Thursday, June 27, 2019

MIFUKO YA UWEZESHAJI IPIMWE KWA MATOKEO YA KIUCHUMI-MAJALIWA


*Asema uboreshwaji wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ni muhimu

SUALA la uwezeshaji wananchi kiuchumi ni jambo muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani, kwa kuwa litawatawezesha kutambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi na hatimaye wataweza kujitegemea na kuondokana na umasikini wa kipato.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo ya Serikali na ya sekta binafsi ambayo inaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

NEEC imekuwa ikiandaa makongamano ya kukutanisha wadau wa masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004, ambapo pia hutoa fursa muhimu ya kupeana taarifa mbalimbali za uwezeshaji.

Kongamano la Nne la Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika Juni mwaka huu katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma ambalo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alieleza umuhimu wa uboreshwaji wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile, kamilisheni na hakikisheni mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya uwezeshaji kwa matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya.”

Alisema uwezeshaji wananchi kiuchumi ni suala mtambuka, sekta mbalimbali za kiuchumi na sekta binafsi zinajihusisha moja kwa moja katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo ni muhimu sana masuala ya uratibu, ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yakafanywa mara kwa mara ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendelee kuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015 - 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

Mbali na agizo hilo, pia Waziri Mkuu alilitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuratibu mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo ya Serikali na ile ya binafsi ili kujua ipo mingapi na inamnufaisha nani na kisha wampelekee taarifa. 

Alisema ni muhimu ikajulikana idadi ya mifuko hiyo ili kujua ipo maeneo gani na namna inavyoendeshwa na kama kweli walengwa wananufaika kwa kiwango gani na je wanajijua, hivyo italiwezesha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuiratibu vizuri.

Alisema Serikali inatambua kuwa kuwawezesha wananchi kiuchumi ni hatua ya msingi katika kujenga Taifa lililoimarika kiuchumi na lenye lengo la kujitegemea hususan katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. 

“Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuhakikisha kuwa fursa ya mikopo kwa ajili ya mitaji inapatikana bila ya urasimu na kwa masharti nafuu ikiwa ni pamoja na kuwafikia wananchi wengi mijini na vijijini.”

Alisema katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa, Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu sambamba na kubuni shughuli za kuwawezesha wananchi katika maeneo yao kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 pamoja na Sheria yake. 

Waziri Mkuu aliongeza kuwa, kwa upande wa sekta binafsi, serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara ili kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. 

Alisema mfano mzuri wa utekelezaji wa jambo hilo ni maboresho ya sheria na mifumo mbalimbali ili kuboresha mazingira kwa sekta binafsi kufanya biashara ikiwemo pamoja na kutekeleza Blue Print. 

“Nyote mtakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Rais ameipa uzito wa kipekee sekta binafsi, miongoni mwa hatua alizozichukua ni kuhakikisha kuwa masuala ya uwekezaji yanakuwa chini ya ofisi ya waziri mkuu ili kushughulikia wawekezaji ambao kwa sehemu kubwa ni sekta binafsi. kadhalika, mifumo ya kodi na tozo mbalimbali imeangaliwa sambamba na sera na sheria husika.”

Pia Waziri Mkuu alizitaka mamlaka husika za serikali zihakikishe zinashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla ili sera, mipango na shughuli zao za kila siku zitoe kipaumbele katika uwezeshaji wananchi kiuchumi. 

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuitaka mikoa na halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama kile cha Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi. 

Waziri Mkuu alitoa muda wa mwaka mmojakwa viongozi wa mikoa ya Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ambayo haijakamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji (Investment Guide) ihakikishe kuwa inakamilisha.

Kadhalika, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu matokeo ya tafiti zilizofanywa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu biashara na uwekezaji nchini kuwa yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya miradi mikubwa inayopendekezwa na shirika hilo.

“Miradi hiyo ni pamoja na ule wa “Harmonized Innovation Solutions for Local Economic Development” ambao upo katika hatua za maandalizi. Lengo la UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi inatekelezwa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.” 

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuziagiza mamlaka zote zishirikiane na NEEC kuhakikisha kuwa fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti za UNDP zinafanyiwa kazi. “Aidha, hakikisheni kuwa miradi mikubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inatokana na tafiti hizo.” 

Alisema ana imani kubwa kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, malengo mbalimbali ya nchi kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi yatafikiwa. Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa ya Miaka 25; na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya umoja wa Mataifa (SDGs).

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, SeraUratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema lengo la mkutano ni kuwakutanisha wadau wote wanaotekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.

Alisema kupitia mkutano huo wanapata mrejesho wa yaliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kujadili, kupima mafanikio, kuona changamoto zilizopo na kujiwekea malengo na mikakati ya kufanya vizuri zaidi kwa mwaka unafuata. 

Waziri huyo alisema katika kukutanisha wadau wa uwezeshaji, Ofisi yao imeanza kutengeneza National Economic Empowerment FrameWorkitakayoelekeza vipaumbelele vya kitaifa vya kisekta kutokana na shughuli za uchumi zilizopo.

Awali,Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’ Issa alisema jukumu la baraza hilo ni kuratibu, kuongoza, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini.

Alisema baraza hilo limeendelea kufuatilia na kutathmini shughuli za mifuko ya uwezeshaji, kiwango cha huduma kwa wananchi na matokeo ya uwezashaji unaotolewa kwa wananchi.

“Hadi kufikia februari mwaka huu mifuko inayotoa mikopo moja kwa moja kwa kushirikiana na ile inayotoa dhamana imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 3.1 kwa wajasiriamali 5,031,219.”

Alisema mifuko inayotoa ruzuku na programu za uwezeshaji zimesaidia kuwezesha kiasi cha zaidi ya sh. trilioni 12 kwa wananchi pamja na kufadhili miradi mbalimbali ya kijamii nchini.

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.