WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua fao la
Ushirika Afya ambalo linawalenga wananchi wanaojishughulisha na kilimo kupitia
ushirika.
Amezindua fao hilo jana (Jumatatu, Julai 16, 2018) kwenye
mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ulowa katika kijiji cha
Kangeme, kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Shinyanga.
Waziri Mkuu alikabidhi kadi 20 kwa niaba ya
wanachama 259 ambao wamejiunga na mpango huo. Wanachama hao wanatoka katika
vyama mbalimbali vya ushirika kwenye Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
Alisema katika kuhakikisha Watanzania wengi zaidi
wanapata huduma za afya katika hospitali yoyote ile nchini, Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, wameamua
kuzindua mpango wa Ushirika Afya, ambao unahusisha wakulima walio katika vyama
vya ushirika.
“Gharama
ya kujiunga na fao hili kwa mwaka ni sh. 75,000 kwa mtu mmoja na sh. 50,000 kwa
mtoto mmoja lakini unakuwa na uhakika
wa kutibiwa katika hospitali yoyote ile hapa nchini,” alisema.
Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania
kuna vyama vya ushirika 10,522 vyenye wanachama 2,234,000 ambapo asilimia 35 ya
wanaushirika huwa wanapata magonjwa ya dharura na wanakuwa hawana namna ya kupata
fedha kwa haraka.
“Tunatambua wote kuwa fedha ya mkulima ni ya msimu,
lakini mkulima ukiwa na kadi ya bima ya afya, utapata matibabu kokote kule hata
kama huna fedha taslimu,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza kijana
aliyebuni mpango huo ambaye anatoka Taasisi ya Ukuzaji wa Sekta ya Fedha
Tanzania (FSDT), Bw. Mwombeki Baregu. “Huyu kijana si mwajiriwa wa NHIF, wala
siyo mtumishi Serikalini, lakini kwa sababu ya uzalendo, alikuja na huu mfumo akauelezea
na kuonesha manufaa yake kwa wananchi wa kawaida, na kwa sababu Serikali yenu
ni sikivu, tukaufanyia kazi na leo ninauzindua,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema
kuna vyama vya ushirika takribani 10,000
ambavyo vina wanachama zaidi ya milioni 2.5 wanaojishughulisha na kilimo cha
mazao mbalimbali ikiwemo pamba, korosho, tumbaku, chai na kahawa.
“Lengo letu ni kuwafikia wanachama hawa pamoja na
familia zao ili kuwawezesha wapate huduma katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
siku alipochangia. Kupitia utaratibu huu, mwanachama atapata huduma za
uchunguzi na matibabu katika vituo zaidi ya 6,000 vilivyosajiliwa na mfuko wetu
nchi nzima,” alisema.
“Kupitia mpango huu wa
ushirika afya, mwanachama atapata huduma za vipimo na matibabu mpaka ngazi ya
Taifa kulingana na ushauri wa wataalam. Mfuko kwa kushirikiana na Tume ya
Maendeleo ya Ushirika, itaendelea kutoa elimu kwa wanachama wa ushirika kwa
lengo la kuongeza uelewa wa mpango huu kwa walengwa,” aliongeza.
Alisema NHIF imeufanyia
maboresho mpango huo ambapo kwa sasa wameanzisha vifurushi mbalimbali ambapo
mwanachama ataweza kuchagua kulingana na uwezo wake na ukubwa na hali ya
familia yake.
“Vifurushi
hivyo vinaanzia kwa mwanachama aliye peke yake, aliye na mwenza, aliye na
mwenza na mtoto mmoja, wawili mpaka wanne. Kwa mwanachama asiye na mwenza
lakini ana familia, mpango huu umeweka utaratibu wake,” alifafanua.
Akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu, Spika Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya NHIF, Mama Anne Makinda alisema uzinduzi uliofanyika jana
umewakilisha kuzinduliwa kwa fao hilo kwenye mikoa yote nchini.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.