Monday, November 18, 2019

WAZIRI MKUU AMTAKA MTENDAJI MKUU TBA AJITATHMINI


 *AWASIMAMISHA KAZI WAKURUGENZI WATATU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake huku akiwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa wakala huo.

“TBA tunaihitaji lakini watu wake wana shida. Hatuwezi kuwaacha, TBA wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo.”

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi wakurugenzi hao leo (Jumatatu, Novemba 18, 2019) wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) eneo la Njedengwa jijini Dodoma.

Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi, Arch.Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi, Abdallah Awadh na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri Arch. Hamis Kileo.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali ukiwemo ujenzi wa jengo la NEC ambalo ujenzi wake ulianza Julai, 2017 na ulitakiwa ukamilike Juni 2018 kwa gharama ya sh. bilioni 13. Hata hivyo mradi huo bado haujakamilika na ujenzi wake umesimama.

Akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa ofisi ya NEC Waziri Mkuu alihoji sababu za mradi huo kutokamilika kwa wakati ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi alisema jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa sababu wakati walipokuwa wanaanza kazi walibaini kuwa kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji wa Bill of Quantities(BOQ). TBA ndio waandaaji wa ramani ya jengo hilo na ndio wajenzi.

“Bajeti ya awali ilikuwa sh. bilioni 10 wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi gharama ziliongezeka na kufikia sh. bilioni 13 ambazo ndizo tulikubaliana katika mkataba. Wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna vitu vimesahaulika kwenye BOQ jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na kufikia sh. bilioni 32.” Amesema Arch. Killo.

Waziri Mkuu akahoji tena “kutoka sh. bilioni 13 hadi kufikia sh. bilioni 32 je unaona inakuja vizuri hiyo” sh. bilioni 10 hadi sh. bilioni 13 tena hadi sh. bilioni 32 inazungumzikaje hii na je mwenye jengo mlikubaliana naye? Awali mwenye mahitaji alisema ana sh. bilioni 10 sasa imefikaje 32 je mlimshauri muhusika kuhusu ongezeko hili?

Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi Arch. Killo alipotakiwa kueleza sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo amesema waligundua tofauti wakati wakiwa kwenye eneo la ujenzi kwamba kuna kazi zilitakiwa zifanyike lakini katika mkataba hazipo na hawakuwasiliana na muhusika.

Miongoni mwa vitu vilivyosahaulika katika BOQ ya mradi huo ni pamoja na kutokuwepo kwa ghorofa ya nne katika jengo moja wanalolijenga katika mradi huo ambalo ni la ghorofa nane, pia hapakuwa na paa la jengo la kuhifadhia vifaa mbalimbali vya NEC.

Waziri Mkuu amesema miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali imeshindwa kukamilika kwa wakati, hivyo amemwagiza Waziri wa NchiOfisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine aje amalizie.

“Jengo la TAMISEMI lililopo katika mji wa Serikali limejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 1.7, nyie wataalamu gani na kwa nini tuendelee kuwaacha ndani ya taasisi? TBA hamfanyi kazi vizuri wakuu wa mikoa na wilaya wanalalamika majengo hayakamiliki ni Serikali gani itakayowavumilia, mmeshindwa kutambua majukumu yenu.”

Waziri Mkuu ameagiza mkandarasi atakayepatikana ahakikishe mradi wa ujenzi huo unakamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa na lijengwe kwa kutumia mfumo wa force account. 


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.