Friday, June 8, 2018

PPRA YAENDESHA MAFUNZO YA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA KWA WATUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Augustino Tendwa akiongoza mkutano wa Mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na mabadiliko yake 2016 yaliyoandaliwa na Kitengo cha manunuzi cha Ofisi hiyo yaliyoanza kuanzia tarehe Juni 6 hadi 9 Juni, 2018 katika Ukumbi wa Mikutano LAPF Dodoma.

NA MWANDISHI WETU:
Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeendesha mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma  ya mwaka 2011 na mabadiliko yake ya mwaka 2016 kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuleta tija na uelewa zaidi kwa watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa sheria za manunuzi kwa watumishi wa Ofisi hiyo ambayo yanafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 6 hadi 9 Juni, 2018 katika Ukumbi wa Mikutano wa LAPF Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Metrida Kaijage alieleza kuwa mafunzo hayo ya siku nne yanalenga kuongeza uelewa kwa Watendaji wa Ofisi hiyo ili kuhakikisha Sheria na Kanuni mbalimbali za manunuzi zinafundishwa ili kuendana na mabadiliko yanayojitokeza.
“Mafunzo haya ya Masuala ya manunuzi yachukuliwe kama chachu kwani waliofadhiri wameona yana tija ya kutupitisha katika sheria hizi za manunuzi ili watumishi wote tufanye kazi kwa kuzingatia sheria, miongozo na kanuni zilizopo”,alisisitiza Kaijage.
Naye Afisa Ugavi Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Benjamin Mdadi alieleza kuwa, uwepo wa mafunzo hayo utasaidia kuongeza uweledi katika kutekeleza kazi za kila siku hususan katika sheria mbalimbali za manunuzi pamoja na kanuni zake.
“Mafunzo haya yatatusaidia hasa katika kutekeleza majukumu yetu hususan haya ya manunuzi ya umma, kwani kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya sheria za manunuzi, mfano sheria ya mwaka 2016 na kanuni zake”,alisema Mdadi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Ofisi hiyo Bw.Augustino Tendwa aliwapongeza wawezeshaji kutoka PPRA kwa kushirikiana na Mradi wa Mpango wa Kuboresha Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) ambao wamefadhili shughuli zote za uendeshaji mafunzo kwa watumishi wa Ofisi hiyo na kuwataka kuyaweka katika vitendo yale watayofundishwa na si vinginevyo.

 “Kimsingi mafunzo ni mazuri na niwapongeze wafadhili wetu Mradi wa SAGCOT kwa kuona umuhimu wa kusaidia uendeshaji wa mafunzo na niwaombe watumishi wenzangu tuyafanyie kazi mambo yote tutayofundishwa yawe katika vitendo”,alisisitiza Tendwa


Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma yaliyoratibiwa na Kitengo cha Manunuzi cha Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Mradi wa Mpango wa Kuboresha Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) Jijini Dodoma

Sehemu  ya washiriki wa mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma yaliyoratibiwa na Kitengo cha Manunuzi cha Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Mradi wa SAGCOT Jijini Dodoma

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Metrida Kaijage akieleza jambo kwa wajumbe wa mafunzo ya Sheria ya manunuzi ya Umma (hawapo pichani) yaliyoratibiwa na Kitengo hicho kwa kushirikiana na PPRA kwa ufadhili wa Mradi wa Mpango wa Kuboresha Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT)

Mwenyekiti wa Mafunzo hayo Bw.Nisetas Kanje akizungumza na wajumbe walioshiriki mafunzo ya manunuzi ya Umma (hawapo pichani) yaliyoratibiwa na Kitengo cha Manunuzi Ofisi ya Waziri Mkuu yanayoendelea mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Bunge na Siasa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Yona Mwakilembe akichangia hoja wakati wa Mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma yanayoendeshwa na PPRA kwa kushirikiana na Kitengo cha Manunuzi cha Ofisi hiyo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.