongezeko la bei, au tarehe ya mnada inakuwa
rahisi kwa sababu wana Mwenyekiti wao au Katibu wao na kupitia kwake, wote
wanaweza wakaitishwa na kupewa taarifa kwa haraka,” amesema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka maafisa ugani waende wakasimamie mifumo rasmi ya ununuzi
wa mazao ili kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri za mazao yao.
“Hatutaki kusikia watu wanatumia mifumo isiyo
rasmi kama chomachoma (kwenye ufuta),
butura (kahawa huko Karagwe), katakichwa (kahawa Moshi), kangomba
(korosho) na vishada (tumbaku). Nenda kapambane nao, wewe ni afisa wa Serikali
na hupaswi kuacha wananchi wanateseka,” alisema.
“Nenda kahimize mfumo wa kuuza mazo kwa
ushirika badala kuruhusu wanunuzi kwenda kwa mkulima mmojammoja. Pia mtusaidie
kufafanua dhana ya Stakabadhi za mazao Ghalani kwamba siyo malipo ya papo kwa
papo. Muwaeleze wakulima kwamba wanapeleka mazao pake wakati wakisubiria bei
iwe nzuri, siyo kwamba wanakopwa,” amesisitiza.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais – TAMISEMI, Bw. Selemani Jafo alisema Aprili mwaka huu, Serikali ilifanya
tathmini ya utekelezaji wa agizo la kuwa na viwanda 100 kwa kila mkoa na
kubaini kuwa umefikia 49.4 ndani ya miezi mitatu tu.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.