CHANGAMOTO ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
wilayani Longido mkoani Arusha kuwa historia baada ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani
ya sh. bilioni 15.8.
Waziri Mkuu ameweka jiwe hilo la msingi leo (Alhamisi, Septemba
21, 2017) kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Longido Mjini pamoja na kijiji cha
Oltepesi ambao chanzo chake ni kutoka mto Simba wilaya ya Hai mkoani
Kilimanajro.
Amesema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata
huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye
makazi yao.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Gerson Lwenge kupeleta wataalamu wilayani Longido ambao watashirikiana
na Halmashuri za wilaya ya Longido na tarafa ya Loliondo kutafuta
vyanzo vingine vya maji ili wananchi waweze kupata maji ya kutosha.
Waziri Mkuu amesema asilimia kubwa ya wananchi wa wilaya za
Longido na Ngorongoro ni wafungaji hivyo wanahitaji maji mengi watakayoyatumia
katika matumizi yao ya kawaida ya nyumbani pamoja na kunyweshea migugo.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza mradi
huo pamoja na miradi mingine midogo tisa katika wilaya ya Longido kutumia vifaa
vinavyotengenezwa na viwanda vya ndani ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Awamu ya Tano kukuza uchumi kupitia viwanda.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema wananchi
wanatakiwa wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za
kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya
mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wawachukulie
hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo,
ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa
zinasababisha ukame.
Awali Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Lwenge aliwaagiza
Wakandarasi wanaojenga mradi huo kuhakikisha wanajenga kwa kuzingatia viwango
vya ubora vinavyohitajika pamoja na kumaliza kwa wakati. Mradi huo unatarajiwa
kukamilika Julai, 2018.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.