WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Afisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa
anayeshughulikia elimu ya msingi, Bw. Selemani Mrope atafute walimu
wawili kutoka Ruangwa na kuwahamishia kata ya Nanganga mara moja.
"Lazima
kuna walimu wamejazana pale Ruangwa mjini, leo tukitoka hapa nenda
kaandike barua za uhamisho. Kesho Jumapili, wahusika wapewe barua zao na
Jumatatu waje kuripoti hapa Nanganga," amesema Waziri Mkuu na kuamsha
shangwe miongoni mwa wakazi wa Nanganga.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Julai 27, 2019) wakati akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Nanganga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi alipopita
kuwasalimia wakazi hao.
Waziri
Mkuu ambaye amewasili Lindi leo kwa mapumziko mafupi, alipokea taarifa
ya shule ya msingi Nanganga ambayo ilionesha kuwa shule hiyo yenye
wanafunzi 237 ina walimu sita tu. Kati ya hao, wavulana ni 124 na
wasichana ni 113.
“Shule
hii ina madarasa nane likiwemo darasa la awali, masomo yanayofundishwa
ni tisa, mkibaki na walimu hawa sita, mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu
hawa waliopo. Afisa Elimu tafuta wawili walimu waje hapa Jumatatu, na
Mkurugenzi wa Halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia hapa,” amesema.
Shule ya msingi Nanganga, iliyoko kata ya Nanganga, iko umbali wa km. 59
kutoka Ruangwa mjini.
Waziri
Mkuu ambaye ni mbunge wa Ruangwa, amewataka wakazi wa kata hiyo
wafikirie kuanza ujenzi wa shule ya sekondari yao ya kata ili
kuwapunguzia safari wanafunzi wa kijiji hicho ambao kwa sasa
wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko umbali wa km. 10.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa sh.
milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo yakikamilika
walimu watapata ofisi pia.
Amesisitiza kwamba fedha hizo zitumike kujenga madarasa manne ambapo walimu pia watapata ofisi moja.
Pia
amemwambia diwani wa kata ya Chinongwe, Bibi Maki Camillius kwamba
katika bajeti ya mwaka huu, kata hiyo itapatiwa sh. milioni 100 kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba nne za walimu katika shule ya sekondari ya
kata ya Chinongwe.
Mapema, akisoma
taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Amiri
Musa Kambona alisema madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka
mwaka 2014 kutokana na mvua na upepo mkali na kusababisha upungufu wa
madarsa na ofisi.
Akielezea
changamoto nyingnea za shule hiyo, Mwalimu Kambona alisema shule ina
upungufu wa nyumba moja ya walimu, darasa moja, matundu mawili ya vyoo
vya walimu, ofisi moja ya walimu na kukosekana kwa chanzo cha maji safi
na salama kwa matumizi ya wanafunzi na walimu.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.