Tuesday, September 5, 2017

FANYENI TATHMINI YA ZAO LA KOROSHO – WAZIRI MKUU


*Apiga marufuku biashara ya kangomba, makato ya unyaufu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania zifanye tathimini ya maandalizi ya msimu ujao kwa wakati na zimpatie taarifa mara moja.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana usiku (Jumanne, Septemba 5, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma kujadili mwenendo wa zao la korosho na ununuzi wa pembejeo.

“Lipo tatizo la tathmini ya maandalizi ya msimu kutofanyika kwa wakati na kusababisha matatizo kutotatuliwa kwa wakati. Bodi na Wizara zitoe tathimini ya maandalizi ya msimu ujao kuhusu vyama vya ushirika vilivyojipanga, upatikanaji wa vifaa kama magunia na nyuzi, maghala, masoko, mizani, minada, malipo na mfumo wake,” alisema.

Waziri Mkuu pia alizitaka Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Korosho zitoe tathimini ya maandalizi ya msimu ujao katika maeneo ya mashamba, miche, pembejeo na viatilifu. 

Alisema tangu Serikali iamue kusimamia mazao makuu matano ya pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku hajapata muda wa kukaa na kuongea na wadau wote. “Serikali imeamua kufuatilia usimamizi wa mashamba; kusimamia upatikanaji wa mbegu, miche na pembejeo; kufuatilia uvunaji na mfumo wa masoko ya korosho na pia kufuatilia mfumo wa ushirika katika baadhi ya mazao,” alisema.

Alisema hivi sasa zao la korosho linalimwa katika wilaya 50 kwenye mikoa 11 ya Dodoma, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro na Mtwara. Mingine ni Njombe, Pwani, Ruvuma, Singida na Tanga. 

“Katika msimu wa mwaka 2016/2017 zao la korosho lilikuwa ni moja kati ya mazao ya kibiashara yenye tija na faida nyingi kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani milioni 346.6,” alisema na kuongeza kuwa katika msimu wa mwaka 2017/2018 watendaji hawana budi kujipanga vizuri ili zao la hilo liendelee kuliingizia Taifa dola nyingi zaidi kwa kuwa Serikali imetoa viatilifu bure.  

“Ninasisitiza eneo hili kwa sababu tumebaini kuwa korosho inachangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato kwenye Halmashauri zinazolima kwa wingi zao hilo. Kwa kuwa zao hili ni la kimkakati, naitaka Wizara inipatie taarifa sahihi na kwa wakati,” alisisitiza.

Alisema Agosti mwaka huu, alipofanya ziara mkoani Tabora, alielezwa kwamba wilaya ya Uyui na Tabora Manispaa zimeanza kulima zao hili kama zao mbadala ili kuinua uchumi wa wananchi wake. “Tabora itakuwa mkoa wa 12, kwa hiyo Wizara ya Kilimo itembelee maeneo haya na kuona inawezaje kuwasaidia, ikaangalie uzalishaji ukoje kwani mti unaweza kukubali kuota pale Tabora lakini usizae kwa wingi kama ilivyo kwa mikoa mingine,” aliongeza.

“Viongozi wa juu Serikalini hadi kwa mtendaji wa kijiji ni lazima tusimamie zao la korosho, kila mtendaji ashirikiane na taasisi ambata, wizara mama iimarishe vyuo vya kilimo na utafiti. Kila mtendaji ni lazima ajue na wakulima wangapi, je kila mkulima ana ekari ngapi na kila ekari ina miche mingapi,” aliongeza.

Ili kurekebisha dosari zilizojitokeza katika msimu uliopita na kuboresha utendaji katika msimu ujao, Waziri Mkuu alisema Wizara na Bodi zinapaswa kufanya tathmini ya uhakika kwa kushirikiana na ofisi za mikoa. 

“Tumepata matatizo ya msimu kutoanza kwa wakati kwa sababu ya kukosekana kwa tathmini za nyuma, hatuna pa kuanzia kufanya marekebisho kwa sababu hatuna uzoefu wa yaliyojiri kwenye msimu uliotangulia. Siyo Bodi, Wizara wala Ofisi ya Mrajisi ambayo imekwishafanya tathmini. Kazi zote zimeacha kwa Wakuu wa Mikoa kupitia Sekretarieti za Mikoa.”

Akielezea kuhusu mwenendo wa biashara ya zao hilo, Waziri Mkuu alisema ili wakulima waweze kuwanufaika zaidi, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa malipo wa stakabadhi ghalani na kupambana na watu wasio waaminifu wanaotumia kangomba. Kangomba ni kopo linalotumiwa na wanunuzi binafsi ambalo ujazo wake haufikii hata kilo moja, lakini wao wanalitumia kama kipimo cha kilo moja kununulia korosho kwa wakulima.

“Kuanzia sasa, biashara ya kangomba ni marufuku, kangomba ni wizi na yeyote atakayekamatwa, achukuliwe hatua za kisheria. Kila mkoa uweke mkakati makini wa kudhibiti biashara ya kangomba,” aliagiza.

“Hatutaki kusikia biashara ya kangomba. Viongozi wa Serikali msiwatumie vijana kwa kuwapa mitaji ili wafanye biashara hii. Mkizikamata korosho za kangomba, piga mnada na fedha ziende kwenye chama cha ushirika cha pale zilipokamatwa,” alisema.

Kuhusu makato ya unyaufu (shrinkage), Waziri Mkuu alisema kuanzia sasa, vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na Chama Kikuu haviruhusiwi kutoza hela ya unyaufu kwa wakulima.

“Sheria ya unyaufu inasema utauza korosho kwa asilimia 0.5 ya bei halisi ya korosho iliyokaa kwa zaidi ya miezi sita. Sasa hapa kwetu msimu wa kuuza ni Oktoba hadi Desemba, unyaufu hapo unatoka wapi? Hili haliwahusu wakulima wetu kabisa,” alisema.

Alisema suala la unyaufu litawahusu wanunuzi ambao watakuwa wamenunua korosho na kuzihifadhi kwenye maghala kwa muda mrefu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi OR- TAMISEMI, Bw. George Simbachawene; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha; Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule; Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Mama Anna Abdallah; Warajis Wasaidizi wa Mikoa; Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi wa Maghala na Mizani, Wajumbe wa Bodi ya Korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi, na Mameneja wa Vyama Vikuu.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.