Saturday, September 2, 2017

FUATILIENI MAENDELEO YA VIWANDA KATIKA MAENEO YETU-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika mikoa yote nchini kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya viwanda mbalimbali katika maeneo yao.

Amesema mpango wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuinua uchumi wa Taifa kutoka wa chini kwenda wa kati, hivyo ni muhimu kuvifuatilia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017) alipozungumza na watendaji na wananchi wa mkoa wa Morogoro alipofanya ziara katika kiwanda cha Moproco.

Alisema licha ya kukuza uchumi wa Taifa, viwanda vitasaidia katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana kwani vinauwezo wa kuajiri watu wengi.

“Viwanda hivi vinatupa uhakika wa ajira nchini kwa sababu vinauwezo wa kuajiri watu wengi na wa kada mbalimbali, hivyo ni muhimu tukafuatilia utendaji wake.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa mbali na kutoa ajira nyingi, pia viwanda vitawezesha wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kukifanya kilimo kuwa na tija.

Alisema kwa muda mrefu sekta ya viwanda nchini ilikuwa haifanyi vizuri jambo ambalo lilisababisha kuongezeka kwa tatizo la ajira na mazao yalikosa soko.

Hata hivyo Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafanyakazi walioajiriwa katika viwanda mbalimbali kuwa waaminifu ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea na uzalishaji.

Pia aliwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ili kuviwezesha viwanda kuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi ndani ya chini.

Awali Meneja Mkuu wa kiwanda cha Moproco, Bw. Arif Abood aliiomba Serikali kuongeza kodi kwa mafuta yanayotoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani.

Alisema uingizwaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa kiasi kukubwa ulichangia kufungwa kwa viwanda vya ndani vya mafuta kutokana na kukosa soko.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage pamoja na maofisa wengine wa Serikali. 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.