WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali zote mbili (Jamhuri ya Muugano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) zinatambua mchango wa sekta
isiyo rasmi, hivyo zimekuwa zikifanya juhudi mbalimbali kuendeleza na
kuongeza tija katika sekta hiyo.
Amesema
katika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea, Serikali imeendelea kuweka
mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwa wajasiriamali wa Tanzania
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuwapatia vyeti vya
uasili ambavyo vimetoa unafuu mkubwa wa kodi na tozo.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Novemba 24, 2019)wakati akifunga
Maonesho ya Wajasiriamali wa Tanzania kusherehekea miaka 20 ya
uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Fumba,
Zanzibar.
Amesema
wanapohitimisha maonesho hayo sambamba na kusherehekea miaka 20 tangu
kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatakiwa wajitathmini kuona
kama wametimiza malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
“Vilevile,
tuendeleze ujirani mwema, kupanua na kuimarisha ushirikiano wa watu wa
Afrika Mashariki ili kuharakisha ukuaji wa kiuchumi sanjari na kuboresha
maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki kiuchumi, kisiasa na kijamii.”
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuzungumzia kuhusu vikwazo visivyo vya
kiforodha vinavyozorotesha wajasiriamali kufanya biashara katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki, ambapo amesema vimeendelea kutatuliwa kupitia
majadiliano baina ya Tanzania na nyingine ndani ya Jumuiya hiyo kwa
lengo la kuvipunguza na kuviondoa kabisa.
Waziri Mkuu amesema kupitia majadiliano hayo, Serikali imefanikiwa kur atibu zoezi la uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 15kati ya 24vilivyoripotiwamwaka 2019 navikwazo tisa vilivyobakiahatua ya kuvipatia ufumbuzi inaendelea.
Hata hivyo,Waziri Mkuu amesema Serikali
imeendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha
wajasiriamali wanachangamkia fursa za kibiashara zitokanazo na Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Waziri
Mkuu amesema mkakati huo unahusisha zoezi la kufanya utafiti wa uelewa
wa Watanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na matokeo ya utafiti
huo yatatumika katika kutoa elimu kwa umma kulingana na mahitaji.
Katika
kutatua changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali, Waziri Mkuu amesema
Serikali inatekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka
2015/2020 ya kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha
vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali.
Amesema
miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kusimamia utekelezaji wa
maelekezo ya Serikali kwa taasisi za fedha na mifuko mbalimbali ya umma
na binafsi kutoa mikopo kwa wajasiliamali kwa riba nafuu na ikiwezekana
isiyo na riba.
“Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Juni, 2019 mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 42.06 kwa vikundi11,487 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ilitolewa. Vilevile, mikopo hiyo inayotokana na asilimia
10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri imeendelea kuzingatia uwiano wa
asilimia nne kwa vikundi vya wanawake, asilimia nne kwa vijana na
asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.”
Pia,
Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha uundwaji wa vikundi vya
wajasiriamali, kusimamia utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi
hivyo sambamba na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuwezesha
wajasiriamali na wawekezaji wengine kufanya shughuli zao bila bughudha.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imeanzisha mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi
kwa lengo la kutoa mitaji na huduma nyingine za kifedha zenye masharti
nafuu kwa wananchi wa Unguja na Pemba. Mfuko huu umelenga wananchi wenye
kipato kidogo ili waweze kuzalisha mali kwa kujiajiri na kupunguza
umaskini.
Amesema
hadi kufikia Juni 2019 kupitia mfuko huo mikopo yenye thamani ya sh.
bilioni 3.5 ilikuwa imetolewa na kuzifikia jumla ya Shehia 346. “Mfuko
huu kupitia mradi wa mbogamboga na matunda umetoa mikopo 263 kwa
wakulima wa mbogamboga na matunda 384 wa Pemba yenye thamani ya sh.
milioni 60.6 na wakulima 384 wa Unguja yenye thamani ya sh. milioni
151.3.
Amesema
Serikali imeendelea kufanya maonesho mbalimbali ya Wajasiriamali wa
Sekta isiyo rasmi ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Maonesho
hayo yametoa fursa kwa wajasiriamali kupata ujuzi, taarifa za masoko,
teknolojia, mbinu na taratibu mbalimbali za kufanya biashara ili kukuza
shughuli zao.
Maonesho
hayo yamewapatia wajasiriamali uthubutu wa kushiriki wao binafsi katika
maonesho mengine kwenye nchi za Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Sudan
Kusini, Msumbiji na Marekani. Pia wameweza kufanya ziara katika nchi ya
China ambako walijifunza na kununua mashine za kisasa kwa ajili ya
kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la
ndani na nje.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.