WANUNUZI
wa zao la pamba wameishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi
wa zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada
inayosimamiwa na Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS).
Hata
hivyo wanunuzi hao wameiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala
makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha
pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.
Kauli
hiyo imetolewa jana (Jumanne, Juni 12, 2018) na mmoja wa wanunuzi hao
ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment LTD, Bw. Emmanuel
Dandu alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa uchambuaji wa pamba kwa
msimu wa mwaka huu.
Alisema
awali kabla pamba haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora
lilikuwa halizingatiwi sana na wakulima kwani pamba yake ikikataliwa na
kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine na,
jambo ambalo lilichangia kuisha thamani.
Hata
hivyo ameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili
waweze kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa
wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze
kujiunga.
Bw.
Dandu ambaye kampuni yao ya NGS Investment LTD, licha ya
kujishughulisha na biashara nyingine, pia inamiliki kiwanda cha
kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,
ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji pamba.
Alisema
pamba inayochambuliwa katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS
walizopangiwa, ambapo alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha
kupata malighafi kwa urahisi na kwa wakati.
“Wanunuzi
wote tunanunua pamba kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri
unaotuweza wote kununua pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa
kuuza pamba kwa wanunuzi wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya
nyuma” alisema.
Akizungumzia
kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, alisema kina uwezo wa kuchambua tani
40,000 za pamba kwa mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani
tano hadi 12 kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha
pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika.
Pia
aliiomba Serikali iwasaidie wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati
pamoja na kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni
bora za kilimo cha zao la pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati
ili waweze kujiongezea tija.
Alisema
kwa sasa kiwanda hicho kina jumla ya wafanyakazi 300, ambao kati yao 62
ni wa waajiriwa wa kudumu na waliosalia ni vibarua.
Bw.
Dandu alisema marobota yanayotengenezwa kiwandani hapo yanakuwa na
uzito wa kilo 200 hadi 220, huku wateja wao wakubwa ni Cotton
Distributors Inc (CDI) ya nchini Uswisi, Saurashtra Cotton and Agro
Product PVT LTD ya nchini India.
Wengine
ni Awatac Impex PTE LTD ya nchini Singapore pamoja na viwanda vya nguo
vya ndani ya nchi kikiwemo cha Mwatex cha jijini Mwanza. Alisema
matarajio ya kampuni hiyo ni kuanzisha kiwanda cha kutengeza nyuzi ili
kuongezea thamani ya pamba kabla ya kuiuza.
Aidha,
Meneja huyo alisema mbegu zinazopatikana baada ya pamba hiyo
kuchambuliwa pamba zinapelekwa moja kwa moja katika kiwanda cha kukamua
mafuta ya kula na mashudu huuzwa kama chakula ya mifugo.
Kuhusu
mabaki yanayopatikana baada ya mafuta kuchujwa, alisema yanatumia kwa
kutengeneza sabuni za kufulia, ambazo wanaziuza kwa wananchi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.