Thursday, September 21, 2017

WATUMISHI WA MIPAKANI DHIBITINI UINGIZWAJI WA SILAHA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi  katika mipaka mbalimbali nchini ukiwemo wa Namanga mkoani Arusha kuhakikisha wanachunguza kwa umakini mizigo yote inayoingia ili kudhibiti  uingizwaji wa silaha na dawa za kulevya nchini.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Septemba 21, 2017) alipotembelea kituo cha Pamoja cha Forodha cha Namanga wilayani Longido kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya na kisha kuzungumza na wafanyabiashara ndogo ndogo.

Waziri Mkuu amesema ni vema watumishi wa vituo vya forodha katika maeneo ya mipaka wakawa makini kwa kuhakikisha wanadhibiti uingizwaji wa silaha pamoja na dawa za kulevya nchini kwa sababu ndiyo zinazotumika katika matukio ya kihalifu.

Pia Waziri Mkuu ameziagiza mamlaka mbalimbali zinazosimamia ubora wa bidhaa kwenye vituo vote vya Forodha nchini kuhakikisha wanachunguza bidhaa zote na kujiridhisha ubora wake kabla ya kuruhusu kuingizwa nchini na kutumika.

“Tusingependa nchi yetu kuwa eneo au shimbo la kutupia bidhaa zisizokuwa na ubora Wizara zote zinazohusika na udhibiti wa ubora wa bidhaa zihakikishe suala la ukaguzi wa viwango vya ubora wa bidhaa zote zinazoingia nchini linapewa kipaumbele.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Longido, Bw. Daniel Chongolo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Juma Mhina kukutana na wananchi wanaofanya biashara ndogo ndogo katika eneo hilo pamoja na viongozi wa  TRA na kuwatafutia eneo lingine kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

Amesema kwa kuwa wananchi hao awali walikuwa wanafanya biashara zao ndani ya eneo hilo kabla ya kujengwa kituo hicho cha Pamoja cha Forodha, ambapo kwasasa hawaruhusiwi kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tanzania na Kenya kuhusu uendeshaji wa kituo hicho hivyo ni vema wakawatafutia eneo jingine nje ya uzio wa kituo hicho.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.