*Ni za ujenzi wa
kituo cha kimataifa cha mabasi cha Moshi
*RPC athibitisha watu
watano wamekamatwa kufuatia agizo hilo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Hamisi Issah awasake na kuwatia mbaroni watu waliohusika na wizi
wa tani tano za nondo na kisha wakatoroka.
Alitoa agizo hilo jana jioni, (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza
na wafanyakazi na wananchi mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi
ya kimataifa ya Moshi, katika kata ya Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi za siku
nne, alisema mradi huo ni maalum kwani uko miongoni mwa miradi ambayo Serikali imekuwa
ikiweka utaratibu wa kupelekea fedha kwenye miradi iliyotengwa na Halmashauri.
“Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9 za kuanzia mradi huu
lakini inasikitisha kuona kwamba wanaMoshi mnahujumu kwa kuiba vifaa vya
ujenzi. Ninazo taaarifa kuwa hapa zimeibiwa tani tano za nondo na zimeshakamatwa.”
“Ni aibu, ni aibu kwa wana-Moshi. Ninyi wenyewe mnauhujumu huu mradi. Manispaa
iweke utaratibu wa ulinzi ili vifaa vingine visipotee zaidi. Mkuu wa Wilaya
chukua hatua ya kuwafuatilia wote waliohusika,” alisema.
Kupitia maswali aliyouliza, Waziri Mkuu alibaini kuwa walinzi wawili
waliokuwepo siku ya tukio walitoroka ndipo akaamua kumwagiza Kamanda wa Polisi
Mkoa, awasake na kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Ujenzi wa stendi hiyo kubwa unafanywa na mkandarasi mkuu ambayo ni kampuni
ya CRJE ya China akishirikiana na wakandarasi wasaidizi watano na unatarajiwa
kukamilika Januari 2021. Hadi kukamilika, ujenzi huo unatarajiwa kugharimu sh.
bilioni 28.8.
Ikikamilika, stendi hiyo ambayo itakuwa na ofisi, maduka, migahawa na
hoteli, itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 300 kwa siku ambayo yataingia na
kutoka. Kati ya hayo, mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja. Pia
kutakuwa na maegesho ya ya magari binafsi 218, teksi 34 na bajaji na bodaboda
20.
Wakati huohuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah
amethibitisha kukamatwa kwa watu watano ambao wanatuhumiwa kuhusika na wizi wa
tani tano za nondo katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo lililopo Ngangamfumuni.
“Hawa watu tumewakamata jana jioni, na kati ya walinzi waliotoroka,
tumemkamata mmoja wao tayari akiwemo mkazi wa Rau, Daudi Audifasi mwenye miaka
48 ambaye anadaiwa kutoboa ukuta wa uzio kwa chini, na kukutwa na nondo nyumbani
kwake ambako ni mita 10 kutoka eneo la tukio.”
Amesema tukio hilo, lilitokea Julai 6, mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi
ambapo walinzi wa eneo hilo ambao ni Maxshield company walitoroka baada ya
tukio hilo. Kamanda Issah alithibitisha kwamba nondo hizo zimekamatwa na ziko
polisi.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.