*Ihakikishe huduma zake zinawafikia wananchi wa mijini na vijijini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta
ya fedha inapaswa kuwa imara na kuhakikisha huduma zake zinawafikia
wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini ili iweze kutoa
mchango unaokusudiwa katika kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Juni 24, 2019) wakati alipofungua Ofisi Ndogo na
Tawi la Benki ya Biashara ya TIB jijini Dodoma. Amesema ukuaji wa sekta ya huduma za kifedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Waziri
Mkuu amesema benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha
kwa wananchi, hivyo, benki zinatakiwa kuzingatia mahitaji ya wananchi,
kuwahamasisha na kuwaelimisha umuhimu wa kutumia benki.
“Wananchi
nao pia wana wajibu wa kuzitumia benki hizi kwa kutunza akiba zao na
kukopa wakati wanapohitaji kuwekeza kwa malengo yaliyokusudiwa. Suala la
msingi ni kuwa mnapokopa mkumbuke pia kurejesha kulingana na
makubaliano.”
“Sifurahishwi
sana na takwimu zinazoonesha kwamba ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania
wote ndiyo wanaopata huduma za kifedha kupitia mifumo halali ya kibenki,
huku asilimia 48.6 wakipata huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu
na asilimia 35 ya waliosalia kutopata kabisa huduma rasmi za kibenki.”
Waziri
amesema hali hiyo haikubaliki kwenye nchi kama Tanzania ambayo
inakabiliana na ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo
ametoa wito kuwa benki zote ziendelee kubuni mikakati na mbinu
zitakazowawezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki
tena kwa gharama nafuu ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua
kutoka kwenye umaskini.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema tozo za mabenki kwa wateja bado ni kubwa na
haziwasaidii wananchi wa kawaida, kwa hiyo, zipunguzwe. “Riba kwa
wakopaji nazo ziko juu sana ukilinganisha na mfumuko wa bei, pia nazo
zipunguzwe.”
Kuhusu
changamoto ya riba kubwa inayotozwa kwa mikopo ya benki, Mheshimiwa
Majaliwa amesema tayari Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania
imefanikiwa kupunguza riba ya hati fungani za Serikali, pamoja na ile
inayotozwa kwa mabenki yanayokopa Benki Kuu. Moja ya lengo la kufanya
hivyo ni kutaka riba za mabenki zipungue.
“Naomba
mabenki yaunge mkono jitihada hizo za Serikali kwa kupunguza riba
zinazotozwa hasa kwenye mikopo ya watu binafsi na biashara ndogo ndogo
kwani hawa wakipata unafuu wataweza kukuza biashara zao na hivyo
kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji.”
Akizungumzia
suala la baadhi ya benki kuwa na tawi moja au mawili jijini
Dar-es-Salaam tu, Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshaiagiza Benki
Kuu ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuzitathimini upya
benki za aina hiyo.
“Leo
narudia tena kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuzisimamia benki zetu ili
zifungue matawi yake hadi vijijini waliko wenye uhitaji.! Kwanini? benki
nyingi zimejikita katika kutafuta faida pekee bila kuwekeza kwa faida
ya nchi yetu? Hadi sasa tuna benki ambazo zimekuwa siku zote na tawi
moja tu tena liko Dar-es-Salaam. Benki Kuu ya Tanzania isisite kuchukua
hatua za kisheria kurekebisha hali hiyo.”
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya TIB, Frank Nyabundege
amesema kwa kipindi cha miaka minne benki hiyo imeweza kukuza mtaji
kutoka sh. bilioni 206 wakati inagawanywa mwaka 2015 mpaka kufikia sh.
bilioni 409 mwishoni mwa mwaka 2018 sawa na ukuajia wa aslimia 98.5.
Mkurugenzi
huyo amesema mbali na kufanikiwa katika kukuza mtaji, pia benki hiyo
imeweza kukuza amana za wateja kutoka sh. bilioni 110 mwaka 2015 mpaka
sh. bilioni 338 mwezi Disemba 2018, sawa na ukuaji wa asilimia 207.
“Mafanikio mengine yabenki
ya TIB katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na kuanza kutengeza
faida angalau ya sh. bilioni 1.3 mwaka jana (2018), kutoa mchango
stahiki katika Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha sh. milioni 250.”
Mkurugenzi
huyo ameongeza kuwa benki hiyo imetoa mikopo na dhamana kwa taasisi za
umma hadi kufikia shilingi bilioni 224.35 kwa kipindi kilichoishia Machi
2019, kulipa kodi Serikalini kiasi cha sh. bilioni 19.2 tangu benki
ianzishwe na kutoa mikopo kwenye sekta ya viwanda jumla ya sh. bilioni
65.12.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.