WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa
ya Kongamano la Uchumi la Dunia la mwaka 2018 inaonesha kuwa Tanzania
inaongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi miongoni mwa nchi za Afrika zilizo
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema
hali hiyo, imetokana na Tanzania kufungua fursa za ujasiriamali ambapo
kuna zaidi ya biashara milioni tatu zinazokuwepo kila mwaka, lengo la nchi ni kuhakikisha kuwa uchumi unakua na unamgusa kila Mtanzania hususan mwananchi wa kawaida.
Waziri Mkuu ameyasena hayo leo (Jumatatu, Juni 18, 2018) wakati akifunguaKongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF, jijini dodoma.
“Pia,
huduma za fedha jumuishi ni kigezo ambacho kimeiweka Tanzania mahala
pazuri kwenye uchumi jumuishi ambapo zaidi ya Watanzania milioni 30
wamekuwa wakifanya miamala mbalimbali ya fedha kupitia simu za mkononi
na hivyo kuongeza huduma za fedha kufikia asilimia 65,” amesema.
Amesema
huduma za msingi za kijamii kama vile elimu, afya na kupungua kwa
rushwa katika utoaji huduma za umma pamoja namtandao wa miundombinu ya
barabara ambayo huwezesha wananchi wengi kujishughulisha na shughuli za
kiuchumi ni kigezo kingine kilichozingatiwa katika kuipatia Tanzania
nafasi hiyo.
Waziri
Mkuu ameongeza kwamba Serikali inaamini kuwa uchumi wa viwanda
ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na matokeo yake yataonekana
wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za
kiuchumi.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema suala la uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025 ni moja ya ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya
Tano, hivyo amezitaka sekta zote zihakikishe zinatoa mchango mkubwa
kwenye uchumi wa viwanda.
Pia
amesema suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi lazima liende sambamba na
uwezeshaji vijana kujiajiri kama inavyoelekeza Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. “Ilani inatambua kwamba kuwawezesha
wananchi kiuchumi ni hatua ya msingi katika kujenga Taifa lililoimarika
kiuchumi na lenye lengo la kujitegemea,”.
Aidha,
Ilani pia, inasisitiza kuhusu umuhimu wa kuhamasisha ushiriki wa Sekta
binafsi katika kuwezesha wananchi kiuchumi, hivyo ni muhimu kukamilisha
taarifa ya uwezeshaji kutoka kwa wadau wa sekta binafsi, ili Serikali
iweze kuona mchango wa sekta binafsi katika kuwawezesha wananchi
kiuchumi.
Waziri
Mkuu amesema utekelezaji wa malengo hayo ya uwezeshaji wananchi katika
maeneo ya fursa za mafunzo ya ujasiriamali na mikopo ya masharti nafuu
ni muhimu sana katika kupambana na umaskini wa kipato.
Amesema
kwa kutambua umuhimu wa ajenda ya uchumi wa viwanda, ndiyo maana
makongamano ya uwezeshaji yamekuwa yakiweka mkazo kwenye masuala ya
viwanda. Hali hiyo pia, inajidhihirisha katika kaulimbiu ya Kongamano la
Tatu ambayo ni: “Viwanda: Nguzo ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi”.
Hivyo
Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema, “tuendelee kuhimiza kuhusu kutekeleza
uchumi wa viwanda kwa lengo la kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi na
kuhakikisha kuwa tunafikia lengo la kuwa na uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025,”.
Kongamano
hilo lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
(NEEC) limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa
Kilimo Dkt Charles Tizeba, Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw.
Charles Mwijage na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo.
Wengine ni Wakuu wa Mikoa mbalimbali, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu
wa Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, Makatibu Tawala wa Mikoa, Mwenyekiti na
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,Wakurugenzi
wa Halmashauri za Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’
Issa, wadhamini wa Kongamano hilo na Wawakilishi kutoka katika taasisi
mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.